- Kilimo, Kilimo Biashara, Udongo

Kilimo hai hupambana na mabadiliko ya tabianchi

Sambaza chapisho hili

Mabadiliko ya hali ya hewa yanatishia msingi wa maliasili katika sehemu kubwa ya ulimwengu hasa nchi zinazoendelea. Mabadiliko ya hali ya hewa huharakisha uharibifu wa mifumo ikolojia na kufanya kilimo kuwa kigumu kwa wakulima mashamba wenye madogo. Matokeo yake ni kwamba wakulima ambao ni muhimu sana kwa usalama wa chakula na uchumi wa mashinani wanakabiliwa na hali mbaya ya hewa ambao unaathiri uzalishaji.

Hii ni pamoja na ukame, mafuriko na dhoruba, wakati huo huo wanakabiliwa na athari za taratibu za mabadiliko ya hali ya hewa, kama vile shinikizo la maji kwa mazao na mifugo, na mashambulizi ya wadudu yasiyotabirika.

Ni wazi kwamba kilimo kinachangia kwa uzalishaji wa gesi chafu inayosababisha mabadili- liko ya tabia nchi. Hivyo wakulima wana jukumu la kukuza bioanuwai na kudhamini huduma za mfumo ikolojia ambao shughuli za kilimo hutegemea. Hii ndio ujumbe wa MkM kwa wakulima mbali na kutoa habari mwafaka kwa wakulima ili kubadili mfumo wa kilimo na kufanya kiwe endelevu zaidi.

Moja ya mifumo ni kilimo hai ambao hutegemea na kutumia rasilimali asili shambani na kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Wakulima wa kilimo hai wamejitolea sana kuboresha udongo. Wengi wanasema, ‘lisha udongo ili uweze kulisha mimea.’ Kwa kuongeza kiasi cha viumbe hai kwenye udongo, wakulima wa kilimo hai huongeza uwezo wa udongo kunyonya maji, kupunguza athari za ukame na mafuriko. Uboreshaji wa uwepo wa viumbe hai kwenye udongo pia huisaidia kunyonya na kuhifadhi virutubisho vinavyohitajika kukuza mazao yenye afya ambayo yanaweza kustahimili wadudu na magonjwa.

Utafiti unaonyesha kwamba udongo chini ya uzalishaji wa kilimo hai unaweza kuondoa hewa chafu ya kaboni dioksidi kutoka katika angahewa kila msimu wa uzalishaji. Ikiwa tutaongeza ekari za shamba tunazozalisha kwa mfumo wa kilimo hai basi tutaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kusafisha hewa na mazingira.

Kwa sababu mbolea inayotokana na mafuta na viuatilifu vingi haipendekezwi, basi kilimo hai haitoi gesi chafu kwa mazingira. Pia, utengenezaji wa kemikali na pembejeo zinazotumika kwa kilimo cha kawaida zinahitaji nishati nyingi.

Sasa hivi, watu wanajali zaidi kuliko hapo awali juu ya kile wanachokula, sababu za kununua chakula kilichozalishwa kwa mbinu za kilimo hai zinaendelea kuongezeka. Chakula cha kilimo hai hukusaidia wewe, afya yako, afya ya watoto wako, nchi na ulimwengu.

Kila mmoja wetu anaweza kusaidia kupunguza ongezeko la joto duniani na kutunza mazingira kwa kufanya chaguzi ambazo hazina madhara kwa mazingira.

Tunaweza kuwa sehemu ya suluhisho

Kwa walaji na watumiaji wa mazao ya kilimo, kuchagua vyakula vya kilimo hai ni njia moja kufaidi mazingira, uchumi wa mashinani, afya ya familia na jamii.

Tunapofanya haya, basi tunaweza pia kuwarudisha wakulima wengi wadogo hasa akina mama na vijana kwenye kilimo, kubadilisha mifumo ya kilimo na chakula. Pamoja na changamoto tunazokabiliana nazo, tunahitaji vijana kulima sasa kuliko wakati mwingine wowote lakini ili kuwashirikisha tunahitaji kilimo kipya, ambacho kinaungwa mkono na sera na uwekezaji, ambacho ni cha ubunifu, kinachukua fursa ya teknolojia mpya, kinaweza kutosheleza soko na kumlipa mkulima.

Kilimo hai kinavutia kwani kinazalisha chakula chenye afya na salama kwa matumizi ya nyumbani na sokoni.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *