- Usindikaji

Mbinu rahisi za kuandaa asali

Sambaza chapisho hili

Asilimia kubwa ya asali kwenye soko la ndani, inakuwa imechanganywa na haina kiwango kinachofaa kwa matumizi.

Asali nyingi inayouzwa sokoni inakuwa na vitu visivyohitajika kama vile poleni, sehemu za miili ya nyuki, nta na hata taka nyingine zisizo husika na asali. Hii inatokana na uelewa mdogo walio nao wafugaji wa nyuki, juu ya namna ambavyo wanaweza kuweka asali katika ubora unaotakiwa. Ubora wa asali hudhihirishwa na namna ambavyo asali inavunwa, kuchujwa, na kuhifadhiwa.

Baada ya asali kuvunwa, ihifadhiwe kwenye chombo kisafi na kifunikwe vizuri ili kuzuia uchafu na unyevu unaoweza kuiaribu. Kuna njia mbili ambazo mfugaji wa nyuki anaweza kutumia kuvuna na kuandaa asali, anatakiwa kuwa na ndoo safi, na kitambaa safi ambacho kimetengenezwa kwa malighafi za nailoni.

Mbinu rahisi

  1. Kunja kitambaa mara mbili ili kuwa na matabaka manne, kisha kifunge kwenye shingo ya ndoo ya plastiki au ya chuma.
  2. Weka asali ambayo haijachujwa iwe inadondokea ndani kwa matone/taratibu.
  3. Taka zote zisizo hitajika kwenye asali zitabaki kwenye kitambaa hicho.
  4. Acha asali nzito ijichuje usiku wote.
  5. Ondoa asali inayoganda kwenye kitambaa kwa kutumia kijiko.
  6. Weka asali kwenye chombo kilichofunikwa vizuri.

Mbinu ya kuyeyusha kwa kutumia maji ya moto

Mbinu hii ni nzuri na inafaa zaidi kwa asali ambayo ilishavunwa na kuhifadhiwa kwa muda mrefu, hasa asali ambayo ilishaganda.

  1. Asali inapashwa kwenye maji ya moto ikiwa kwenye chombo kingine, hii husaidia asali kuyeyuka na kuchujika vizuri (Kama inavyooneshwa kwenye mchoro). Ni lazima uhakikishe kuwa joto linatosha kuwezesha asali kuyeyuka na kutiririka, liwe kiasi cha nyuzi joto 45°C.
  2. Koroga asali mfululizo ili kuhakikisha kuwa joto linasambaa kote.
  3. Kupasha joto husaidia pia kuondoa ukungu ambao husababisha asali kuvunda, ambapo hilo hutokea unyevu kwenye asali unapokuwa zaidi ya 17%.
  4. Asali iliyoyeyuka inapopita kwenye kitambaa unachochujia, funika ndoo kwa mfuniko mzuri. Acha itulie kwa muda wa siku tatu.
  5. Ondoa tabaka la juu la asali iliyoganda kama ulivyofanya katika mbinu ya kwanza, kwa kutumia kijiko.
  6. Weka asali kwenye chupa iliyofungwa vizuri tayari kwa kuuza au kwa matumizi ya nyumbani.

Namna ya kupima asali ambayo ina vitu vinavyopunguza ubora

Baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, huongeza vitu vingine visivyokuwa asali kama vile molasesi, sukari, na glukosi ili waweze kuuza zaidi. Utafiti unaonesha kuwa asilimia 25 ya asali inayouzwa katika soko la ndani, inakuwa siyo halisi au haijachunjwa inavyotakiwa.

Ni vizuri walaji wakafahamu namna ya kutambua asali halisi na asali ambayo imechanganywa na vitu vingine.

Asali nzuri ina sifa zifuatazo:

  • Inamiminika kwa urahisi na ni laini.
  • Ina harufu na ladha nzuri. Hakikisha unaionja asali kama bado haijafungwa ili kuwa na uhakika kuwa haudanganywi.
  • Inapomiminwa hutengeneza tabaka la mapovu madogo mdogo kama maji.
  • Rangi ya asali inaweza isisaidie kutambua kama asali ni nzuri au la. Rangi ya asali hutegemeana na aina ya mimea ambayo nyuki walikusanya poleni.
  • Huganda inapowekwa kwenye hali ya ubaridi.
  • Ili kupima kiwango cha unyevu kwenye asali, weka kiasi cha asali kwenye kipande cha pamba, washa njiti ya kiberi na uweke pamba hiyo karibu. Endapo asali hiyo ina kiasi fulani cha maji, itatoa mlio wa kupasuka, na kama ina ubora unaotakiwa basi itaungua kawaida.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *