- Mifugo

Je, unafahamu umuhimu wa njia za moto?

Sambaza chapisho hili

Hivi karibuni tumeshuhudia uwepo wa mlipuko wa moto katika sehemu mbalimbali hapa nchini, na katika nchi nyingi duniani. Hii inatokana na mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji hafifu wa mazingira yetu.

Ni jambo lisilopingika kuwa wakulima wamekuwa na bidii sana katika kuhakikisha kuwa wanazalisha na kupata chakula pamoja na kipato kwa ajili ya familia zao.

Halikadhalika wakulima wamekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira, jambo linalofanya mashamba yao kuwa nadhifu na uzalishaji ulio bora.

Pamoja na hayo, changamoto hazikokosekani kwani si wote wanaofanya kwa kiwango kinachotakiwa na wengine hawafuati kanuni zinazoainishwa kitaalamu ili kuweka mazingira salama wakati wote na kuepuka athari kama za moto hasa wakati wa kiangazi.

Kutokana na hali hiyo, mlipuko wa moto umekuwa ukiathiri mashamba na kfanya upotevu wa mazao mara kwa mara, halikadhalika upotevu wa rasilimali nyinginezo kama vile miti, lakini pia upotevu wa viumbe hai muhimu kwa mazingira yetu.

Kwa kutambua hilo, MkM tumekuandalia makala hii ambayo itakuwezesha kufahamu umuhimu wa njia za moto katika mashamba yetu, na kwenye mazingira yetu, ili kuweza kukabiliana na janga la moto pindi linapotokea.

 

Njia za Moto ni nini?

Hii ni nafasi iliyopo kati ya uoto au vitu vinavyoweza kuwaka/kushika moto na inayoweza kuzuia au kupunguza uwezekano wa moto kushika au kuwaka.

Njia za moto hutumika kuyalinda mashamba ya mazao yanayowaka haraka kama vile ngano, ulezi, mtama na miti hasa ya miti inayopandwa kama mipaina/pines, milingoti/mikaratusi na aina nyingine za miti.

Mambo ya kuzingatia!

  • Hakikisha kuwa umbali wa njia ya moto angalau iwe na upana wa mita 5 kwa njia ndogo za kutenganisha kitalu(ploti) kimoja na nyingine zisizozidi ukubwa wa heka 10.
  • Njia za moto zinazotenganisha shamba moja na jingine ziwe na njia za moto zenye upana wa mita 10 na zaidi ili kuzuia moto kuhama kirahisi.
  • Zingatia muda muafaka wa kutengeneza njia za moto ambapo mara nyingi ni wakati wa palizi/kupalilia.
  • Ondoa nyasi au miti iliyoota kwenye njia za moto na palilia tena wakati wa kiangazi hasa kuanzia mwezi Juni na Julai ili kuhakikisha zipo safi na salama kwa kuzuia moto.

Njia hizi zinapokuwa safi, moto hauwezi kuvuka kutoka kitalu kimoja kwenda kingine, kwani kutokuwepo na visaidizi kama vile nyasi na majani makavu hufanya moto usisambae.

 

Aina za njia za moto

  1. Njia za moto za asili: Njia za moto zinaweza kuwa za asilia, sehemu ambazo hazina uoto au vishikamoto kama vile mito, ziwa au mkondo wa maji.
  2. Njia za moto za kutengenezwa: Hizi zinaweza kuwa njia za kutengenezwa na binadamu na nyingi ya njia hizi zinaweza kutumika kama barabara za kutenganisha mashamba ya miti, barabara za kuvunia miti au barabara za njia kuu.

Aina ya njia za uzuiaji wa moto kwenye shamba la miti

  1. Uzuiaji wa Moto nje ya shamba
    Uzuiaji wa moto nje ya shamba ni njia muhimu na yenye tija katika kulinda mashamba ya miti kutokana na moto kichaa. Maeneo mengi ya nje ya shamba la miti yamezungukwa na uoto wa asili kama vile nyasi pori, miti ya asili, hifadhi za maliasili na mazao mengine ya kilimo. Njia nzuri na inayofaa kwa zoezi hili hutokana na aina ya mazingira yaliyolizunguka shamba, pia vifaa vinavyotumiwa kwa kazi hiyo.

Njia zifuatazo zinaweza kutumika kutengeneza njia za moto;

  • Uchomaji moto wa nyasi au uoto unaolizunguka shamba.
  • Kupanda miti iayoweza kuzuia moto kuzunguka shamba.
  • Kulima njia za moto kwa upana usiopungua mita 5/ miguu 5 au futi 16.
  • Kuvuta na kutoa nyasi ndani ya njia za moto.
  • Kukwangua barabara na mipaka ya mashamba.
  1. Uzuiaji wa Moto ndani ya shamba

Ni muhimu kwa mkulima kuhakikisha kuwa anapunguza au kuzuia kabisa madhara ya moto ndani ya shamba la mazao na miti kuliko kutegemea njia za moto iwapo moto utaanzia ndani ya shamba.

 

Moto unaweza kuanzia ndani ya shamba la miti na hapa utengenezaji wa njia za moto za ndani unahitajika zaidi. Jambo hili linahitaji uangalizi mkubwa na linaruhusiwa kwenye mashamba yenye eneo dogo tu.

 

Unashauriwa kulima njia za moto ndani ya shamba, kusafisha mipaka ya shamba, kuchoma nyasi/uoto pembezoni mwa maeneo yenye unyevu/maji kama mito au mabwawa.

 

Pia unaweza kuchepusha maji yanayotembea kama yapo ili kuweza kusaidia kuzuia na kuzima moto. Kuondoa na kuhamisha miti au uoto pia kunasaidia kuzuia moto ndani ya shamba la miti.

Kwanini ni muhimu kuweka njia za moto?

  • Kuzuia uwezekano wa moto kusambaa kwenye mashamba mengine.
  • Kupunguza nguvu ya moto uliolipuka.
  • Kulinda uoto wa misitu na kupunguza madhara ya uchafuzi wa hali ya hewa.
  • Jingine kubwa na muhimu kwa mkulima au mmiliki wa shamba la mazao au miti ni kulinda miti ili kuongeza pato lake kutokana na biashara ya mazao ya na miti.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *