- Mifugo

Fahamu maandalizi muhimu kabla ya nguruwe kuzaa

Sambaza chapisho hili

Nguruwe wanaozaa kwa mara ya kwanza wanaweza kupelekwa kwenye nyumba ya kuzalia masaa machache kwa siku kutoka siku kumi kabla ya siku ya kuzaa ili waweze kuzoea mazingira.

Mara nyingi tumekuwa na makala zinazoelezea ufugaji wa nguruwe katika nyanja tofauti, ikiwa ni pamoja na aina, matunzo na magonjwa ya nguruwe na hata bidhaa zinazotokana na nguruwe na usindikaji wake.

Katika makala hii tutaeleza jambo muhimu kabisa katika hatua za utekelezaji wa mradi wa nguruwe, ili kuweza kumfanya mfugaji kukamilisha ndoto yake ya kuwa na mradi wenye mafanikio makubwa katika ufugaji wa nguruwe.

Maandalizi muhimu

Nguruwe wadogo ni rahisi kuathiriwa na magonjwa, inashauriwa chumba cha kuzalia kisafishwe vizuri kwa kutumia dawa ya kuua wadudu kabla ya kutumika na kiachwe kikauke kwa siku tatu hadi nne kabla ya kuweka nguruwe.

Wiki moja kabla ya kuzaa nguruwe aogeshwe vizuri kwa maji safi na sabuni. Baada ya kuogeshwa anyunyiziwe dawa ya kuzuia wadudu wa ngozi, kisha ahamishiwe kwenye chumba cha kuzalia.

Nitatambuaje dalili za kuzaa!

Nguruwe huonesha dalili mbalimbali kabla ya kuzaa. Mfugaji anashauriwa kumchunguza nguruwe anaekaribia kuzaa mara kwa mara ili kuzitambua dalili hizo.

Umuhimu wa kuzitambua dalili hizo ni kumuwezesha mwangalizi au mfugaji aweze kuwepo wakati wa kuzaa na kutoka msaada inapobidi hasa kwa nguruwe anaezaa kwa mara ya kwanza.

Zifuatazo ni dalili za nguruwe kuzaa

Ni muhimu mfugaji kuhakikisha kuwa anapoona dalili hizi ni ishara dhahiri kuwa nguruwe anakaribia kuzaa:

  • Kuongezeka kwa ukubwa wa kiwele na chuchu kutokana na kujaa maziwa.
  • Maziwa yanaweza kutoka yenyewe kwenye chuchu.
  • Njia ya uke huvimba na kuwa nyekundu na mara nyingine hutoa ute.
  • Nguruwe kuhangaika na kupumua kwa nguvu.
  • Kukojoa mara kwa mara.
  • Kukusanya majani na kuandaa mahala pa kuzalia.
  • Kuongezeka kwa joto la mwili.
  • Nguruwe hupoteza hamu ya kula na tumbo hupwelea.

Uangalizi wa nguruwe wakati wa kuzaa

Ni muhimu nguruwe anapozaa awepo mwangalizi, ili kumsaidia nguruwe endapo kutatokea matatizo kama vile kushindwa kuzaa, kushindwa kufunguka kwa kondo, watoto kushindwa kupumua kutokana na maji ya uzazi n.k.

Kwa kawaida wakati wa nguruwe kuzaa, watoto huzaliwa kila baada ya dakika 15 hadi 20, ambapo watoto hutanguliza kichwa wakati wa kuzaliwa. Huzaliwa wakiwa wameshikamana na kitovu. Damu hutoka mfululizo wakati wa kuzaa.

Huduma muhimu mara baada ya nguruwe kuzaa

Huduma muhimu ambazo hutolewa baada ya nguruwe kuzaa  ni kama ifuatavyo;

  • Mfugaji ahakikishe kondo limetoka lote kwa kuhesabu vipande, kulingana na idadi ya watoto. Endapo vipande havikulingana na idadi ya Watoto unashauriwa kumuona mtaalamu wa mifugo aliye karibu nawe. Kwa kawaida kondo la nyuma hutoka kwa pamoja kati ya dakika 30 hadi 60 baada ya kuzaliwa mtoto wa mwisho na baada ya kutoka lichomwe moto au kufukiwa.
  • Kumpangusa kila mtoto kwa kutumia kitambaa kisafi na kikavu ili kuondoa maji maji ya uzazi.
  • Hakikisha watoto wanaoonesha matatizo ya kupumua wanasaidiwa kwa kuwashika miguu ya nyuma na kuwaning’iniza kichwa chini. Pia unaweza kuwamwagia maji baridi kwenye kichwa au kifua ili kumshtua na kumsaidia kupumua.
  • Hakikisha watoto wote wananyonya ili wapate maziwa ya kwanza, ambayo ni muhimu katika kuwapa kinga dhidi ya magonjwa.
  • Hakikisha watoto wanawekwa mahala penye joto la kutosha ili kuwakinga dhidi ya baridi kali.
  • Kuhakikisha vitovu vinakatwa na kuacha sentimita tano kwa kutumia vifaa visafi, na kisha kupaka dawa ya joto ili kuzuia magonjwa.
  • Hakikisha nguruwe anapewa maji wakati wote.
  • Hakikisha nguruwe hawalalii au kuwala watoto.

Utunzaji wa nguruwe anaenyonyesha

Baada ya kuzaa, nguruwe apewe ongezeko la kilo moja ya chakula kila siku hadi siku ya nne. Kuanzia siku ya tano hadi ya nane, apewe hadi kilo nne. Baada ya hapo apewe kilo tatu na moja ya tatu kwa kila mtoto. Kwa mfano; nguruwe mwenye watoto 12 apewe chakula kiasi cha kilo saba (kilo 3+1/3×12=7).

Siku ya kuachisha watoto kunyonya, chakula kipunguzwe hadi kilo 2.5 kwa siku ili kupunguza uzalishaji wa maziwa na kuepuka uwezekano wa kupata ugonjwa wa kiwele. Nguruwe apewe maji ya kutosha wakati wote.

Nguruwe hurudia kuingia kwenye joto baada ya siku tano hadi kumi baada ya kuachisha kunyonyesha. Mfugaji anashauriwa kumpandisha nguruwe mara tu anapoona dalili za joto kama ana afya nzuri.  Ikiwa afya yake hairidhishi, itabidi alishwe chakula cha ziada ili kumwandaa kumpandisha katika joto la pili.

Utunzaji wa watoto wa nguruwe baada ya kuachishwa ziwa

Utunzaji wa watoto ni muhimu kwani ni rahisi kupata magonjwa mbalimbali, kudumaa katika ukuaji, na hatimaye kuchukua muda mrefu kufikia umri na uzito wa uzalishaji au kuuzwa hivyo kupunguza tija na kipato kwa mfugaji.

Mambo muhimu ya kuzingatia katika utunzaji wa watoto ni pamoja na ulishaji, kinga dhidi ya magonjwa na huduma nyingine muhimu.

Joto kwa watoto wa nguruwe

Watoto wa nguruwe huzaliwa bila manyoya na huwa hawana mafuta ya kutosha kuwapatia joto mwilini. Inashauriwa katika chumba cha kuzalia kuwepo na sehemu maalumu ya kuwapatia  watoto joto la ziada na kulishia.

Vyanzo vya joto la ziada vinaweza kuwa umeme au taa ya chemli. Nguruwe wadogo wanahitaji joto kiasi cha nyuzi joto 28-32°C katika wiki ya kwanza.

Makala hii imeandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kitengo cha elimu kwa wafugaji. Pia unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa mifugo kutoka SUA Augustino Chengula kwa simu +255767605098.

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

14 maoni juu ya “Fahamu maandalizi muhimu kabla ya nguruwe kuzaa

  1. Mimi ni Mfugaji Mdogo wa Nguruwe Hybrid .ninao 15 napenda kujifinza zaidi .Mawasiliano kupitia email Yangu

  2. Nimeanza ufugaji wa nguruwe 3.nitapenda kuwasiliana nanyi sana kila mara kwa ushauri

    1. Habari,
      Karibu sana Mkulima Mbunifu na hongera kwa hatua njema uliyoanza. Kuhusu ushauri, usisite kuwasiliana nasi wakati wote tupo tayari kukusaidia. Unaweza pia kutupigia simu ya mkononi kwa namba 0717 266 007

  3. Mimi ndo nmeanza ufugaji wa nguruwe kwa mara ya kwanza kabisa ningependa kujifunza mengi zaidi kuhusu nguruwe

    1. Habari, karibu sana Mkulima Mbunifu.

      Ungependa kufahamu nini juu za ufugaji wa nguruwe? Karibu

    1. Habari. Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kueoma makala za jarida hili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *