- Kilimo

Zao lenye faida kubwa kiuchumi na kiafya

Sambaza chapisho hili

Nanasi ni moja kati ya matunda ambayo yanapendwa sana na watu wa kada zote. Tunda hili halihitaji gharama kubwa ya uzalishaji, huku likiwa na bei nzuri tofauti na ilivyo kwa aina nyinginezo za matunda.

 

Nchini Tanzania, zao hili hulimwa zaidi katika  maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Geita, Mwanza, Tanga, Mtwara, Lindi, Zanzibar na maeneo mengine.

Zao hili lina kiasi kikubwa cha vitamini A na B na kiasi kidogo cha vitamini C, pia kuna madini kama potashiamu, kalishamu, chuma na magnesiamu.

Kustawi

Manansi hustawi zaidi ukanda wa pwani, kiasi cha mita 900 kutoka usawa wa bahari ambapo kuna mvua nyingi kiasi cha milimita 1500 na unyevu wa kutosha. Unaweza pia kupanda kwenye maeneo yenye mvua chache lakini kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji.

Hali joto: Joto linalohitajika kwa ajili ya ustawishaji wa nanasi ni kuanzia nyuzi joto 15 – 32 sentigredi. Kwa kawaida zao hili huwa halistahimili baridi.

Udongo

Udongo wenye rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji unafaa zaidi kwa ajili ya kilimo cha mananasi.

Mbolea

Unaweza kutumia samadi au mbole vunde ili kuongezea rutuba ya udongo wako.

Msimu

Kwa ukanda wa pwani wenye mvua mbili kwa mwaka upandaji wa mananasi huanza mara baada ya mvua za kwanza kuanza. Ni vizuri kupanda kwa muda mfupi ili uzaaji usipishane sana na pia kusaidia kupata mvua za kutosha kabla ya msimu kwisha.

Kupanda

Tumia miche ya aina moja na yenye umri sawa ili huduma zifanane na pia uzaaji uwe wa mpangilio.

Nafasi

Umbali toka mmea hadi mmea uwe sentimita 30, mstari hadi mstari uwe sentimita 60, na umbali kati ya mstari na mstari uwe  sentimita 90.

Idadi ya miche shambani

Kwa ekari moja unaweza kupanda miche 25,200 na kwa hekta moja unaweza kupanda miche 44,000.

Namna ya kupanda

Tengeneza mtaro mdogo kisha panda miche ya nanasi kwenye mitaro huo. Hii husaidia kupata unyevu wa kutosha na kufanya mananasi kustawi vizuri.

Wadudu

Wadudu wanaoshambulia mananasi ni aina ya mealybug ambao unaweza kuwaondoa kwa kunyunyizia dawa za asili au aina nyingine zisizokuwa na madhara kama itakavyoelezwa na wataalamu.

Magonjwa

Ugonjwa wa kuoza moyo wa miche unaweza kuzuiwa kwa kuzamisha miche kwenye dawa za ukungu (fungicides)kabla ya kupandwa shambani

Kuvuna

Mananasi huwa tayari kuvunwa miezi 18 mpaka 24 baada ya kupandwa kutegemeana na mbegu na matunzo, ikiwemo kiasi cha mvua, mbolea na unyevu shambani.

Uvunaji  hufanyika kwa kutumia visu na vibebeo maalum kuhakikisha ubora wa zao hili unadumu.

Matumizi

Nanasi huliwa kama tunda, na kutengeneza aina mbalimbali za vinywaji.

Pia mabaki yake hutumika kama chakula cha mifugo na matandazo shambani.

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *