- Mifugo

Fuga mbuzi uongeze kipato mbadala

Sambaza chapisho hili

Mbuzi ni mnyama mdogo lakini mwenye faida kadha wa kadha na huweza kutunzwa eneo na kwa gharama ndogo.

Kwa jamii nyingi za kiafrika, mbuzi kama kuku, ni moja ya mnyama anayefugwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Katika jamii nyinginezo, hufuga mbuzi kwa ajili ya kitoweo, maziwa na pia kuwatumia katika katika sherehe na shughuli mbalimbali za kitamaduni.

Hivi sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa ambapo wafugaji wamekuwa wakifanya hivyo ikiwa ni sehemu moja wapo ya shughuli zao za kujiongezea kipato, pamoja na kupata maziwa na lishe kwa ajili ya familia zao. Mara nyingi ufugaji wa mbuzi hufanywa pamoja na ufugaji mwingine  kama wa ng’ombe au uzalishaji wa mimea tofauti.

Mnyama huyu ni mdogo lakini mwenye faida kadha wa kadha, huweza kutunzwa kwa gharama ndogo sana kwa kuwa malisho yake hutegemeana na mazingira alipo mfugaji na pia hutumia muda mwingi kujitafutia malisho.

Ili kuwa na mbuzi bora na wanaofanya vizuri katika uzalishaji, chagua mbuzi chotara wanaoweza kuzalisha nyama na maziwa. Mbuzi aina hii ukuwa kwa haraka.

Ili kupata ufanisi zingatia mambo machache yafuatayo;

Malisho

Unaweza kuwalisha mbuzi kwa kutumia miti malisho, aina tofauti za nyasi, matete, nafaka na pumba inayotokana na miti malisho pamoja na nafaka. Pia ni vizuri kuwapa mbuzi uhuru wa kujitafutia malisho kwenye miti iliyo karibu na eneo lako. Kumbuka; kamwe usiwape mbuzi nafaka zilizo oza.

Uhuru wa mazoezi na kucheza

Mbuzi wadogo wanakuwana uwezo wa kucheza na kuruka ruka katika kipindi cha siku mbili toka kuzaliwa. Wanaonesha utofauti wa maeneo ya kuchezea kwa kuruka vitu vinavyowazunguka.

Hii ni hatua muhimu katika ukuaji wao, ni vizuri mbuzi wakaachiwa kuruka ruka huku na kule na kucheza kuimarisha afya. Endapo wataachiwa huru ni wazi kuwa wanakuwa na furaha na ni wazi watakuwa vizuri. Mazoezi yatafanya mifupa na misuli kukomaa vizuri.

Malazi

Ni muhimu ukawafuga mbuzi kwenye banda lililonyanyuliwa juu. Banda lililonyanyuka juu linaruhusu kinyesi cha mbuzi kudondoka chini. Nafasi za kupitisha kinyesi ni lazima ziwe ndogo sana ili kuepuka miguu ya mbuzi kutumbukia. Ni muhimu kufanya hivyo ili kuepuka mbuzi kuumia miguu. Sababu ya kuweka sakafu ya banda la mbuzi kuwa juu ni ili kuzuia mbuzi asilale mahali palipolowana. Hii inaepusha mbuzi kukohoa na kutia maziwa doa pamoja na kuwakinga wasishambuliwe na wadudu kama vile viroboto, kupe na siafu.

Chanjo

Ni jambo muhimu na la busara kuwapatia mbuzi chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali. Chanjo dhidi ya ugonjwa wa miguu na mdomo ni lazima, hasa katika eneo ambalo kuna mifugo wengi waliowekwa katika eneo moja.

Dawa ya minyoo

Ni muhimu kuwapa mbuzi dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu au minne. Inashauriwa kutofautisha tiba ya aina nyingine na ya minyoo ili kuepuka madhara yanayoweza kutokana na aina moja wapo ya dawa. Ni vizuri mbuzi wakapatiwa dawa ya minyoo walau mara moja kwa mwaka inayotibu homa ya mbuzi na kukosa hamu ya kula, na walau mara moja kwa mwaka dawa inayotibu minyoo ya mapafu.

Ukishawapatia mbuzi wako mahitaji hayo muhimu na mengine ya ziada kama utakavyoona ama kushauriana na wataalamu wa mifugo basi ni hakika kuwa utaweza kuwa na mifugo bora na yenye tija, kwa kuwa mbuzi wana uwezo wa kuzaliana mara mbili kwa mwaka.

Fuga kwa malengo

Jambo lolote linapofanyika kwa nia na kwa umakini hufanikiwa na kuwa na tija. Wafugaji walio wengi wenye mafanikio siku za leo hawakuanzia kwenye mafanikio hayo, bali walianza katika hali ya chini kabisa, lakini kutokana na kuwa na malengo leo hii wana mafanikio makubwa.

Anza pole pole

Inashauri mfugaji kuanza na mbuzi wachache na kuendelea kupanua ufugaji huko akijenga uzoefu wa kulisha na kuwatunza mbuzi hawa. Cha muhimu ni kutumia beberu wa hali ya juu ili kuendeleza ubora wa mbuzi na uzalishaji wao. Uza au chinja mbuzi wanaoonekana wenye mwili ndogo, wanaokua pole pole au wenye uzalishaji wa chini.

Changamoto kubwa kwa wafugaji wa mbuzi huwa kujifunza namna ya kutibu mbuzi kwa njia za kiasili. Usumbufu wa magonjwa pia huwa tatizo kwani mkulima asipojua ni ugonjwa gani umewashambulia mbuzi basi kuto matibabu mwafaka inakuwa ngumu. Hivyo, inashauri mfugaji kuwa karibu na afisa wa mifugo katika eneo lake.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *