- Binadamu, Usindikaji

Jifunze kutengeneza keki ya asili ya ndizi na kuongeza pato

Sambaza chapisho hili

Ndizi ni zao la chakula maarufu sana katika mikoa mbalimbali hapa nchini kama vile Kilimanjaro, Arusha, Bukoba na sehemu zingine.

Mbali na chakula zao hili pia limepata umaarufu sana katika ulaji kama matunda lakini pia uzalishaji wa kaukau (crips) pamoja na unga.

Aidha matumizi ya zao hii yamezidi kuongezeka na hhata sasa kuweza kutumika kutengeneza keki.

Keki ya ndizi

Hii ni aina ya keki ambayo malighafi yake kuu ni ndizi mbivu ambazo wingi wake kwenye keki hulingana na kiwango cha keki kinachopaswa kutengenezwa kama vile nusu kilo, kilo moja au hata zaidi.

Malighafi ya kutengeneza keki ya ndizi (nusu kilo)

  • Ndizi mbivu kubwa 4 zilizoiva vizuri (Hasa zile zilizokwisha kuanza kuweka madoti kwenye ganda).
  • Mayai ya kienyeji 2
  • Mafuta yam aji/siagi au blueband robo
  • Iliki ya unga kijiko 1 cha chai
  • Mdalasini kijiko 1 cha chai
  • Baking powder vijiko 2 vya chai.
  • Bicarbonate of soda robo kijiko cha chai.
  • Unga wa ngano robo na nusu ya robo.

Vifaa

  • Bakuli kubwa la kuchanganyia malighafi.
  • Chuma maalumu cha kuponda au mwiko.
  • Vifaa vya kupima malighafi kama vile kijiko cha chai, kijiko cha chakula na kikombe cha ujazo cha robo, sinia, kifaa cha kuokea.

Namna ya kutengeneza keki ya ndizi

Hatua ya kwanza

Katika hatua ndipo ambapo viambaupishi au malighafi hupimwa na kuchanganywa kwa kiwango sahihi

  • Osha ndizi zako kwa maji safi na salama, kisha menya na weka kwenye bakuli kwaajili ya kuchanganyia.
  • Chukua kifaa cha kuponda au mwiko kisha ponda ndizi mpaka upate rojo unayohitaji. Unaweza ukaponda hadi kuwa kama uji, ama ukaponda kupata rojo zito au ukavunjavunja ndizi kwa kiwango fulani upendacho wewe au mteja wako.
  • Safisha mayai kwa maji safi na salama kisha vunja na changanya kwenye ndizi kisha endelea kukoroga mpaka kuhakikisha yamechanganyika vyema.
  • Chukua unga wa ngano, ongeza bicarbonate na baking powder kisha anza kuchuja kwa kutumia chujio ili kuupata unga mlaini na kuweza kuchanganya malighafi. Kuchuja pia husaidia kuondoa uchafu kama utakuwa umeingia kwenye unga.
  • Baada ya kuchuja ongeza iliki na mdalasini kisha changanya na weka pembeni.
  • Chukua mafuta/siagi vijiko 2 vya chakula kwenye rojo la ndizi kisha koroga vizuri kuhakikisha mafuta yameyeyuka na kuchanganyika.
  • Chukua mchanganyiko wa unga na viungo kisha anza kuweka kidogokidogo kwenye bakuli lenye rojo ya ndizi huku ukiendelea kukoroga hadi uchanganyike vyema.

Hatua ya pili

Katika hatua hii ndipo tunapoenda kutafuta umbo la keki, hii tutatumia chombo cha kuokea chenye umbo unalolipenda, mfano mraba, duara n.k

  • Baada ya kutengeneza mchanganyiko wa kutengeneza keki, Chukua chombo cha kuokea keki kisha paka mafuta/siagi kidogo kusunguka chombo chote.
  • Chukua unga kidogo sana na nyunyizia kwenye chombo hicho juu ya mafuta uliyopaka. Hii inasaidia keki isishike kwenye chombo mara baada ya kuoka.
  • Baada ya kuweka unga, mimina mchanganyiko wako kwenye chombo tayari kwa kuoka.

Hatua ya tatu

Katika hatua hii ndipo keki yetu inapopikwa/okwa tayari kwa ajili ya matumizi. Unaweza kuoka kwa kutumia mkaa, au oven ya jiko la umeme/gesi.

  • Kwa kutumia ovena, washa jiko lako ili kupata moto kabla ya kuweka keki ili kuoka.
  • Jiko likishapata moto weka keki yako na hakikisha kwenye nyuzi joto za sentigredi C° 170 na muda wa dakika 45. Hii itasaidia keki kuiva vizuri na kutokuungua

Hatua ya nne

Angalia kama keki imekwisha kuiva baada ya dakika 45, na hii utaelewa kwa kutumia kisu, utachoma katikati ya keki, kikitoka kisafi keki iko tayari, kikinata au kutoka na mchanganyiko wa keki basi keki haijaiva rudisha tena kuoka.

  • Baada ya keki kuiva utachukua tayari kwa kupamba kwa kadri upendavyo.
  • Unaweza kupamba kwa kutumia mapambo ya kisasa au kutumia vitu vya asili.
  • Baada ya kupamba keki yetu iko tayari kutumika au kupeleka sokoni.

MUHIMU: Keki hii haijawekwa sukari kwani ndizi tayari zina sukari yake ya asili ila kama unapenda sukari zaidi unaweza kuongeza. Pia waweza kuongeza harufu kama vile ya vanilla na nyingine nah ii utaweka wakati wa kumalizia kuchanganya malighafi.

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *