- Kilimo Biashara

Vijana wajiajiri kupitia kilimo hai

Sambaza chapisho hili

Kumekua na muamko wa vijana kutumia fursa ya kilimo kujipatia kipato. Mkulima Mbunifu ilikutana na vijana mkoani Arusha ambao waliamua kujifunza na kutengeneza mboji kwa ajili ya biashara.

Kutokana na changamoto za ajira vijana hawa wameweza kubuni mradi na kutumia elimu waliyonayo ya ujenzi wa mitambo ya biogas na utengenezaji wa mbolea hai kama fursa ya kujiingizia kipato.

Pia, wanufaikaji wengi wa mitambo ya kuzalisha biogas hawana ufahamu mkubwa juu ya ubora wa mabaki ya mwisho kwenye mitambo yao (baioslari). Mabaki hayo yanaweza kutumika kama mbolea nzuri shambani badala ya kuipoteza bure.

Vijana hawa walianzaje uzalishaji wa mbolea

Tukiwa vijana wanne ambao ni Frank Kisamo (21), Benedict Jeremiah (20), Selline Antony (20) na Edward Jacob (21), wawili kati yetu wakiwa wanafunzi bado tumefanikiwa kuanza biashara hii mwaka jana Julai (2020) kama biashara rasmi. Kabla ya kua-nza uzalishaji wa mbolea hii tulikuwa tunaifanyia majaribio ambapo tulijihusisha na utengenezaji wa mitambo ya biogas.

Kikundi chetu hukutana mara chache kujadiliana kuhusu mradi wetu wa biashara ya mbolea ambapo twakutana kila baada ya wiki mbili (2) na nje ya hapo huwa tunafanya shughuli zetu kupitia vikao na mafunzo ya mtandaoni.

 Changamoto

Ukweli ni kwamba wazazi wengi wanatamani kuwaona vijana wao wa-kifanya kazi za ofisini zaidi kuliko kazi za ujasiriamali. Hivyo, ilikuwa ngumu kwao kukubali kwa moyo mmoja hadi walipoona taasisi nyingine zikitambua kile ambacho tumekuwa tukifanya na kutusaidia ili kufanikisha.

Muamko wa matumizi ya mbolea hai

Muamko wa matumizi wa mbolea hai ni mkubwa kutokana na ukweli kwa-mba jamii kubwa za wakulima ni wafugaji na pia watu wa vipato vya chini. Pia kutokana na elimu inayotolewa wakati wa uwekaji mitambo ya biogas vijijini, wakulima wengi tunawajuza faida ya mabaki yapatikanayo kwenye mitambo tu-liyowawekea kwenye kilimo na ufugaji.

Jinsi ya utengenezaji

Mbolea hii tunaipata kwa kuchukua mabaki ya mwisho kabisa kwenye mfumo wa biogas, tunaisindika kwa kuikausha vyema kuondoa majimaji ambapo itabaki kuwa kama udongo. Tunaichambua kwa kuondoa vitu a-mbavyo havihusiki kama plastiki, mawe na mabaki mengine. Baada ya hapo tunaichekecha vyema na kuiweka kwenye vifungashio

Kwa upande wa mbolea vunde yenyewe ni mbolea iliyo maarufu kwa wakulima wengi ambapo tunate-ngeneza kwa kuchanganya kinyesi ya ng’ombe, majani makavu na mabichi na huwekwa mara nyingi nyuma ya banda la mifugo. Mbolea hii hupoozwa kwa maji au mvua kunyeshea.

Baada ya siku 59, mbolea hiyo (biwi) hugeuzwa na kuendelea kulivundika hadi pale maada zote zitakapoanza kugeuka na kuwa kama udongo ambapo mbolea huwa tayari kupelekwa shambani.

Namna ya kuwafikia wateja na bei

Tunawafikia wateja wetu kupitia maonyesho mbali mbali, kwa mfano, maonesho ya kitaifa ya wakulima (Nane Nane), semina zinazoandaliwa kwenye vituo mbalimbali, mafunzo tunayofanya maeneo ya vijijini juu ya mitambo ya biogesi na mbolea hai.

Uuzaji

Pia, tunauza mbolea tunazozalisha kwa bei tofauti ambapo mbolea kwa ajili ya kusia na kukuzia bustani iliyo kwenye kifungashio cha 1Kg tunauza kwa shilingi elfu mbili (TSh 2,000/=). Mbolea ya maji ambayo inauzwa kwa ndoo ya lita ishirini (20) yenyewe ina-tegemea na umbali wa mteja japo mara nyingi huwa haizidi shilingi elfu tatu (TSh 3,000/=).

Mbolea hii ya maji huchanganywa na maji mengine ndoo kubwa mbili ambazo zitaongeza ndoo ya tatu. Mbolea hii huweza kutumika kama mbolea dawa kwa mimea, na huweza kutumika kwenye eneo kubwa.

Shukrani

Tunashukuru jarida la Mkulima Mbunifu, kwani mara ya kwanza tuliliona kwenye maonesho ya Nane Nane mwaka jana. Tulitamani kutoa andiko letu juu ya kazi tunayoifanya ili kuhamasisha vijana wengine juu ya kilimo hai kwani kuna shughuli nyingi za kufanya na zinalipa kuliko kusubiria ajira.

Hata hivyo, gazeti hili linatoa hamasa kwa wakulima kufanya kilimo hai kutokana na jinsi wakulima wengine walivyo weza kueleza mafanikio yao.

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na KSM Organic Company, kwa simu namba 0763579692 / 0742002091, barua pepe: ksmorganiccompany@ gmail.com

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *