- Usindikaji

Unaweza kusindika stroberi kwa kutengeneza jamu

Sambaza chapisho hili

Wakulima wengi wamekuwa na mawazo finyu hasa katika kutatua changamoto zitokanazo na upotevu wa mazao yao shambani jambo lililowapelekea, kusahau kuwa kuna mbinu mbalimbali zakukabili changamoto hizi kama vile kujikita katika utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na mazao.

Katika nakala hii Mkulima Mbunifu inakuangazia kijana Charles Watson kutoka Mbeya aliyejikita katika kilimo cha stroberi na uchakataji wa bidhaa zitokanazo na zao hili kama vile jamu kwa lengo la kuongeza pato na kuzuia upotevu wa mazao.

Malighafi zinazohitajika kutengeneza Jamu

Ili kutengeneza jamu ya stroberi zifuatazo ni malighafi muhimu.

  1. Stroberi zilizoiva vizuri
  2. sukari nyeupe
  • limao
  1. Pectini

Vifaa

  1. Sufuria kubwa moja (Canner). Hii inatumika katika kuchemshia jamu wakati ikiwa imeshapakiwa katika vifungashio au makopo maalumu kwa ajili yakuhifadhia jamu. Jamu lazima ichemshwe katika maji ya moto ili kuondoa vijidudu au bakteria.
  2. Kijiko kikubwa. Hii inatumika kuweka jamu katika vifungashio, pamoja na kuchotea jamu wakati wa kuangalia kujua kama imeiva vizuri.
  • Sufuria ya wastani. Hii itatumika kuchemshia mchanganyiko wako ambao ni matunda kwa ajili ya kutengeneza jamu. Hapa unashauriwa kutumia sufuria nzito zisizozidiwa na moto mkali, pia iwe rahisi kusafisha baada yakutumia.
  1. Makopo maalumu (jars). Haya ni makopo maalumu yanayotumika kufungashia au kuhifadhi jamu inapokuwa tiyari.
  2. Chanzo cha nishati (jiko la umeme, gesi au mkaa). Unaweza kuandaa jamu yako kwa kutumia chanzo kimojawapo katika.

Namna ya kutengeneza

  1. Andaa vifungashio pamoja na vyombo vya kupikia kwa kuosha vizuri. Chagua matunda yaliyoiva (na ambayo hayajaiva kupitiliza). kisha ondoa sehemu ya juu ya stroberi au kikonyo, na osha matunda yako kwa maji safi na salama. Epuka kutumia matunda yaliyoharibika kutengeneza jamu kwani ni hatari kiafya.
  2. Pondaponda matunda hayo ili kutengeneza rojo nzito. Hatua hii ya kuponda itasaidia matunda kutoa pectin ya asili lakini pia hatua hii inapunguza muda wa mchanganyiko wako kukaa jikoni huku ikirahisisha hatua ya kutenganisha mbegu kwa matunda.
  3. Ongeza kiasi cha sukari. Kwa matunda haya unashauriwa utumie vikombe vinne (4) vya sukari kwa vikombe sita (6) vya rojo ya stroberi. Kumbuka katika utengenezaji huu wa jamu tutatumia pectini hivyo unatakiwa kukoroga mara kwa mara ili pectini iweze kuchanganyika vizuri. Katika hatua hii unashauriwa kuweka vikombe (2-3) na kisha kumalizia vilivyobaki katika hatua nyingine inayofuata.
  4. Changanya mchanganyiko wako na pectini kisha bandika jikoni na anza kuchemsha mchanganyiko huo kwa dakika 5 hadi 10 na endelea kukoroga mara kwa mara ili kuzuia isishike sufuria kwa chini, lakini pia ili ichanganyike vizuri. Sababu yakuongeza pectini ni kufanya rojo uwe mzito. MUHIMU: Matumizi ya pectini katika maandalizi ya jamu, huwa na faida kama, uji kuwa mzito, kupunguza muda wa kupika, kupunguza kiasi cha sukari katika jamu na kudumisha virutubisho muhimu vilivyopo katika tunda husika.
  5. Ongeza kiasi cha sukari kilichobakia pindi mchanganyiko wako unapofikia kiasi cha kuiva kisha endelea kuchemsha kwa dakika (1) zaidi. Hapa unashauriwa utumie moto wa wastani au wa chini ili kuepuka mapovu kujitengeneza.
  6. Kama povu limejitengeneza unatakiwa kutoa kwa kutumia kijiko. Wataalamu wa vyakula wanasema povu linaweza kusababisha jamu kuharibika mapema, hivyo ni vyema ukaondoa au ukatumia moto wa wastani ili povu lisitokee.
  7. Kagua ubora wa jamu yako. Chukua kiasi kidogo cha jamu na uweke katika jokofu kwa dakika 2 kisha toa. Chukua uji huo tandaza katika sahani kisha chora mstari mmoja katikati, kama mstari utabaki kwa mda bila kupotea au kuchanganyika basi jamu yako itakuwa iko tayari.
  8. Epua kisha pakia jamu katika vifungashio kisha weka katika maji ya uvuguvugu kwa dakika 2. Toa jamu katika maji na acha ipoe tayari kwa matumizi. unaweza kutumia hii jamu kwenye mkate, mandazi, n.k

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Charles Watson kwa simu namba 0620244852.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *