- Kilimo, Kilimo Biashara, Mazingira, Udongo

Kanuni ya haki na uangalizi katika misingi ya kilimo hai

Sambaza chapisho hili

Kama ambavyo maandalizi sahihi hufanyika katika shughuli yeyote ya kimaendeleo, katika kilimo hai pia kanuni ya haki na usawa pamoja na uangalizi visipozingatiwa vyema mkulima hawezi kufaidika na kilimo hai.

Kanuni ya haki na usawa

Kilimo hai sharti kizingatie msingi wa mahusiano yatakayohakikisha usawa katika mazingira na fursa ya kuishi.Usawa unaojali na kuzingatia heshima, haki na kujituma kwa kila mmoja wetu na mahusiano ya viumbe hai kwa ujumla.

Kanuni hii inasisitiza kuwa wale wote wanaojihusisha na kilimo hai lazima wazingatie mahusiano yenye usawa katika ngazi zote bila upendeleo.

Hii ni kwa wazalishaji, walaji, wasindikaji, wafanyakazi, wafanyabiashara na wasambazaji ili kuboresha mazingira na kuhifadhi maliasili na rasilimali. Kilimo hai lazima kifanikishe uwiano na urari wa kimazingira kwa kubuni na kuhimiza mfumo na kutunza rasilimali asilia na ukuaji wa kilimo.

Wote wanaozalisha, wanaosindika, wanaouza au kununua, kula na kutumia bidhaa za kilimo hai wanapaswa kushiriki kikamilifukatika kukinga na kuzuia uharibifu wa mfumo mzima wa mazingira unayojumuisha hali ya hewa, viumbe, bayoanuai, hewa na maji.

Kilimo hai kinapaswa kuwapatia maisha bora na mazuri wale wote wanaojihusisha nacho na kuchangia katika uhakika wa chakula na kupunguza umaskini. Malengo ya kilimo hai ni kuzalisha chakula na bidhaa za kutosha kwa kuzingatia viwango vya ubora. Kanuni inasisitiza kuwa wanyama lazima wapatiwe fursa na hali ya kimazingira inayoendana na maumbile, tabia zao za asili na hali bora.

Rasilimali za asili na za kimazingira zinazotumika katika uzalishaji au matumizi mengine ni lazima zisimamiwe vema na matumizi hayo yakubalike kuwa tija kwa jamii na ikolojia ya mazingira kwa kujali haki na urithi wa vizazi vijavyo. Mfumo wa uzalishaji, usambazaji na biashara wenye uwazi, haki na unaowajibika kwa mazingira na jamii unahitajika ili kujenga usawa na haki.

Kanuni ya uangalizi

Kilimo hai lazima kiweke tahadhari na uwajibikaji unaoweka kinga kwa afya na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo pamoja na kujali mazingira endelevu.

Mfumo wa kilimo hai unapaswa kubadilika ili kuendana na matakwa ya hali ya ndani au nje ya mazingira husika. Wanaojihusisha na kilimo hiki wanapaswa kuongeza ufanisi na tijakatika uzalishaji, pasipo kuleta athari za kiafya na ustawi kwa kufanyika tathimini na uchambuzi wa teknolojia mpya na zilizopo.

Kwa kuwa hakujafikiwa muafaka wa uelewa juu ya mfumo wa kimazingira na kilimo, tahadhari ya uangalizi lazima izingatiwe. Kanuni hii inaweka tahadhari na wajibu muhimu wakati wa kuchagua teknolojia za kilimo hai kwa kuzingatia maendeleo na mazingira endelevu.

Inatambulika kuwa sayansi ni muhimu kwa kilimo hai ili kiwe salama na bora kwa mazingira, binadamu,viumbe n.k. Hata hivyo, maarifa ya kisayansi pekee hayatoshi, ujuzi na maarifa ya asili, uzoefu, hekima, busara na ubunifu uliojengeka kwa vizazi kadhaa unahitajika kutoa suluhisho na ufumbuzi wa matatizo ya mazingira na uzalishaji.

Kilimo hai lazima kizuie athari za kimazingira na kiafya kwa kubuni na kutumia teknolojia sahihi. Pia kuzikataa zile ambazo sio endelevu na ambazo athari zake hazijafahamika bayana kama vile viini tete maarufu kama GMO.

Maamuzi ya teknolojia na pembejeo gani zitumike katika kilimo lazima yazingatie mahali na mahitaji ya wote waoweza kuathirika, hivyo ni muhimu wahusishwe katika mchakato ulio wazi na shirikishi wakati wa kuchambua na kuchagua teknolojia iliyosahihi kulingana na mazingira husika.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *