- Kilimo, Mimea

Mapapai bora hupelekea soko lenye tija

Sambaza chapisho hili

Mapapai ni zao moja kati ya mazao ya matunda yenye vitamin A na madini ya kalsiamu kwa wingi na zao hili hulimwa karibu kila mahali hapa nchini kwa wastani wa tani 2,582 kwa mwaka.

Ili kuweza kuzalisha zao la papai kwa wingi na kwa ubora unaotakiwa ni muhimu kuhakikisha unazingatia kanuni zote za kilimo bora za uzalishaji wa mapapai. Ubora wa matunda baada ya kuvunwa hutegemea jinsi yalivyozalishwa

Papai bora hutokana na kilimo kilichofuata kanuni sahihi za uzalishaji

Fanya uchaguzi bora wa aina za papai

Katika uzalishaji wa papai, ni muhimu kuhakikisha unachagua aina iliyobora yenye sifa zifuatazo;

  • Chagua aina bora ya kupanda kulingana na uhitaji wa soko
  • Hakikisha aina utakayoichagua inamudu udhibiti wa wadudu, magonjwa pamoja na magugu.
  • Mapapai hushambuliwa kwa urahisi na magonjwa na wadudu hivyo ni muhimu kuhakikisha unafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kugundua dalili za mashambulizi.
  • Endapo kuna dalili za mashambulizi, dhibiti mapema ili kuzalisha mazao bora yanayoweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
  • Hakikisha shamba na barabra zake ni safi wakati wote ili krahisisha uvunaji pamoja na usafirishaji.

Maandalizi kabla ya kuvuna

Kagua shamba ili kuona kama kuna mapapai yaliyokomaa. Mapapai hukomaa katika kipindi cha miezi mitano kutoka maua yanapochanua.

Dalili za kukomaa

Tunda hubadilika rangi kutoka katika ukijani kibichi na kuwa na kijani nyepesi hadi manjano.

Vifaa kwa ajili ya kuvunia

Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kuvuna mapapai ni pamoja na vichumio, mifuko na ngazi.

Vifaa vya kufungashia

Ili kufungasha mapapai kwa usahihi vifaa vinavyohitajika ni makasha ya mbao, au plastiki au hata makasha ya makaratasi magumu.

Vyombo vya kusafirishia

Mara baada ya kuvuna mapapai ni lazima kusafirisha katika hali yenye ubora kwa kutumia vyombo kama vile mikokoteni, magari pamoja na matela ya matrekta.

Namna ya kuvuna

  • Uvunaji bora wa mapapai ni wa kutumia mikono ambapo tunda huchumwa kwa mkono kwa kutumia kichumio.
  • Vuna mapapai yaliyokomaa tu na vina papai pamoja na kikonyo chake.
  • Vuna wa uangalifu ili kuepuka kudondosha chini matunda.
  • Matunda yakidondoka huchubuka, huoasuka na hupondeka hivyo husababisha upotevu.
  • Weka mapapai yaliyovunwa kivulini mara tu baada ya kuyavuna.

Kuchambua

Ni muhimu kuchambua mapapai ili kutenga yaliyooza, kupasuka na yenye dalili za magonjwa au kubonyea. Lengo la kuchambua ni kupata matunda yenye ubora kulingana na matumizi kwa mfano kusindika, kuuza au kusafirisha.

Matunda yaliyooza na yenye wadudu ni vyema yafukiwe ili kuangamiza wadudu waharibifu na vimelea vya magonjwa na pia kuzuia kuenea kwa wadudu na magonjwa hayo.

Matunda yaliyopasuka, kubonyea au kuchubuka kidogo yatumike haraka kwa kuliwa.

Matunda mazuri ambayo hayatapata madhara yeyote yatumike kwa ajili ya kusindika, kuliwa, kuuzwa au kusafirishwa.

Kusafisha

Baada ya kuchambua safisha mapapai kwa maji safi na salama ili kuondoa uchafu wa masalia ya madawa.

Baada ya kusafisha, yatumbukize mapapai kwenye maji ya moto yenye nyuzi joto lipatalo 49 za sentigredi kwa muda wa dakika 20. Maji ya moto husaidia kuua mayai ya viwavi vya wadudu waharibifu wanaoweza kushambulia matunda wakati wa kuhifadhi au kusafirisha.

Muhimu: Mapapai hulainika na kubadilika ladha endapo joto la maji litazidi nyuzi 49 za sentigredi zilizoshauriwa.

Kupanga madaraja

Madaraja hutakiwa kupangwa kwa lengo la kurahisisha ufungashaji, usafirishaji na uuzaji kwa bei ya juu.

Unatakiwa kupanga madaraja ya mapapai kwa kufuata ubora ambavyo vigezo vyake hutegemea matakwa ya mteja.

Vigezo vya ubora vinavyohitajika ni kama vile ukubwa wa tunda, umbo, rangi, aina na uivaji.

Kufungasha

Fungasha mapapai kwenye makasha ili kuzuia yasichubuke, kubonyea au kupasuka wakati wa kusafirisha.

Tandika makaratasi ndani ya makasha ya mbao kabla ya kupanga matunda ili kuzuia kuchubuka kwa matunda.

Hakikisha maksha yana nafasi ya kuruhusu mzunguko wa hewa na kila kasha lisizidi kilo 20 ili kurahisisha ubebaji.

Kuhifadhi

Hifadhi mapapai kwenye vyumba vyenye nyuzi joto 10 hadi 20 za sentigredi na unyevu upatao asilimia 85 hadi 95.

Matunda yaliyohifadhiwa katika hali hiyo huweza kudumu kwa muda wa wiki moja bila kuharibika, hasa kama yalikuwa yamekomaa vizuri, kuvunwa vizuri na kutokuwa na michubuko.

Makala hii ni kwa hisani ya Wizara ya ilimo na chakula, Idara ya usalama wa chakula. Kwa maelezo zaidi wasiliana na Lucy Mvungi kwa simu namba 0755 565 621

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *