- Mifugo, Usindikaji

Sindika maziwa kupata jibini na kuongeza pato

Sambaza chapisho hili

Jibini ni zao linalotengenezwa kwa kutumia maziwa. Zao hili hupatikana kwa kugandisha maziwa kwa kutumia rennet na kimea na baadaye kuondoa sehemu ya maji baada ya maziwa kuganda.

Jibini inaweza kutengenezwa kuwa laini, ngumu kiasi au ngumu kabisa. Ili kutengeneza jibini, ni lazima kuwa na malighafi mbalimbali zitazoweza kutumika.

Mahitaji

  • Maziwa yenye mafuta yasiyozidi asilimia 3
  • Kimea
  • Rennet
  • Mashine ya kuengua mafuta ya maziwa (milk separator)
  • Kifyatulio (cheese mould)
  • Kipima joto
  • Chumvi
  • Vyombo vya kuchemshia mfano sufuria
  • Kitambaa cheupe kisafi au chujio lisilopata kutu
  • Kitambaa cheupe safi (cheese cloth)
  • Visu
  • Vyombo vya kuhifadhia maji ya chumvi (Brine)
  • Kabati la kuivishia jibini
  • Chumba maalumu chenye ubaridi na unyevunyevu
  • Vifungashio

Hatua za utengenezaji

Hatua za utengenezaji wa jibini hutegemea aina ya jibini inayokusudiwa kutengenezwa.

Jibini laini

Jibini laini ina asilimia 75 ya maji, hii ni nyeupe. Asili yake ni bara la Amerika ya Kusini

Namna ya kutengeneza

  • Chukua maziwa mabichi yenye asilimia 3 ya mafuta
  • Chuja maziwa kwa kitambaa safi cheupe
  • Chemsha maziwa hadi nyuzi joto 82C
  • Chukua maji ya limao asilimia 3 ya maziwa uliyonayo, weka kwenye maziwa na ukikoroga kwa dakika 3 ili mgando (curd) utokee.
  • Ipua, acha mgando upoe kwa dakika 15 ukiwa umefunika
  • Chuja kwa kitambaa kuondoa maji ya maziwa (whey) na kubakiza jibini.
  • Koroga jibini huku ukiongeza chumvi asilimia 3 au kutegemea na hitaji la soko.
  • Weka jibini kwenye kifyatulio (cheese mould) ukitanguliza kitambaa, kisha weka uzito ili kugandamiza whey itoke yote. Muda wa kugandamiza hutegemea uzito uliowekwa.
  • Ondoa jibini kwenye kifyatulio na kitambaa
  • Fungasha tayari kwa matumizi
  • Hifadhi kwenye jokofu
  • Muda wa matumizi usizidi wiki nne (4) baada ya kutengeneza.

Matumizi

  • Jibini hii hutumika kama chakula hivyo ni sehemu ya mlo.
  • Hutumika kutengenezea sandwich na katika mapishi mbalimbali.

 

Jibini ngumu kiasi

Aina hii ya jibini ni kama vile Mozzarella, pastafilata na scamoza ambayo asili yake ni Italy, hii ni maalumu kwa ajili ya mapishi mfano pizza.

Hatua za utengenezaji

  • Pima ubora wa maziwa.
  • Tumia maziwa yenye mafuta asilimia 3 hadi 5.
  • Pasha moto maziwa kufikia nyuzi joto 35C.
  • Weka kimea cha yogoti (thermophilic) asilimia 2 ya maziwa yanayotumika.
  • Koroga ili kimea kichanganyike vizuri na maziwa, kisha funika.
  • Acha maziwa yatulie kwa dakika 15.
  • Weka rennet mililita 300 katika lita 100 za maziwa kisha koroga na vundika maziwa kwa dakika 30 hadi 45 ili mgando utokee.
  • Kata mgando kwa kisu kisafi kupata vipande ukubwa wa sentimita moja.
  • Koroga taratibu huku ukiendelea kukatakata
  • Pasha moto mchanganyiko wa whey na curd kufikia nyuzi joto 42 hadi 45C
  • Acha maziwa yatulie kwa saa moja na nusu hadi tatu
  • Jaribisha utayari wa curd kwa kuzamisha kiasi kidogo cha curd kwenye maji yanayochemka na kuviringisha kwa vidole, kama inaweza kutengeneza uzi mrefu kiasi cha mita moja bila kukatika basi itakuwa tayari.
  • Pima kiasi cha curd weka ndani ya maji koto, kanda curd hadi ilainike, tengeneza umbo la duara.
  • Weka kwenye kifyatulio kwa dakika 10 hadi 15.
  • Poza jibini kwenye maji ya baridi kwa saa moja.
  • Weka jibini kwenye maji yenye chumvi asilimia 15 ya maji yatakayotumika. Jibini ndogo kwa saa 4 na jibini kubwa kwa saa 8 hadi 12
  • Ondoa jibini kwenye maji ya chu-mvi, kausha kwa kitambaa kisafi na weka kwenye shelfu kwa siku 14 hadi 21 ili ikomae
  • Katika kipindi hicho jibini ioshwe kwa maji ya chumvi na kugeuzwa kila baada ya sik mbili.
  • Baada ya hapo hifadhi kwenye jokofu
  • Pima uzito wa jibini kisha fungasha tayari kwa soko
  • Andika tarehe ya kutengeneza na ya mwisho wa matumizi
  • Muda wa matumizi usizidi miezi 12 baada ya kutengenez

Matumizi

  • Hutumika kwa mapishi ya vyakula mbalimbali mfano pizza.
  • Pia hutumika kama kitafunwa.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *