- Kilimo

Utengenezaji wa makingo na umuhimu wake hasa msimu huu wa mvua

Sambaza chapisho hili

Madhumuni makubwa ya kutengeneza makingo shambani ni pamoja na kugawa au kufupisha urefu wa mteremko.

Katika kipindi hiki ambacho hutarajiwa kuwa na mvua nyingi katika maeneo mbalimbali ya nchi, ni vyema wakulima wakahakikisha wanaweka makingo ya kutosha ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na maji mengi ya mvua.

Madhumuni makubwa ya kutengeneza makingo shambani ni pamoja na kugawa au kufupisha urefu wa mteremko.

Kupanda, kulima na kupalilia kwa kukinga mteremko peke yake haviwezi kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Kwa nini ni muhimu kuwa na makingo

Makingo yanahitajika sana kwenye mashamba yaliyopo kwenye miteremko yenye udongo unaomomonyoka kwa urahisi ambapo njia za kawaida za matayarisho ya mashamba haziwezi kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Makingo hutumika kupunguza au kuzuia kabisa udongo wa juu, ambao hutengenezwa kwa chakula cha mimea usichukuliwe na maji. Makingo yakiwekwa shambani husaidia kuhifadhi udongo, rutuba na maji.

Hatua za utengenezaji wa makingo

Kama ilivyo kwa shughuli zingine za kilimo, wakati wa uchimbaji na utengenezaji wa makingo kuna hatua stahiki ambazo ni lazima mkulima kuzifuata ili kuweka makingo bora na imara.

Kupima mteremko wa shamba

Kabla ya kuanza upimaji wa makingo ni muhimu kuchunguza na kupima mteremko wa shamba au eneo linalofanyiwa hifadhi ya ardhi.

Mteremko wa shamba huchangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na maji.

Mmomonyoko wa udongo huongezeka kwa kadri mteremko unavyoongezeka na upimaji wa mteremko hufanyika kwa kutumia vifaa rahisi kama vile pima maji na line level. Asilimia ya mteremko hutumika kupata nafasi kati ya makingo.

Nafasi kati ya makingo

Kwa ujumla nafasi kati ya makingo hutegemea hali ya udongo, mteremko wa shamba na kiasi cha mvua inayonyesha katika eneo hilo.

Aidha utafiti unaonyesha kuwa, kushuka kwa mteremko kwa kiasi cha mita 1.5 kwa mteremko mkali na mita 2.0 kwa mteremko kwa mteremko wa wastani zaweza kutumika na kipimo husika pia kutumika huku upimaji ukifanyika pembeni mwa shamba kuelekea mteremko.

Hata hivyo, upimaji hufanyika kuanzia juu ya shamba kuelekea chini ya shamba na mambo hutumika kwa ajili ya kuweka alama, na alama hizi ndizo zitakazotumika kwa ajili ya kuweka makingo.

Upimaji wa makingo

Baada ya kupima nafasi kati ya makingo na baada ya kuamua aina ya makingo yanayofaa katika shamba lako, sasa upimaji wa makingo yenyewe hutakiwa kuanza.

Kwa kutegemeana na hali ya mteremko, aina ya udongo na kiasi cha mvua katika eneo husika makingo yanayomwaga maji au yasiyomwaga maji ndiyo yanayotumika.

Katika maeneo yenye mvua za wastani na udongo unaonyonya maji kwa urahisi makingo yasiyomwaga maji hutumika zaidi.

Makingo yanayomwaga maji hutumika zaidi katika maeneo au sehemu zenye mvua nyingi na udongo usionyonya maji kwa urahisi.

Upimaji wa makingo vilevile huanzia juu kabisa ya shamba ambapo mambo zinazoonesha nafasi kati ya makingo hutumika kama mahali pa kuanzia.

Uchimbaji wa makingo

Kazi ya uchimbaji wa makingo hufanyika kwa kuchimba mitaro ambayo husaidia kuweka kizuizi cha maji yanayotiririka shambani.

Uchimbaji wa mitaro ya makingo husaidia kujenga tuta linalotumika kupanda miti au majani ya malisho.

Makingo ya fanya chini yanapendekezwa zaidi kwenye miteremko ya asilimia 5 hadi 12 kwa udongo unaomomonyoka na asilimia 8 hadi 20 kwa udongo usiomomonyoka kwa urahisi.

Kina cha sentimita 45 na upana wa sentimita 45 vinapendekezwa kwa makingo ya fanya chini.

Ni muhimu kuendeleza au kutobadilisha kina na upana kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kupunguza athari ya maji mengi kukusanyika sehemu moja na kuvunja kingo.

Kutunza na kuimarisha makingo

Ili kuimarisha na kudumisha makingo, ni muhimu kuzingatia upandaji miti na majani kama vile inavyoshauriwa na wataalamu.

Mizizi ya miti na majani huushika udongo na kuzuia usichukuliwe na maji hasa wakati wa mvua nyingi.

Kwa kufuata njia hii, makingo huimarishwa na kufanya kudumu kwa muda mrefu. Licha ya kuimarisha makingomiti na majani yaliyopandwa juu ya makingo yanaweza kutumika kwa malisho, kuni na kurutubisha ardhi.

Ili kupata makingo imara na malisho ya kutosha, mistari miwili ya majani ya tembo au Guatemala ipandwe juu ya kingo katika hali ya mshahazari.

Majani ya jamii ya mikunde yanaweza kupandwa pamoja na majani ya tembo au Guatemala na miti inayofaa kwa kilimo mseto ipandwe kwa kiasi cha sentimita 50 kutoka mstari wa majani.

Utunzwaji na uimarishaji wa makingo ufanywe kwa kujaza udongo na kupanda majani sehemu zilizobomolewa na maji.

Ni muhimu shughuli za kurepea na kuimarisha makingo zifanyike mara tu mvua za msimu zinapomalizika. Aidha, shughuli hizi ni za kudumu na inafaa ziende sambamba na shughuli nyingine za kilimo.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *