- Mifugo, Samaki

Je, unayafahamu haya kwenye ufugaji wa Samaki?

Sambaza chapisho hili

Wakulima wengi hasa wanaotumia maji ya bomba wangependa kuanza ufugaji wa samaki lakini huenda kuna mambo kadha wa kadha hawafahamu kuhusu ufugaji kwa kutumia maji ya bomba.

Aidha, mambo ni mengi ya kuzingatia ili kuanza ufugaji wa samaki lakini tuanze kujibu maswali haya kutoka kwa mkulima anayetaka kufanya ufugaji huu.

Husein Mshegia anauliza: Natarajia kufuga samaki kwa kutumia maji ya kuingiza kwenye bwawa kwa kutumia pampu. Napaswa kuyabadilisha kila baada ya muda gani? Na, bwawa la kufugia samaki 50,000 liwe na ukubwa gani?

Jibu: Kufuga samaki kwa kutumia maji ya kuingiza kwenye bwawa kwa kutumia pampu siyo vibaya. Hii inaruhusiwa, kikubwa ni kuzingatia maji unayoingiza kwenye bwawa chanzo chake kiwe ni salama na maji yaliyo safi na salama.

Ni vyema kama unavuta maji kwenye chanzo hicho kuhakikisha unaweka kifaa cha kuchujia maji yasiweze kuingiza uchafu au vijidudu visivyohitajika ndani ya bwawa.

Wadudu hawa wanaweza kuwa hatarishi kwa samaki. Hakikisha maji unayo ingiza kwenye bwawa yanakuwa na kina kisichopungua mita moja na kisicho zidi mita moja na nusu.

Ukiweka maji yenye kina cha chini ya mita moja ni hatari kwa samaki kupata joto kali jambo ambalo hupunguza kiwango cha hewa ya oksijeni, na kusababisha samaki kufa au kudhofika katika ukuaji wake.

Ni wakati gani maji yabadilishwe?

Maji kwenye bwawa mara nyingi huwa hatusemi unabadilisha baada ya muda gani kwa sababu mtaalamu anaweza akakuambia unabadilisha maji kila baada ya miezi miwili, halafu ikatokea yale maji ndani ya mwezi mmoja yakawa yamechafuka.

Badilisha maji kutegemea aina ya ufugaji wa samaki na mfugaji anashauriwa kufanya upimaji wa maji angalau mara moja kwa wiki au mwezi ili mabadiliko yanapotokea unaweza kuchukua hatua muda wowote siyo lazima maji yachafuke yote ndio ubadilishe.

Njia za kubadili maji

Kuna njia ya kupunguza maji na kuongeza maji pindi hali ya ukijani ndani ya bwawa inapokuwa imezidi.

Kwa kufanya hivi, maji yatakuwa salama. Zoezi hili unaweza kulifanya mara moja kwa mwezi au zaidi kutegemea na hali ya ukijani imeongezeka kiasi gani.

Mambo ambayo mfugaji inabidi aangalie kama vile hali ya harufu mbaya kwenye maji, joto na hali ya ukijani au tope kwenye bwawa, na pia kama mfugaji anaweza kumudu kununua vifaa vya kupimia kiwango cha hewa kwenye maji, asidi na besi.

Endapo vitu hivyo vitajitokeza kwenye bwawa inabidi upunguze majina uongeze maji safi. Kumwaga maji yote kwenye bwawa hutegemea na kiwango cha uchafukaji.

Mambo ya kuepuka

Mfugaji anaweza kuepuka vitu ambavyo huchafua maji kwenye bwawa kama vile

  • Kulisha chakula kingi
  • Aina ya chakula kisichofaa
  • Kutotoa uchafu na vitu vinavyoelea au kuonekana kwenye bwawa kama vile takataka na samaki waliokufa. Hali hii inapelekea kuchafuka kwa maji.

Ukubwa wa bwawa la kuweka samaki elfu hamsini

Ukubwa wa bwawa hutegemeana aina ya ufugaji.

  1. Mfugaji mdogo: Hii ni aina ya ufugaji ambao kiwango chake cha uwekezaji sio mkubwa na usio gharama kubwa sana, na hupandikizwa samaki 1-3 kwa mita moja ya mraba. Kiwango cha maji kubadilishwa sio wa mara kwa mara, huenda ikachukua hata miezi 3.

Chakula chake huwa ni cha asili, sio lazima ulishie kila siku na utunzaji wake sio mkubwa sana. Mavuno yake huwa ni madogo. Njia hii hutumiwa na watu wa kiwango cha chini kiuchumi.

Mfano, mita moja ya mraba unaweka samaki 3, hivyo, unahitaji mita za mraba 16,666.666 kwa Samaki 50,000.

  1. Mfugaji wa kati: Huu ni ufugaji wa kati ambapo kiwango chake cha uwekezaji ni kuanzia samaki 4-10 kwa mita za mraba. Hii ikitegemeana na upatikanaji wa maji, chakula na matunzo mengineyo huwa ni wastani.

Pia mavuno yake huwa ni ya wastani ambayo huridhisha. Kwa wafugaji wenye kiwango cha kati kiuchumi hutumia zaidi njia hii. Mfano, mita moja ya mraba unaweka samaki 5, hivyo unahitaji mita za mraba 10,000 kupandikiza samaki 50,000, ambazo ni sawa na upana wa (mita 100 kwa 100).

  1. Mfugaji mkubwa: Huu ni ufugaji mkubwa. Kiwango chake cha uwekaji huwa ni kikubwa kuanzia samaki 10 na kuendelea kwa mita moja za mraba.

Katika nchi zilizoendelea, kutokana na vifaa vya kutosha, hupandikiza samaki mpaka 200 au zaidi kwa mita za mraba. Hii huhitaji maji yanayozunguka au kubadilishwa mara kwa mara, mashine za kuongeza hewa, chakula cha uhakika na uangalizi wa hali ya juu.

Katika nchi yetu, bado hatujafanikiwa kutekeleza aina hii ya ufugaji kwa sababu uwekezaji wake ni mkubwa ingawa mavuno yake ni makubwa pia.

Mfano, unapandikiza samaki 10 kwa mita za mraba. Hivyo, unahitajika uwe na mita za mraba 5,000 kupandikiza samaki 50,000. Ambazo ni sawa na upana wa (mita 50 kwa mita 100).

Kwa njia zote hizo za ufugaji, mahitaji muhimu ni bwawa la uhakika lisilopitisha maji, liwe na njia za kutolea na kuingiza maji.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *