- Usindikaji

Sindika karoti na nazi kupata mafuta na kukuza pato

Sambaza chapisho hili

Vijana wengi kwasasa wameanza kuthamini na kuwa na mwamko katika ujasiriamali kutokana na uhaba wa ajira lakini pia uhitaji mkubwa kwa walaji wa bidhaa salama zinazozalishwa ndani ya nchi.

Wengi wao wamejikita kusindika mazao mbalimbali na kupata bidhaa bora zinazowasaidia kupata kipato kwa urahisi.

Bi. Christina Macha ni miongoni mwa wasindikaji wa mafuta yanayotokana na mazao mbalimbali kama vile nazi, karoti, karafuu lakini mafuta ya nazi yakiwa ndiyo mama kwenye ujasiriamali wake.

Anaeleza kuwa, yeye anapenda kula vyakula vya asili hivyo aliamua kutafuta elimu kupitia SIDO na kutengeneza mafuta kwa ajili ya nyumbani na baadaye kufikia kuwa mzalishaji mkubwa wa bidhaa tatu ambazo ziko sokoni kwa jina la NONERIA virgin coconut oil, NONERIA carrot oil, na NONERIA clove oil.

Kwanini mafuta ya karoti

Karoti ni moja katika mazao ya mizizi aina ya mboga yenye vyanzo vingi vya madini ya kalsiamu, chuma na wingi wa vitamin B.

Karoti pia ni miongoni mwa mazao kadhaa ya bustani (mbogamboga) yenye thamani kubwa kwa sasa hapa nchini na duniani kote na ni moja ya zao linaloweza kulimwa kwa urahisi  kama mazao mengine ya mbogamboga.

Faida za karoti kiafya

  • Karoti husaidia kuongeza kinga ya mwili..
  • Husaidia kuzuia magonjwa mbalimbali kama vile kisukari
  • Husaidia macho kuona vizuri..
  • Karoti husaidia kuimarisha fizi na meno
  • Husaidia kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu.
  • Karoti husaidia kulainisha ngozi

Namna ya kusindika mafuta ya karoti

Malighafi

Karoti, sufuria, kisu, nazi, kitambaa cha kuchujia mafuta na moto

Namna ya kutengeneza

  • Chukua kiasi cha karoti unachotaka kusindika.
  • Safisha kwa maji safi na salama kuondoa udongo na uchafu mwingine.
  • Ondoa alama zote zisizofaa zinazoonyesha utofauti kwenye karoti kama vile alama nyeusi.
  • Katakata vipande vidogo sana au saga kisha weka kwenye sufuria
  • Changanya na mafuta ya nazi kisha chemsha kwa muda mpaka ilainike.
  • Kamua kwa kutumia kitambaa safi ili kupata mafuta.
  • Weka kwenye chupa maalumu au vifungashio tayari kwa matumizi au kupeleka sokoni.

Matumizi

Mafuta haya hutumika kula kwa kupikia vyakula vya aina mbalimbali visivyohitaji moto sana au tumia kupaka ngozi.

Sindika nazi kupata mafuta

Malighafi

Nazi zilizokomaa, mbuzi/mashine ya kusaga, maji safi na salama, chujio/kitambaa safi na moto

Namna ya kupata mafuta

  • Chukua nazi zilizokomaa vizuri
  • Kuna nazi kwa kutumia kifaa chochote kama vile mbuzi.
  • Chemsha maji mpaka yapate uvuguvugu
  • Chukua maji hayo kisha changanya na nazi uliyokuna kwa kutumia mikono yako kwa muda wa angalau dakika moja.
  • Kamua kwa kutumia chujio la nazi au kitambaa cha kukamulia kisha rudia mara mbili hadi tatu kuweka maji ya vuguvugu na kukamua ili kutoa mafuta yote
  • Ukishapata tui weka katika chupa na kuiweka masaa 24 ili mafuta yajitenge na maji.
  • Unaweza kuweka jikoni kwa moto wa wastani kwa muda wa saa moja au mpaka maji yakauke yote kisha kubakia mafuta tu.
  • Toa mapovu ya juu halafu weka mafuta yako katika chupa utakayotumia tayari kwa matumizi au sokoni.

Kuhusu usindikaji wa mafuta haya na mengine, wasiliana na Christina Macha kwa simu namba 0767188854

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *