- Binadamu, Kuku, Mifugo

Tumia mayai ya kuku kuimarisha afya ya mama na mtoto

Sambaza chapisho hili

Mayai nichanzo kizuri cha protini ambayo ni muhimu kwa kujenga tishu za mwili. Mayai yana vitamini na madini kadhaa, ikiwa ni pamoja na choline, ambayo ni nzuri kwa ukuaji wa ubongo wa mtoto. Pamoja na faida za kula mayai, usile mayai mabichi au ambayo hayajapikwa yakaiva vizuri.

Ikiwa lengo kubwa la kilimo na ufugaji ni kuhakikisha usalama wa chakula kwa familia nzima na nchi kwa jumla wakati ambapo eneo la kulima ama kulishia mifugo linaendelea kuwa dogo wanyama wadogo kama vile kuku ni chanzo muhimu wa lishe bora kwa familia nzima, hasa watoto na akina mama.

Mchango wa kuku kupitia uzalishaji wa mayai kwenye lishe ya familia

Kuku wanafugwa na jamii nyingi nchini; ni ngumu kupata kaya ambayo haifugi kuku. Hii ni kwa sababu ni ndege anayehitaji eneo na mtaji mdogo kufuga, na anasifika kwa nyama na mayai ambayo ni chakula na pia kuku anaweza kuuzwa kwa haraka ili kugharamia mahitaji kadhaa.

Virutubisho kwenye yai

Virutubishi vinavyopatikana kwenye yai vina faida lukuki kwa ukuaji wa mtoto aidha akiwa tumboni na hata baada ya kuzaliwa.

Wakati na baada ya ujauzito, mtoto anakua kwa kasi sana na anahitaji virutubishi kwa ugavi unaotosha na kwa viwango vinavyoongezaka kulingana na umri. Virutubishi hivi ambavyo vinapatikana kwenye yai ni pamoja na protini, mafuta, vitamini A, B12, B6, choline, madini ya folate, fosforasi, selenium, chuma na zinki.

Kutokana na mchanganyiko huu wa virutubishi, mayai yanaweza kuboresha afya ya mama mjamzito, lishe ya mtoto, hasa ukuaji wake wa ubongo. Ikilinganishwa na vyanzo vingine vya protini kama vile nyama, mayai hutoa virutubishi vinavyoweza kuchukuliwa kwa urahisi na kutumiwa na mwili wa binadamu.

Viwango vya matumizi

Kwa watoto kati ya miezi 7-12, yaani wale ambao wameanza kupewa chakula cha ziada mbali na maziwa ya mama, yai moja kwa siku linachangia maradufu. Shirika la Afya Duniani (WHO), linashauri kuanzisha mayai kwenye lishe ya mtoto katika mwezi wa sita baada ya kuzaliwa. Yai moja linaweza kutosheleza takriban asilimia hamsini (50% – yaani nusu) ya hitaji la protini kwa siku moja.

Chemsha yai zima, kisha usage au kupigapiga liwe laini kabisa ili kuwa rahisi kumeza. Hii pia inategemea umri au hatua ya ukuaji wa mtoto. Epuka kuongeza chumvi au vitoweo vingine. Ili kuepuka matatizo yoyote, unaweza kujaribu kuanzisha yai lililopikwa kwenye mlo wa mtoto wako polepole; kwa viwango vidogo-vidogo. Kwa watoto wakubwa, mayai ya kuchemsha hukatwa yakawa vipande vidogo vinavyoweza kuchukuliwa kwa vidole, inakuwa rahisi mtoto kuchukua na kuweka mdomoni.

Kwa mama mjamzito na yule anayenyonyesha, mayai mawili kwa siku yataimarisha upatikanaji wa virutubisho na madini muhimu, na inachangia takriban asilimia thelathini (30% – yaani theluthi moja) ya mahitaji ya protini kwa siku hasa inapochanganywa na vyakula vingine. Utumiaji huu unategemeana sana na upatikanani wa mayai.

Kwa watoto wanaokwenda shuleni, yanapoliwa kama kiamsha kinywa, mayai yanaweza kuongeza kiwango cha shibe cha mtoto. Hii inapunguza njaa katika siku nzima ya shule yenye shughuli nyingi, na hivyo kupunguza hitaji la mtoto kula vyakula visivyofaa hasa vyenye sukari nyingi na vyenye mafuta mengi.

Kwa nini ulaji mdogo?

Hata hivyo, kiwango cha ulaji wa mayai ni cha chini miongoni mwa wanawake walio katika umri wa kuzaa na watoto wadogo chini ya miaka mitano. Vikundi hivi vinahitaji viwango vya juu vya lishe hasa protini, vitamini na madini.

Baadhi ya sababu ambazo zinazuia ulaji wa mayai ni pamoja na;

  • Kuna sababu za kitamaduni ambazo huchangia katika mazoea mengi ya lishe katika kaya, ikiwa ni pamoja na dhana kwamba si vyema kuwalisha watoto mayai, eti kwamba itachelewesha uwezo wao wa kuzungumza. Nyingine ni kwamba mama akiwa mjamzito akila mayai basi mtoto atakuwa mkubwa sana na kuleta matatizo wakati wa kujifungua kuzaliwa.
  • Upatikanaji mdogo unaotokana na uzalishaji mdogo au utagaji wa mayai kwa ajili ya kushughulikia mahitaji mengine katika familia.
  • Uzalishaji wa mayai ya kuku na upatikanaji wa chakula msimu wote wa mwaka pamoja na magonjwa. Mfugaji anatakiwa kutambua kuwa, kuku wachache kwa ajili ya matumizi ya familia wanaweza kulishwa kwa kutumia mabaki ya vyakula na yale ya jikoni.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *