- Binadamu, Kilimo, Mifugo

Mbolea hai na madawa ya asili ni muhimu kwa mimea, wanyama na binadamu

Sambaza chapisho hili

Mkulima anapotumia mbolea za viwandani na kemikali kwa muda mrefu, ni dhahiri kuwa udongo hudhoofika na kushindwa kuzalisha. Afya yake pia ipo mashakani kwa kuwa kemikali zina madhara makubwa sana.

Kilimo ni lazima kuwezesha na kuongeza afya ya udongo, mimea, wanyama na binadamu. Udongo ni nguzo muhimu katika maisha ya viumbe wote kwa ujumla.

Udongo ulioharibiwa hauwezi kuzalisha chakula vizuri, na hakutakuwa na malisho ya kutosha kwa ajili ya mifugo. Ili kuweza kupata chakula cha kutosha kwa ajili ya binadamu na malisho kwa wanyama, ni lazima kuboresha rutuba katika udongo. Afya ya binadamu na wanyama inaunganishwa moja kwa moja kwenye umuhimu na uwezo wa udongo kuzalisha.

Tumia mbolea ya asili kukuzia mimea

Kuna faida nyingi zinazotokana na matumizi ya mbolea za asili kama mboji na nyinginezo. Mbole asili hutokana na kuoza kwa vitu vyenye uhai kama vile majani, miti na mabaki ya vyakula.

Vitu hivi vinapooza hugeuka na kutengeneza virutubisho ambavyo husaidia kurutubisha udongo na kupunguza gharama kwa mkulima kwa kuwa vitu vinavvyotumika ni vya asili. Mbolea ya kukuzia mimea inatokana na tope chujio, au mbolea hai inayotokana na kinyesi cha ng’ombe.

Namna ya kutengeneza

Mbolea hii hutengenezwa kwa kuchanganya kinyesi na kiasi cha maji ili kuweza kunyunyiza kwenye mimea na kutoa matokeo ya haraka kwa muda mfupi.

Mahitaji

Ndoo ya lita 40, kiroba (mfuko), mti, maji, na mbolea hai.

Kutengeneza

  • Weka maji robo tatu ya ujazo wa juu kwenye ndoo
  • Weka mbolea hai kwenye mfuko ukiwa umeutumbukiza kwenye maji hayo, huku ukiwa umeshikilia kwenye mti uliokatiza juu ya ndoo.
  • Funga baada ya maji kujaa kwenye ndoo
  • Acha kwa muda wa siku 3, kasha zungusha taratibu ili kukamua
  • Rudia zoezi hilo kila baada ya siku 3
  • Acha kwa muda wa siku 14, hapo mbolea maji yako itakuwa tayari kwa ajili ya kunyunyizia kwenye mimea yako ili kuikuza

Matumizi

  • Tumia gramu 100 kwa kila mche (unaweza kutumia kikopo cha mafuta kupima).
  • Unapoweka mara moja, mboga zitastawi vizuri mpaka wakati wa kuvuna bila kurudia tena.

Mbolea hii ya maji inafaa tu endapo unatumia mbolea mboji kwenye shamba lako. Baada ya siku 14 usitumie tena mbolea hii kwani baada ya hapo itabadilika na kuwa dawa badala ya mbolea.

 Kuthibiti magonjwa na wadudu

Madawa ya asili

Hizi ni dawa zinazotokana na mimea ambayo hupatikana katika maeneo ya wakulima. Matumizi ya dawa hizi ni njia mojawapo ya kuepuka dawa za viwandani ambazo huathiri udongo, mazingira na afya za watu na wanyama.

Hadi sasa kuna dawa takribani 67. Madawa yasipotengenezwa vizuri na kutumiwa ipasavyo yanaweza yasifanye kazi ipasavyo, hivyo huwa ni vigumu kuwashawishi wakulima kuzitumia. Inashauriwa kutumia dawa hizi kama kinga kabla mashambulizi hayajashamiri kwani zinafanya kazi taratibu, hivyo ni vizuri kuzitumia kama kinga kuliko tiba.

Sifa za dawa za asili

  • Upatikanaji wake uwe rahisi na isiwe na ushindani wa virutubisho na mazao.
  • Iwe rahisi kutengeneza na isiyohitaji maandalizi ya kiteknolojia na isichukue muda mrefu kutengeneza.
  • Matokeo yenye kuonekana. Mara nyingi dawa hizi hufukuza wadudu zaidi kuliko kuua.
  • Unafuu wa gharama. Dawa hizi hupatikana bure ila utayarishaji wa dawa hizi lazima upimwe. Kulingana na gharama zitakazojitokeza kulingana na mgongano wa mazingira yakilinganishwa na madawa yaliyokwisha tengenezwa la sivyo wakulima wataendelea kutumia sumu. Uwezo wa kuua wadudu walengwa tu bila kudhuru viumbe hai marafiki.

Zifuatazo ni baadhi ya dawa za asili na jinsi ya kutengeneza

  1. Majivu
  • Weka majivu moja kwa moja kwenye mashina ya mimea michanga baada ya kuotesha ili kuzuia wadudu wakatao mimea kama vile sota (Cutworms).
  • Majivu yataonyesha matokeo mazuri endapo yatachanganywa na mafuta ya taa kidogo.
  1. Pilipili kali
  • Chukua gramu 55 za pilipili kisha katakata
  • Chemsha kwa dakika ishirini kwenye maji lita 5.
  • Chuja kisha ongeza maji lita 5.
  • Dawa hii huua wadudu wenye ngozi ngumu (mbawa kavu) na laini mfano vidukari, wadudu wa kabeji na kadhalika.
  1. Vitunguu saumu
  • Hutumika kwa kufukuzia wadudu kutokana na harufu yake.
  • Chukua gramu 100 za vitunguu kasha vitwange.
  • Changanya na maji lita 2.
  • Chuja kisha nyunyizia kwenye mimea.
  • Pia dawa hii inaweza kuchanganywa na mojawapo ya dawa za asili ili kutoa harufu kali itakayofukuza wadudu.
  1. Tumbaku
  • Tumia ugoro au chemsha sigara miche 20. Dawa hii hutumika kuzuia wadudu wanaoshambulia mahindi shambani (maize stalk borer), wadudu wanaokata miche, kupe, vidukari, viwavi na kadhalika.
  • Chukua gramu 500 za tumbaku.
  • Changanya maji lita 8 na chemsha.
  • Chuja baada ya kupoa kisha ongeza tena maji lita 8 na gramu 60 za sabuni ili kuongeza ubora.

Tumbaku ni sumu kwa binadamu na wanyama hivyo weka mbali na wanyama wafugwao. Inashauriwa kuvuna mazao siku 4-5 baada ya kunyunyizia dawa hii.

  1. Mwarobaini
  • Mwarobaini ni mti unaostahimili ukame, unatoa kivuli na pia umeonekana kuwa na manufaa makubwa kama tiba kwa binadamu na mafuta yake hutengeneza sabuni.
  • Kati ya dawa zote za asili, mwarobaini umeth ibitika kufanya vizuri zaidi kutokana na uwezo wake maradufu
  • Mwarobaini unaonyesha matokeo mazuri kuliko baadhi ya dawa za viwandani

Matumizi ya Mwarobaini

Kutengeneza dawa kutokana na mbegu

  • Twanga mbegu kiasi zilizokomaa na kukaushwa ili kupata unga
  • Changanya na maji lita 1.
  • Nyunyizia bustani kuzuia wadudu.

Au

  • Lainisha mbegu gramu 500 kisha twanga
  • Ongeza maji lita 10 kisha iache ikae usiku mmoja
  • Chuja kwa kitambaa kisha nyunyizia kwenye mimea
  • Rudia kila baada ya siku 10-15 au kila wiki endapo kuna wadudu wengi.

Au

  • Saga kilo 2 za mbegu
  • Changanya na maji lita moja
  • Acha kwa usiku mmoja
  • Ongeza maji lita 10
  • Nyunyizia mimea

Majani ya Mwarobaini kama dawa

  • Chukua kilo 1 ya majani ya mwarobaini
  • Twanga kisha changanya na lita 1 ya maji
  • Funika na acha kwa saa 12-24 au hatawiki moja
  • Koroga vizuri, ongeza maji lita 4 na gramu 30 za sabuni. Endelea kukoroga hadi sabuni iyeyuke
  • Chuja kisha nyunyizia mara 3 kwa wiki

Mwarobaini hukua ukanda wa pwani karibu na usawa wa bahari una nguvu mara 2 zaidi ya inayooteshwa milimani.

  1. Ndulele
  • Chukua matunda ya ndulele 30 au 40 haijalishi yameiva au mabichi
  • Yakatekate na uyakamue ili kupata juisi
  • Ongeza maji lita 1
  • Koroga vizuri kisha chuja
  • Ongeza maji lita 2
  • Tumia lita moja ya dawa kwa lita 15 za maji
  • Nyunyizia mimea mara 2 kwa wiki
  1. Mbangibangi (bangi mwitu)
  • Fuata hatua kama zile za mwarobaini
  • Mbali na kutengeneza dawa, mmea huu huoteshwa pamoja na mazao.Harufu yake husaidia kufukuza wadudu na hata minyoo fundo inayoathiri mizizi ya mimea mfano nyanya.
  • Mmea huu huonyesha matokeo mazuri unapooteshwa na kabichi au nyanya.
  • Mmea huu pia una uwezo mkubwa wa kuvuta vithiripi na kupunguza mashambulizi ya wadudu hawa kwa mazao.
  1. Mchicha
  • Chukua kilo 1 ya mchicha
  • Twanga kisha loweka kwenye maji lita 1, acha ikae kwa saa 12.
  • Ongeza sabuni gramu 20.
  • Koroga ili sabuni iyeyuke kisha ongeza maji lita 2 na uchuje.
  • Tumia kwa uwiano wa 1:10 yaani lita 1 ya dawa kwa lita 10 ya maji.
  1. Sabuni
  • Mchanganyiko wa sabuni na maji au mchanganyiko wa sabuni, maji na mafuta ya taa unaweza kuwa sumu na kuua wadudu wenye ngozi laini kama vidukari.
  • Sabuni ya kipande, ya unga au ya maji inaweza kutumika.
  • Kwa kila lita 1 ya maji ongeza gramu 5-8 za sabuni sawa na kijiko 1-1.5 cha chai.
  • Mchanganyiko mkali ni kwa ajili ya mbawa kavu na viwavi na mchanganyiko mwepesi ni kwa ajili ya wadudu laini
  1. Mkojo wa ng’ombe (mfori)
  • Mkojo wa ng’ombe au wanyama wengine ukivundikwa vizuri kwa muda wa siku 10-14 unaweza kuwa kiua wadudu kizuri kwa ajili ya wadudu wengi waharibifu wa mimea
  • Tengeneza mtaro wa kukinga mchanganyiko wa mkojo na kinyesi cha ng’ombe kutoka kwenye zizi
  • Chimba shimo dogo kisha weka ndoo kukinga mkojo huo
  • Hifadhi mchanganyiko huo ili uchachuke kwa muda wa siku 10-14
  • Zimua kiasi 1 cha mkojo na maji 2 hadi 6 (1:2-1:6)
  • Ongeza sabuni kidogo au majivu.
  • Chuja vizuri tayari kwa kunyunyizia kwenye mimea kwa uwiano wa 2-6:15

Inashauriwa kwamba mchanganyiko huu ujaribiwe kwenye mimea michache kwanza ili kuona kama ni mkali sana kwani unaweza kuathiri mimea, hasa majani laini na machanga.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

1 maoni juu ya “Mbolea hai na madawa ya asili ni muhimu kwa mimea, wanyama na binadamu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *