- Mifugo

Kilimo bora cha kabeji ya kichina 

Sambaza chapisho hili

Kabeji ya kichina kwa miaka mingi ilikuwa inalimwa na kuliwa sana katika nchi za China, India na Japani. Ikijulikana kwa majina ya common choy, pak choy na gai choy au Indian mustard.

Miaka ya karibu mboga hii ya majani imepata umaarufu katika nchi yetu na hulimwa kwa ajili ya kuboresha lishe na kama zao la biashara, lijulikanavyo katika maeneo mengi kwa kifupi kama chainizi.

Aina za kabeji za kichina

Common choy; shantung cabbage or mchihili

Aina hii ni bora sana na hulimwa hapa nchini. Ubora wake unatokana na ulaini wa majani yake, majani hayana vinyweleo kama aina zingine pia ina ladha inayowavutia walaji wengi.

Gai choy or Indian mustard

Aina hii ina harufu kali kuliko aina zingine za kabeji za kichina, majani yake ni mapana na kijani zaidi na majani hayafungi na kutengeneza vichwa.

Pak choy or Chinese cabbage

Aina hii huzaa majani machache, haifungi na kutengeneza vichwa, vikonyo vya majani ni vinene.

Hali ya hewa

Kabeji ya kichina hustawi vizuri katika maeneo mengi ya Tanzania yenye mwinuko usiozidi mita 1500 toka usawa wa bahari. Kabeji ya kichina hustawi vizuri sehemu zenye joto la wastani. Joto ridi la chini ya sentigredi 16 huwezesha utoaji wa maua mapema.

Udongo

Kabeji ya kichina hustawi vizuri kwenye udongo wa aina mbalimbali usiotuamisha maji. Hustawi vizuri kwenye udongo tifutifu wenye mboji nyingi. Udongo wa kichanga hudumaza ukuwaji wa kabeji ya kichina.

Upandaji wa zao hili (Chinese cabbage)

Mbegu za kabeji ya kichina huoteshwa kitaluni au moja kwa moja shambani. Uoteshaji kitaluni ni mzuri kwa sababu ya kutumia mbegu kidogo na huudumiaji huwa rahisi katika hatua za mwanzo.

Upandaji wa kabeji ya kichina moja kwa moja shambani huambatana na utumiaji wa mbegu nyingi katika kila kishimo kitakacho chimbwa pia upunguziaji wa miche na kuacha mche mmoja katika kila kijishimo.

Kitalu

Kitalu ni muhimu katika uzalishaji wa zao la kabeji ya kichina kwani kuna faida nyingi ziletwazo na kitalu. Tengeneza matuta yenye upana wa mita moja na urefu wowote kulingana na mahitaji yako ya miche. Changanya mbolea ya asili katika kila tuta kabla ya kusia mbegu.

Pia viriba vinaweza kutumika kama vitalu vya zao hili ili kupata miche bora zaidi. Mbolea ya samadi ni vizuri iweimeoza na kupoa kabla ya kuisambaza katika matuta ya kitalu. Mboji iliyotengenezwa kitaalam inafaa kusambazwa kitaluni.

Kusia mbegu za kabeji ya kichina

  • Tengeneza vifereji kukatiza tuta kwa umbali wa sentimita 15
  • Sia mbegu za kabeji ya kichina ndani ya vifereji hivyo kwa mtawanyiko mzuri yaani usio songamanisha mbegu hizo.
  • Fukia mbegu hizo kwa kutumia udongo laini
  • Kandamiza kiasi (firming) ili mbegu zishikane na udongo vizuri
  • Funika matuta yaliyosiwa mbegu kwa matandazo ya nyasi au majani makavu
  • Mwagilia maji juu ya matandazo hayo kwa kutumia keni (watering can) yenye matundu madogo.
  • Nyweshea kitalu chako mara moja au mbili kwa siku kulingana na hali ya hewa ya eneo hilo
  • Mbegu za kabeji za kichina huota haraka sana yaani siku 3 hadi 5 hivyo ondoa matandazo mara mbegu zitakapo ota.

ZINGATIA:

Sehemu yenye jua kali unaweza ukajenga kichanja ili kuipa miche michanga kivuli.

Kukomaza miche (hardening off)

Kabla ya kupandikiza miche shambani unaweza kukomaza miche iliianze kuzoea mazingira ya shamba kwa kupunguza umwagiliaji wa maji mara kwa mara, pia kuipunguzia miche kivuli cha kichanja taratibu taratibu.

Kupandikiza miche shambani

Miche ya kabeji ya kichina huanza kupandikizwa wiki 3-4. Ukichelewa kupandikiza miche hukomaa na hutoa mavuno kidogo na pia husongamana kitaluni.

  • Andaa shamba mapema kabla ya upandikizaji kuanza
  • Mwagilia shamba maji ya kutosha siku moja kabla ya shughuli ya upandikizaji kuanza
  • Tayarisha mashimo ya upandikizaji kwa umbali wa sentimita 40 mstari hadi mstari na sentimita 30 mche hadi mche.
  • Weka mbolea ya mboji ya kutosha kiasi cha viganja viwili katika kila shimo
  • Changanya mboji na udongo kabla ya kufukia shimo
  • Fukia shimo kiasi kwa kuacha sehemu ya kupandikizia miche
  • Ng’oa miche na pandikiza kwa umakini

Zingatia

  • Usifukie majani ya miche yako
  • Mizizi isijikunje bali itawanyike.
  • Usikate mizizi wakati wa kupandikiza.

Visumbufu vya kabeji ya kichina

Wadudu- Kabeji ya kichina huvunwa baada ya siku chache hivyo hupunguza mashambulizi makali ya wadudu kama:-

  • Vidukari
  • Vithiripi
  • Nzi weupe
  • Sota
  • Funza wa mizizi

Magonjwa

Yapo magonjwa yanayoshambulia zao hili kama:-

Muozo mweusi (black rot), Muozo laini (soft rot), Ubwiri poda (powdery mildew), Madoa meusi (black spots), Kinyaushi (damping off), Batobato (mosaic virus)

Muhimu

Magonjwa na wadudu wa kabeji ya kichina huzuilika kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha mboga.

Mfano;

  • Tumia mbegu zilizothibitishwa kitaalam
  • Usafi wa shamba
  • Kufuata mzunguko wa mazao
  • Umwagiliaji maji kwa usahihi
  • Na uvunaji kwa wakati

Mavuno

Kabeji ya kichina huvunwa kwa njia kuu mbili:-

  1. Uvunaji wa kung’oa njia hii hutumika kwa aina inayofunga na kutengeneza vichwa.
  2. Uvunaji wa kukata majani- huvunaji huu ni kwa ajili ya kabeji ambazo hazitengenezi vichwa. Uvunaji wa kukata majani ni rahisi kwa kutumia mikono kwa kukandamiza kikonyo cha jani chini kisha peleka kushoto kulia hadi jani livunjike sehemu yake iliyoshika shina.

ZINGATIA:

  • Usiache vikonyo vya majani yaliyovunwa vikabaki kwenye mashina kwa sababu hudumaza ukuwaji wa mmea.
  • Vuna majani yaliyotayari wakati wa asubuhi kabla ya mmea kupoteza maji kwa sababu ya jua kali.
  • Kabeji ya kichina inauwezo wa kutoa tani 3-8 kwa ekari moja.

Muhimu

  • Aina zinazovunwa majani hutoa mavuno mengi zaidi kuliko zile zinazotoa vichwa
  • Uvunaji huanza baada ya siku 50-80 tokea kusia mbegu.

Imetayarishwa na Suleiman Mpingama (mtaalamu wa kilimo), simu namba, 0685 460300 au 0763 551259, barua pepe mpingama@yahoo.com

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *