- Kilimo, Masoko

Mkulima atumia kilimo hai kujiendeleza baada ya kustaafu

Sambaza chapisho hili

“Naitwa Felister Mangalu (64) mkulima wa kilimo hai. Nilikua mfanyakazi wa serikali na nikastaafu mwaka wa 2019. Kabla ya kustaafu nilikuwa nikijiuliza maswali kuhusu nini nitafanya ili kuendelea kujikimu kimaisha endapo muda wangu wa ajira ukiisha.

Najua hili ni swali ambalo watu wengi hujiuliza wakiwa na sababu kama zangu. Hata hivyo, najua tumejaliwa vipawa mbalimbali na tuna uwezo tofauti tofauti. Wakati wa kustaafu ama mtu anapofikiria kitu cha kufanya, uamuzi utategemea sana kile alichozoea kufanya, ujuzi na pia rasilimali zinazopatikiana kwake.

Kwa upande wangu, nilisomea stashahada ya sayansi ya mimea, ambapo shahada ya uzamili nilisoma kuhusu kilimo endelevu. Kwa hivyo, niliamua kujitosa katika ulingo wa kilimo. Hii ndio kazi ambayo niliona ninaweza kuimudu, ingawa nilikua na hofu kama nitaweza kuisimamia vizuri ili nipate faida.”

MkM ilifanikiwa kumjua mama Mangalu kupitia soko la kilimo hai la Mesula ambapo wakulima wa kilimo hai hupeleka mazao ya mbogamboga kuuza. Mama huyu ambaye ni mkulima wa kilimo hai pia ni mnufaika wa jarida la Mkulima Mbunifu.

Mkulima Mbunifu iliamua kumfuatilia nyumbani ili kuangalia shughuli anazofanya kujifunza kutoka kwake ili kuwafikishia elimu wakulima wengine. Mama Mangalu anasema kwamba aliamua kufanya kilimo hai baada ya kutambua kuna faida katika kilimo hiki tofauti na kilimo cha kawaida ambacho kinahusisha matumizi ya mbolea za viwandani na dawa za kemikali, na hii hufanya gharama ya uzalishaji kuwa juu hasa kwa wakulima wadogo wenye mapato ya chini.

Mama huyu anaongeza kuwa, kwake yeye, afya na usalama wa chakula ni jambo la msingi kwani tunahitaji kula kila siku na sio tu kushiba bali kupata virutubisho muhimu kwa ukuaji na kuhakikisha tunakula chakula ambacho hakijumuishi vitu au mabaki ambayo ni hatari kwa miili yetu. Anauliza, “Je, aina gani basi ya chakula kinaliwa leo na kesho na kesho kutwa?” Hapa, anamaanisha, uendelevu wa ulaji chakula kilicho salama.

Hivyo, aliamua kufanya kilimo hai kwani ndio jibu kwa mahitaji yake. Kwanza, alitengeneza mbolea ya mboji katika eneo karibu na shamba. Pili, aliamua kufanya kilimo hai katika eneo dogo la wazi na kwenye kitalunyumba (greenhouse).

Kwenye maeneo hayo anazalisha mbogamboga tofauti kama vile karoti, spinachi, mbilinganya, chainizi pokchoi, maharage, nyanya, ndizi na hata bidhaa za viungo. Lengo la kuzalisha mazao haya zaidi ni kwa matumizi ya familia na kuuza ya ziada.

Changamoto

Moja ya changamoto anayokumbana nayo ni wadudu wanaoshambulia mboga pamoja na magonjwa hasa katika eneo la uzalishaji la wazi. Lakini, kupitia jarida la Mkulima Mbunifu na ushauri wa wataalamu mbalimbali ameweza kujifunza jinsi ya kudhibiti wadudu waharibifu pia magonjwa kwenye mimea. Anatumia madawa ya asili na kuhakikisha kwamba udongo ni wenye rutuba ya juu ili kuwa na mimea yenye nguvu na afya.

Faida

Mama Mangalu anaeleza kuwa, kupitia kilimo hai, ameweza kutengeneza marafiki wengi ambao kwake wamemhamasisha zaidi katika kufanya mradi wa kilimo hai. Wengine wamempa ushauri juu ya soko, wengine amewashirikisha juu ya changamoto, kuweza kujadili kwa pamoja na kupata suluhisho. Wakati mwingine wanafanya majaribio na kushirikishana matokeo. Hii imekua njia ya kujifunza kadri anavyotekeleza na kusimamia mradi. Zaidi amekuwa na jambo la kumfanya awe imara zaidi kwani kila akiamka ana kazi ya kufanya.

Funzo

“Kabla ya kuanza mradi huna budi kuondoa hofu ambayo huwapata watu wengi na kudumaza hatua muhimu za kwanza. Ni vizuri kutafuta uzoefu kutoka kwa watu wengine wanoafanya mradi kama huo wako na hata wataalamu kwa ushauri ili uweze kujitayarisha vyema kwa changamtoto zozote zinazoweza kutokea kwani hazikwepeki, ila zinatatuliwa na mradi kusonga mbele”.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *