- Kilimo, Mimea

Vijana wanaweza kujifunza mengi kutokana na ubunifu kwenye kilimo hai

Sambaza chapisho hili

Kilimo hai kinafanyika kwa ufanisi na manufaa endapo wakulima wenyewe wanafanya ubunifu kulingana na mazingira yao. Ili kilimo hai kiwe endelevu ni muhimu ubunifu kutoka kwa vijana kutiliwa mkazo.

Vijana wanauwezo wa kufanya kilimo kwa ufanisi

Kilimo kwa kutumia mifuko (viroba)

Kilimo cha kutumia mifuko (viroba), ni kilimo kizuri na chenye manufaa kwa wakulima, kwani unaweza kulima sehemu yeyote pasipo kuathiri mazingira. Watu wengi wanakijua kilimo hiki kama (kilimo cha nyumbani au harufani).

Namna ya kulima kwa kutumia mifuko (Viroba)

Kwanza kabisa kabla ya kulima kwa kutumia mifuko, mkulima anatakiwa kuwa na mahitaji yafuatayo:

  • Mifuko (viroba)
  • Udongo wenye rutuba nzuri
  • Mbolea
  • Maji (hutegemeana na msimu wa mvua)

Jinsi ya kuandaa

Baada ya kuwa na mahitaji muhimu yanayohitajika kwaajili ya kilimo cha mifuko, mkulima anatakiwa ajue na kuelewa jinsi ya kuandaa kilimo cha mifuko.

Chukua ndoo moja ya udongo lita kumi (10) weka kwenye kiroba chako, vikombe 2 – 4 vya mbolea changanya udongo vizuri kisha mwagilia maji kuruhusu mbolea kuoza, fanya hivyo kwa idadi ya mifuko iliyopo, baada ya mchanganyo huo subiri kwa siku 7-14, kabla ya kupanda kuruhusu mbolea kuoza.

Muhimu:

  • Matumizi ya mbolea (2-4) yanategemeana na hali ya rutuba ya udongo, unaweza kutumia kikombe kimoja tu cha mbolea ikiwa udongo wako ni mzuri.
  • Acha kwa siku 7-14 kabla ya kupanda itategemeana na aina ya mbolea ambayo mkulima atachagua kutumia. Mbolea ya kuku pamoja na mbuzi inaoza vizuri kwa kipindi cha siku (7-14), mbolea ya ng’ombe huchelewa kuoza  kwani huchukua hadi siku 91, mbolea inayotengenezwa mfano mboji (compost), E.M fertilizer panchagavia na bustatea manure’’) unaweza kutumia wakati wa kupanda.

MUHIMU: Zingatia siku, kwani mbolea wakati inaoza hutoa joto ambalo huweza kusababisha mimea kuungua.

Jinsi ya kupanda kwenye mifuko

Baada ya kujua namna ya kuandaa kilimo cha mifuko, mkulima anatakiwa ajue jinsi ya kupanda kwenye mifuko. Unaweza kupanda kwa njia ya moja kwa moja kwa kutumia mbegu au kupandikiza mmea.

Mazao yanayolimwa kwenye kilimo cha mifuko

Mazao yanayo stawi kwenye mifuko ni mazao yote isipokua yale tu ambayo mizizi yake ni mirefu mfano miembe, mipera, miparachchi.

Mazao yafutayo yanastawi vizuri kwenye kilimo cha mifuko.

  • Chainizi
  • Mnavu
  • Sukuma wiki
  • Maboga
  • Nyanya
  • Nyanya chungu
  • Biringanya
  • Bamia
  • Kabichi
  • Tangawizi

Faida za kilimo cha mifuko

  • Utunzaji wa mazingira
  • Huongeza uzalishaji wa mazao kwa kutumia eneo dogo
  • Kuhakikisha matumizi mazuri ya kiwango cha mbolea kinachohitajika kwa mmea.
  • Kupunguza adha ya magonjwa, magugu na ukosefu wa rutuba kwa mimea.
  • Ni kilimo rahisi kufanya kwa gharama nafuu.
  • Hupunguza gharama na muda wa palizi

Trei ya asili (Maganda ya mayai)

Mwanafunzi Rajabu Mbaya ameweza kutumia njia ya asili ya kusia miche kwenye maganda ya mayai (egg shell).

Mahitaji: Maganda ya mayai, udongo na mbolea (mboji).

Changanya udongo na mbolea ya mboji alafu weka kiasi kwenye ganda la yai kisha mwagilia maji kidogo na usie mbegu.

Njia hii inamanufaa kwa mkulima mdogo kwasababu zifuatazo:

  • Gharama yake ni nafuu
  • Upatikanaji wa maganda ya mayai ni rahisi sana
  • Husaidia mmea kukua kwa haraka
  • Inasaidia kupunguza athari za kukatika kwa mmea kipindi unapotoa kwenye kitalu na kupeleka shambani kwa lengo la kupanda.
  • Ni rahisi sana kuzuia wadudu na magugu kwenye kitalu.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya mboji

Mbolea ya mboji hutokana na mabaki ya majani na miti. Majani na miti yanapooza hugeuka na kutengeneza virutubisho ambavyo husaidia kurutubisha udongo na kupunguza gharama.

Mbolea ya mboji ina madini yanayosaidia kuyeyusha madini mengine yaliyo kwenye udongo na kufanya yapatikane zaidi kwa ajili ya mimea kwa muda mrefu. Vijidudu ambavyo hujilisha kwa njia ya mbolea ya mboji kwa muda mfupi hushikilia udongo pamoja, na kuufanya udongo uwe bora na wenye afya.

Mahitaji: Nyasi kavu, Mbolea ya ng’ombe, mabaki ya chakula, udongo, vijiti vidogo vinavyoweza kuoza na maji.

 

Hatua:

  • Andaa eneo kwa kulisafisha kisha mwagia maji.
  • Panga vijiti hidogo vinavyoweza kuoza chini alafu weka nyasi kavu na umwagie maji. kama utatumia nyasi mbichi usimwagie maji,
  • Weka mbolea ya ngombe kavu, pamoja na mabaki ya vyakula
  • Weka udongo kisha mwagia maji
  • Rudia hizo wahatua hadi ifikie kiwango cha mbolea unachohitaji.
  • Juu malizia kwa kuweka nyasi kavu alafu mwagilia maji.
  • Chomeka kijiti ambacho utatumia kupima joto kwenye mbolea yako.

Acha kwa muda wa siku 21 wakati ukinyunyizia maji kila siku kulingana na hali ya hewa.  Ikifika siku ya 21 unaweza kugeuza kwa mara ya kwanza. Alafu utanyunyizia tena maji na kuacha kwa muda wa siku tano na kugeuza tena. Utakua ukigeuza hadi pale mchanganyako huo utakapoiva na kua kama udongo, ndipo mbolea yako itakua tayari kwa matumizi shambani.

Matuta ya kina kirefu (Double dug)

Hii ni mbinu ya bustani inayotumiwa kuongeza hewa kwenye udongo. Inajumuisha kufunguliwa kwa tabaka mbili za udongo, na kuongeza ya kikaboni. Kuchimba mara mbili hufanyika wakati wa kutengeneza bustani mpya, au wakati mchanga wa juu unahitajika.

Mahitaji

  1. Nyasi kavu au mbichi
  2. Mbolea ya ng’ombe mbichi
  3. Mabaki ya vyakula

Jinsi ya kufanya

  1. Safisha shamba
  2. Pima ukubwa wa matuta unaouhitaji
  3. Chimba udongo wa juu na kuutenga pembeni (Top soil)
  4. Utachimba udongo wa chini na kuutenga pembeni (sub soil)
  5. Chimba tuta urefu wa mita moja (1m) kwenda chini
  6. Weka nyasi kwanza, kisha mbolea mbichi ya ng’ombe ikifuatiwa namabaki ya vyakula na vitu vinavyoweza kuoza
  7. Baada ya hapo utaweka udongo wa juu (top soil) ulioutenga na uchanganye na mbolea ya ngombe kisha funika shimo kwa udongo kutengeneza tuta.

Tuta lako litakua tayari kwa kupanda mazao kufuatana na mahitaji yako.

Faida za Matuta ya kina kirefu: Njia hii husaidia kuufanya udongo ukae na rutuba kwa muda mrefu  na husaidia kuzalisha mazao yenye ubora bila gharama

Pancha Gavya (mbolea pia ni dawa ya kufukuza wadudu)

Mahitaji

  • Maziwa fresh lita mbili (2lt)
  • Mtindi lita mbili (2lt)
  • Samli nusu (1/2) kilo
  • Mkojo wa ng’ombe
  • Mbolea mbichi ya ng’ombe

Jinsi ya kuandaa:

  • Changanya mkojo na mbolea mbichi ya ng’ombe ikae kwa siku tatu (3) bila kuchanganywa.
  • Ongezea maziwa ya mtindi na samli changanya alafu koroga asubuhi mara moja na jioni mara moja.
  • Koroga mchanganyiko huo kila siku kwa muda wa siku kumi na tano (15) alafu itakua tayari kwa matumizi.

Jinsi ya kutumia mchanganyiko huo kama dawa ya kufukuza wadudu (Insect repellant)

Changanya lita 97 za maji na lita 3 za pancha gavya kisha weka kwenye  pampu na upulize kwenye mimea.

Inaweza kutumika kama mbolea shambani na pia inaweza kutumika kuongeza virutubisho katika chakula cha samaki, kuku na ngombe pia.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na mkuu wa chuo, Simu 0754274392 Mwl. Simu: 0753245198, chuo cha kilimo na maliasili CANRE, S.L.P 6875

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

14 maoni juu ya “Vijana wanaweza kujifunza mengi kutokana na ubunifu kwenye kilimo hai

    1. Habari Geofrey

      Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za MkM.

      Tupo kwa ajili yako.
      Karibu

    2. Natamani sana kuwa napata nakala za jarida zenu kila mwezi.
      Kweli,napenda pia kupata taarifa za vifaa vya kilimo

      1. Habari David
        Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za Mkulima Mbunifu.
        Kuhusu kupata jarida letu, unaweza kujisajili ili kupokea kwa njia ya tovuti au email, lakini pia kama una kikundi cha wakulima/wafugaji kuanzia watu 5 kwenda juu, unahitajika kututumia jia la kikundi chako, maji ya viongozi na namba za simu, idadi ya wanakikundi, na sanduku lenu la posta kwani yanatumwa kwa njia ya posta.

        Ni muhimu pia kutujulisha kuwa mnashughulika na nini hasa.

        Karibu Mkulima Mbunifu

        1. Habari, Karibu sana Mkulima Mbunifu. Je, upo na kikundi cha wakulima ama ni wewe peke yako? Kama ni wewe peke yako tunaomba ututumie email (barua pepe) yako nasi tutakutumia kila wakati makala inapokuwa tayari. Karibu sana MkM

  1. Ni mefurahi sana kuona aina na njia tofauti za ubunifu ambazo zinafuata sifa na wajibu wa kilimo endelevu nmefurahi sana kwa hili
    Mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa pili ambae Nasomea fani ya kilimo Katika chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) pia ni mjasiria malia ambae najishughulisha na shughuli tofauti za kilimo

    1. Karibu sana Mkulima Mbunifu

      Tuko tayari kusaidiana na kushirikishana pale tunapoweza kwa lengo la kuhakikisha unafikia malengo yako.
      Karibu

  2. Natamani sana kuwa napata nakala za jarida zenu kila mwezi.
    Kweli,napenda pia kupata taarifa za vifaa vya kilimo na kazi zake pamoja na bei yake ya kila kimoja.

    1. Habari, Karibu sana Mkulima Mbunifu
      Unahitaji kuwa unayapokea kwa njia gani? Lakini pia ni taarifa ya vifaa gani unahitaji japo sisi hatuuzi bidhaa wa kifaa cha aina yeyote zaidi ya kutoa elimu kwa njia ya majarida ya kila mwezi.

      Karibu sana

  3. Mimi ni kijana ninayetaka kuanzisha kilimo cha mbogamboga kwenye viroba.. nawashukuru sana kwa nakala hii.nmejifunza mambo muhimu ambayo mwanzo ckuyajua.
    Asante Sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *