- Kilimo, Mimea

Wakulima wanasemaje kuhusu masoko ya mazao ya kilimo hai

Sambaza chapisho hili

Mkulima anaezalisha kwa mazao kwa kufuata misingi ya kilimo hai, Bw. Zadock Kitomari alisema kuwa, unapoanza kujishughulisha na kilimo hai ambacho hakitumii kemikali unaona kuwa uzalishaji unakuwa mdogo lakini kwa kadri unavyoendelea uzalishaji unakuwa mkubwa.

Anaeleza kuwa, kilimo hai ni aina ya kilimo kinachoangalia uhai wa mazingira, uhakika na usalama wa mlaji na usalama wa chakula jambo ambalo linamuhakikishia mkulima kipato kwa kutumia fursa alizonazo mkulima.

Akizungumzia upatikanaji wa masoko ya kilimo hai, Kitomari anasema, “Masoko ya kilimo hai yapo, isipokuwa yanapatikana tu, kwa wale wakulima waliothibitishwa na kufanyiwa utafiti kuwa ni kweli mazao yao yanazalishwa kwa misingi ya kilimo hai”

Anesema kuwa, mashirika kama OICOS, na MESULA yamekuwa yakisaidia wakulima kwa kiasi kikubwa kujiingiza katika vikundi vya uzalishaji kwa misingi ya kilimo hai, kuwapa elimu sahihi kuhusu kilimo hai, pamoja na kuwatafutia masoko ya pamoja ambapo huweza kuuza bidhaa zao.

Anaongeza kuwa, wakulima wengi wamekuwa wakilalamika kuwa hakuna soko lakini tatizo kubwa ni kuwa hawajajikita haswa katika uzalishaji kwa kufuata misingi ya kilimo hai. Aidha, wanatakiwa kuangalia jamii inayowazunguka kwanza kwani soko linaanzia nyumbani ndipo uingie katika masoko makubwa na hata sasa wakulima wengi bado wanahitajika kwa ajili ya kuzalisha mazao na bidhaa za kilimo hai.

Sifa za shamba la mkulima wa kilimo hai

Bw. Kitomari anasema kuwa, ili uweze kutambulika kuwa ni mzalishaji wa mazao ya kilimo hai, kuna baadhi ya sifa zinazokutambulisha wewe hata bila kutoa maelezo. Sifa hizo ni kama zifuatavyo;

Mazao ya kilimo hai ni muhimu sana kwa afya ya binadamu

Ni lazima eneo lako la kilimo kuwe na mboji. Wakulima wengi wanadai kuwa wanafanya kilimo hai lakini ukitembelea maeneo yao hawana mboji.

Hakikisha unatengeneza mboji hiyo kila wakati, kwa kutumia mabaki ya mifugo na mazalia mengine isipokuwa taka ngumu.

Mkulima wa kilimo hai ni lazima shambani kwake kuwe na uzio kwa ajili ya kuzuia sumu kali zinazotoka kwenye mashamba yanayotumia kemikali na dawa za viwandani na hata kuzuia wanyama waharibifu.

Uzio wa mkulima wa kilimo hai lazima kuwepo na miti ya dawa, ambayo hutumika kukinga wadudu waharibifu na pia huchumwa na kutengenezea dawa.

Mkulima wa mazao ya kilimo hai ni lazima awe na elimu ya kutosha juu ya kilimo hai na aweze kuwaelimisha na kuwashauri wakulima wenzake waliomzunguka kuhusu faida na hasara za kilimo hai.

Nini mchango wa wataalamu kuhusiana na masoko hayo

Wataalamu mbalimbali wanaeleza kuwa, kwa sasa bidhaa zinazotokana na kilimo hai zinazidi kuongezeka na hii ni kutokana na baadhi ya wanajamii kuufahamu kwa kiasi kikubwa madhara yanayotokana na mazao yanayozalishwa kwa kutumia madawa na kemikali za viwandani.

Lukas Rwechoka ambaye ni Afisa masoko wa halmashauri ya Arusha anasema kuwa, kwa sasa wakulima wamekuwa na mwamko mkubwa sana kuhusiana na uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo hai, ila tatizo kubwa limekuwa soko ambalo mara kwa mara limekuwa likiwakatisha tama ya kuendelea kuzalisha bidhaa hizo.

Katika mahojiano maalumu na Mkulima Mbunifu, Rechoka aliweza kubainisha mambo kadha wa kadha yanayogusa soko la mazao ya bidhaa za kilimo hai:

Suala la ukosefu wa soko la mazao ya kilimo hai!

Ukosefu wa soko la mazao ya kilimo hai ni tatizo kubwa na linapunguza kipato  kwa wakulima na kuondoa morali ya kuendeleza uzalishaji kwa misingi ya kilimo hai. Hii pia inapelekea jamii na taifa husika kushuka kwa uchumi.

Je, wakulima wanatakiwa kufanya nini ili kuondokana na tatizo hili?

Wakulima wa mazao ya kilimo hai wanatakiwa wawe waaminifu na wafuatae misingi yote ya uzalishaji wa mazao ya kilimo yai. Aidha, wasiwe wadanganyifu katika shughuli nzima ya uzalishaji wa mazao na bidhaa zote zitokanazo na kilimo hai.

Vipi kuhusu uelewa wa walaji kuhusiana na bidhaa za kilimo hai?

Uelewa kwa walaji bado ni changamoto kubwa kwani wengi wanapenda kutumia bidhaa zitokanazo na misingi ya kilimo hai lakini wigo wa uelewa wa suala zima la kilimo hai bado ni mdogo kwa walaji hao hasa wa ndani. Kuhusu walaji wa nje, wao wana uelewa mkubwa na wakisaidiwa na sera za nchi zao na ufafanuzi mzuri juu ya mazao yatokanayo na kilimo hai.

Je, kuna njia yoyote ambayo wakulima wanaweza kutumia kurahisisha upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo hai wanazozalisha?

Njia ambayo wakulima wanaweza kutumia kurahisisha upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo hai ni kuwa wakweli na waaminifu katika shughuli zote za kilimo hai.

Wanatakiwa kuwa na takwimu sahihi na kufahamu kwa ufasaha hatua za uzalishaji tangu kulima, kupanda, kuhudumia mazao, kuvuna na kuhifadhi mazao hayo.

Ili kufanikisha hayo, hakuna budi kuwaruhusu wakaguzi (mawakala) wa kilimo hai walioidhinishwa wafanye ukaguzi na kutoa mwongozo na ushauri juu ya suala zima na kuwataarifu wanunuzi juu ya hatua sahihi zilizofuatwa katika kilimo hai.

Ni aina ipi ya mazao na bidhaa zinazozalishwa kwa misingi ya kilimo hai ambazo ni maarufu sana katika soko?

Mazao na bidhaa zinazozalishwa kwa misingi ya kilimo hai ambazo ni maarufu sana katika soko ni pamoja na mbogamboga, matunda na hata kufuga kuku ambao mayai hayawi na kemikali.

Nini wito kwa wakulima?

Wakulima wanatakiwa kujikita katika kilimo hai kwani kina tija kubwa, na watu wengi wanahitaji mazao na bidhaa zinazotokana na kilimo hai hasa kwa ajili ya kulinda afya zao na bei pia ziko juu hivyo ni dhahiri kuwa wakulima watajiongezea kipato na kuinuka kiuchumi.

Wito kwa wadau wa kilimo hai

Wadau wote wa kilimo hai wanahitajika kuongeza nguvu juu ya kilimo hai, kwa kusaidia kutoa elimu ya kutosha kwa jamii na kwa taifa juu ya faida za kilimo hai na kusaidia pia katika upatikanaji wa masoko ya mazao yatokanayo na kilimo hai.

Wito kwa serikali juu ya kilimo hai

Serikali ni vyema ikaendeleza kilimo hai na kushiriki kwa kiasi kikubwa katika kutoa mafunzo stahiki, ikiwa ni pamoja kusimamia vyema shughuli za uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo hai.

Aidha, serikali inahitajika kutengeneza mazingira mazuri na kuweka sera nzuri zitakazo inua kilimo hai ikiwa ni pamoja na kusaidia wazalishaji kunadi na kutafuta soko la bidhaa za kilimo hai sehemu mbalimbali ndani ya nchi na hata nje kwa kuwa walaji ni wengi.

Ni kwa namna gani unaweza kutambua kuwa mazao haya yanatokana na kilimo hai?

Ni rahisi kutambua mazao yatokanayo na kilimo hai kwa kupata historia ya uzalishaji wa mazao hayo, wakulima husika na takwimu za ukaguzi zilizofanyika hatua kwa hatua kupitia kwa wakaguzi au mawakala wa kilimo hai walioorodhesha na kutolea taarifa sahihi na ushauri juu ya zao husika kwa jinsi walivyofuatilia na mkulima jinsi alivyokuwa mwaminifu na mkweli juu ya kilimo hicho.

Kabla mkulima hajazalisha mazao ya kilimo hai ni nini cha msingi anachotakiwa kuzingatia?

Mkulima ni lazima kuzingatia kwa ufasaha misningi ya uzalishaji wa mazao ya kilimo hai pamoja na kuwa mawaminifu na mkweli na kufuata hatua zote za uelewa juu ya kilimo hai kabla hajazalisha mazao ya aina yeyote.

Changamoto zinazoikumba masoko ya kilimo hai

Katika shughuli zozote zinazofanywa hasa za kilimo, suala la changamoto haliwezi kuachwa kutajwa, na kwenye upatikanaji wa masoko ya mazao na bidhaa za kilimo hai pia zipo kama zifuatavyo:

  • Uelewa wa walaji juu ya mazao yatokanayo na kilimo hai
  • Sera za nchi za uuzaji wa bidhaa za kilimo hai kutokuwa wazi na kutiliwa maanani katika uzalishaji.
  • Uchache wa wataalamu, wakaguzi au mawakala wa kutathmini uzalishaji wa kilimo hai.
  • Vikwazo vya nje ya nchi kuhusiana na bidhaa za kilimo hai kulinganisha na matakwa ya walaji wan chi husika katika masoko yao.
  • Ubobevu na mazoea ya matumizi ya bidhaa zinazozalishwa kwa kutumia pembejeo sanisia za viwandani zenye kemikali.

Serikali imejipangaje kuhakikisha masoko ya mazao ya kilimo hai yanapatikana

Juhudi za serikali ni kujipanga kuhakikisha masoko ya mazao yanayozalishwa kwa misingi ya kilimo hai yanapatikana hasa kupitia mikononi mwa watunga sera katika wizara ya biashara na masoko, wizara ya kilimo, chakula na ushirika, wizara ya mifugo na maendeleo ya uvuvi juu ya uzalishaji wa kilimo hai, na uuzaji wa mazao na bidhaa zitokanazo na kilimo hai.

Wadau hawa wakiwemo wakulima wenyewe na walaji, wapewe elimu ya kutosha juu ya faida za kilimo hai na bidhaa zake. Pia kupitia wizara ya mambo ya nje na wizara husika kutangaza na kuhamasisha uzalishaji na utumiaji wa bidhaa zinazotokana na kilimo hai na kuhakikisha kilimo hai kimejikita katika kanuni kuu nne za msingi ambazo ni kanuni ya afya, kanuni ya mazingira, kanuni ya haki na usawa, na kanuni ya uangalizi.

Kila moja ya kanuni hiziz ian kauli mbiu inayofuataiwa na maelerzo ya ufafanuzi. Kanuni hizi zinatumika na kuangaliwa kwa ujumla wake na kuwa mfumo kamili. Zimewekwa kuwa kanuni zinazosimamia maadili yanayohamasisha uwajibikaji kwa taifa na kwa ulimwengu mzima.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Wakulima wanasemaje kuhusu masoko ya mazao ya kilimo hai

  1. I am called Joseph Sekiku, working with FADECO COMMUNITY RADIO, Karagwe. I am on the mailing list for mkulima mbunifu for seeral years. I am coming to Arusha specifically to explore further ways of spreading the content via radio IN THE WEEK OF 26.7.2010

    1. Thank you very much, We are so happy to receive from you and we are hanging to see you very soon. So much welcome

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *