- Mifugo

Athari za ukame kwa mifugo na namna ya kukabiliana nayo

Sambaza chapisho hili

Ukosefu wa mvua umeathiri wafugaji na mifugo yao kwani maeneo ya malisho yanakauka na maji hayapatikani. Hii imepelekea maeneo mengi ya malisho kukauka na pia wafugaji wengi kuhama na mifugo yao ili kutafuta maeneo yenye maji na malisho.  

Athari za ukame zimeonekana wazi katika maeneo mengi ya wafugaji. Mifugo kukonda, afya za mifugo imezidi kuwa mbaya kutokana ukosefu wa lishe na maji, mifugo mingi imeanguka na kushindwa kusimama, mingine kufa. Kutokana na afya kuwa mbaya bei ya mifugo imeshuka kwa kiwango kikubwa na kuathiri uchumi wa wafugaji.

Magonjwa ya mifugo, kutokana na ukame afya ya mifugo imezidi kuwa mbaya, na kukosa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Hali hii imesababisha wafugaji kuhama ambapo jambo hili limeinua u migogoro kwani wafugaji wamejikuta wakiingia kulisha mifugo maeneo yasioruhusiwa.

Nini kifanyike kukabiliana na janga la ukame

Wadau wa sekta ya mifugo wakiwemo wafugaji wenyewe wanatakiwa kukaa na kujadili mikakati sahihi ya kujidhatiti na ukame.  Hata hivyo baadhi ya vipaumbele kama suluhu ambazo zimeshajadiliwa ni kama;

  • Kupunguza idadi ya mifugo, ili kupunguza athari za ukame. Wafugaji wanashauriwa kubadili mitazamo kwa kuacha kufuga kwa mazoea kwa kuwa na makundi makubwa ya mifugo isiyo na eneo la kutosha au malisho ya kutosha kwa msimu mzima wa mwaka.
  • Kuchimba mabwawa na malambo ya kunyweshea mifugo, hii itaondoa tatizo la ukosefu wa maji katika maeneo ya malisho kipindi cha ukame na kuwepo kwa maji msimu wote hivyo kutokuhamahama kutafuta maji.
  • Kupanda, kuvuna na kuhifadhi malisho yatakayotumika wakati wa ukame, wafugaji wanashauriwa kuwa na tabia ya kuweka akiba ya malisho, unaweza kuhifadhi malisho kwa njia mbalimbali kama kutengeneza silage, kuhifadhi masalia ya mazao kama mahindi, maharage sehemu iliyo kavu ili kuzuia wadudu waharibuifu.
  • Kutenga maeneo ya malisho yatakayotumika wakati wa ukame, wafugaji wanashauriwa kugawa maeneo yao ya malisho (paddocks) yaweze tumika wakati wa uhaba wa nyasi.
  • Wafugaji kukatia bima mifugo yao, hii itasaidia hata kama mifugo itakufa kwa kukosa chakula na maji mfugaji atalipwa fidia.

Kuvuna na kuhifadhi malisho ili kutumika msimu wa ukame

Malisho yanaweza kuhifadiwa kwa ajili ya matumizi ya baadae na njia zifuatazo zinaweza kutumika

  • Kuyakakausha(hey)
  • Kuyavundika(silage)
  • Uhifadhi wa masalia ya mazao kama majani ya mahindi, maharage,
  1. Kuyakausha (hey)

Hey ni majani yaliyohifadhiwa kwa kukaushwa baada ya kukatka au kuachwa kukauka yakiwa shambani kwa matumizi ya baadae,

Jinsi ya kutengeneza hey

  • Vuna malisho yanapoanza kutoa maua
  • Yaanike kwa siku 3 mpaka 6 kulingana na aina ya malisho na hali ya hewa na pia yageuze mara moja au mbili ili yakauke vizuri
  • Baada ya kukauka yafunge katika marobota, na kuhifadhi marobota hayo juu ya kuchanja cha mbao ili kuzuia yasipate unyevunyevu na kuharibiwa na wadudu.

  1. Sileji

Sileji ni chakula maalum kinachotengenezwa kwa kutumia aina yoyote ya malisho yanayofaa kwa mifugo kama majani, nyasi, mabua ya mahindi, mtama na ufuta. Kwa kawaida sileji hutengenezwa wakati wa mvua ambapo majani hukua kwa haraka na kukatwa tena na tena mpaka kiangazi kitakapoanza, kama una shamba binafsi la majani ya napier unaweza ukawa unayaka kila baada ya wiki sita katika kipindi cha mvua. Silage utokea baada ya majani kuozeshwa na vimelea katika mfumo usiotumia oksijeni (anaerobic fermentation)

Vifaa vinavyohitaji kutengeneza sileji

  • Majani na mabua kama chakula cha mifugo
  • Molasses
  • Panga au mashine ya kukata kata majani
  • Maji
  • Mfuko mkubwa mweusi wa plastiki au shimo lililojengewa kuta zake

Namna ya kutengeneza sileji

  • Katakata malisho yako katika vipande vidogo vodogo kwa kutumia panga au mashine maalum.
  • Changanya molasses kiasi cha kila lita moja kwa lita mbili za maji au lita mbili na nusu za maji kama malisho ni makavu kiasi na lita tatu za maji kama malisho ni makavu Zaidi
  • Changanya mchanganyiko wa maji na molasses pamoja na malisho kiasi malisho yako yalowane kisasi tu.
  • Weka kwenye mfuko wako au kwenye shimo lililo jengewa na shindilia vizuri
  • Funga vizuri mfuko wako na uuweke mahali pasipo na jua
  • Kama unatuma shimo lililojengewa lifunike vizuri na plastiki na unaweza kuweka udongo kiasi juu yake.
  • Hakikisha kwamba hamna hewa inayoopenya kwenye mchanganyiko wako

Matumizi

Silage huwa tayari baada ya miezi 3 – 4 kutegemeana na aina ya malisho yaliyotumika, umri wa malisho, ubora wa uchanganyaji na mengineyo. Baada ya kuwa tayari unaweza kuanza kulisha mifugo yako silage uliyotengeneza wakati wa mvua nyingi, silage inauwezo wa kukaa hadi miaka minne tangu kuanza kutengenezwa kwake

Faida

  • Hupunguza tatizo la chakula wakati wa kiangazi
  • Huongeza utoaji wa maziwa wakati wa kiangazi
  • Mifugo huwa na afya bora hata wakati wa jua kali na malisho duni
  • Mifugo yenye afya bora huzaliana vizuri wakati wote
  • hupunguza gharana ya mashudu kwani silage ina virutubisho vingi
  • Mayai ya minyoo hufa wakati wa kutengeneza silage
  1. Uhifadhi wa masalia ya mazao

Masalia ya mazao kama mabua ya mahindi, mpunga, majani ya maharage yanaweza kuhifadhiwa sehemu kavu isiyo na unyevunyevu juu ya kichanja cha mbao au fito. Kwa kuongeza ladha nzuri (palatability) kwenye mabua molasi au urea huongezwa

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *