- Kilimo, Masoko

Soko la mazao ya kilimo hai Tanzania

Sambaza chapisho hili

Ingawa taasisi nyingi zinasisitiza kilimo hai nchini Tanzania, kuna walaji wachache sana walio na uelewa wa bidhaa za kilimo hai. Soko la mazao ya kilimo hai lipo tu na kufahamika katika miji mikubwa kama vile Dar es Salaam na Arusha, na mashirika machache yaliyoidhinishwa katika kuuza mazao kwa misingi ya kilimo hai kwa ajili ya soko la ndani na hata nje.

Uuzaji nje bidhaa za kilimo hai na usajili

Kwa kawaida soko la nje la bidhaa za kilimo hai huhitaji usajili na nembo kwenye bidhaa. Kwa usajili, kampuni inayojitegemea ni lazima iwadhibiti wazalishaji (kwa kawaida mwaka mmoja) ili kudhibitisha kuwa bidhaa hiyo imezalishwa kwa kufuata misingi na vigezo vya kilimo hai. Vigezo vinaelezea kwa undani ni kwa namna gani bidhaa inaweza kuzalishwa, kuwekwa nembo na kuuzwa kama bidhaa ya kilimo hai.

Mfano, nchini Tanzania, Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM) ndilo linalothibitisha bidhaa za kilimo hai ambazo huzalishwa na kuuzwa nchini n ahata nje ya nchi.

Usajili na kuweka nembo unahakikisha kuwa si kila mzalishaji anaweza kudai kuwa bidhaa yake imezalishwa kwa kufuata kilimo hai. Nembo husaidia kutoa uhakika kuwa ni kweli bidhaa husika imezalishwa kwa kuzingatia mfumo wa kilimo hai. Kama umempata mnunuzi wa bidhaa za kilimo hai ni lazima ufuate masharti na kanuni halisi za uzalishaji hai.

Orodha ya mahitaji ni kubwa na inaweza kuwa tofauti na ile inayofuatwa katika kilimo cha jadi na kilimo cha kisasa. Unachohitajika ni kufahamu mahitaji halisi na vigezo, mfano: – ni dawa zipi zinazohitajika kutumima kudhibiti wadudu na magonjwa, uzalishaji, uhifadhi na vifungashio vya bidhaa vinavyotakiwa. Udhibiti na usajili hugharamiwa na mkulima mwenyewe.

Mafunzo ni muhimu kwa ajili ya uzalishaji uliosajiliwa

Ni changamoto kwa wakulima wadogo wadogo kuondokana na kilimo cha kisasa na kuingia katika kilimo hai. Baadhi ya mashirika yamekuwa yakiingia mikataba na wakulima kwa ajili ya kuzalisha kwa kuzingatia misingi ya kilimo hai, kisha kununua kwa ajili ya kuuza nje, na kwa kawaida huwapatia mafunzo. Kwa sababu ya gharama kubwa za kupata usajili, wakulima wadogo ni lazima wajiunge katika vikundi vya wazalishaji. Kwa misingi hii, gharama za usajili zitagawanywa kwao na hii itawapa unafuu mkubwa sana.

Soko la nyumbani la mazao ya kilimo hai

Masoko machache ya ndani yasiyo rasmi, taasisi n.k, mara nyingi hayahitaji usajili, na badala yake yanaweza kutegemea gharama ndogo kutambulika. Kwenye miji mikubwa, kuna nafasi kubwa ya kupata soko la bidhaa za kilimo hai.

Kuna mifano mingi ya mafanikio katika kuanzisha soko la bidhaa za kilimo hai. Kwa kutumia usajili na nembo, mlaji anaweza kushawishiwa na uhalisia wa bidhaa za kilimo hai. Kuna mashirika mengi ambayo kwa sasa yanajihusisha na kilimo hai, ikiwa ni pamoja na vikundi vya vijana. Kila siku vijana wamekuwa wakiweka mboga na bidhaa nyingine katika mashamba yao kwenye meza na kisha kuwaelewesha na kuwafundisha wanunuzi ni kwa jinsi gani hizo bidhaa zina ubora wa hali ya juu. Ni kwa nini wewe usiwafuate ukawa mfano wa kuigwa?

Kama una uhakika na unachozalisha, basi wafahamishe walaji wa ndani kuhusu bidhaa zako, ubora wake na ni kwa nini wanunue kutoka kwako. Hii inaweza kufanyika kwa mdomo tu au kwa vipeperushi. Jivunie ulicho nacho.

Kwa maelezo zaidi Unaweza kuwasiliana na Mkulima Mbunifu kwa simu namba +255 0717266007 au kwa barua pepe info@ mkulimambunifu.org

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *