- Kilimo, Kilimo Biashara, Masoko

Fursa ya kibiashara kwa misingi ya Kilimo hai

Sambaza chapisho hili

‘’Mimi ni mkulima wa mfano, ninazalisha mazao mbalimbali kwa misingi ya kilimo hai na nimefaidika sana’’. Hayo ni maneno ya mkulima wa kilimo hai, Bw. Michael Laizer (73), toka Kijiji cha Emaoi, Ngaramtoni, mkoani Arusha ambaye anajishughulisha na uzalishaji wa mazao ya biashara kwa misingi ya kilimo hai.

Bw. Laizer, ambaye jina la kibiashara linalotambulika kama nembo kwenye bidhaa zake likiwa ni kilimo hai. Anaeleza kuwa, watu wengi wamezoea kilimo hai kama ni kiilimo kinachoweza kufanyika tu katika eneo dogo hasa la bustani, na kwamba haiwezekani kufanya kilimo hai katika maeneo makubwa na kama kilimo biashara

Bwana Laizer alieleza kwamba alifanya kazi SIDO kuanzia mwaka 1980 hadi 1994 na akarudi tena 2012 hadi 2019. nilipostaafu. Mnamo mwaka 2020 niliamua kujiajiri mwenyewe kwa kuanza kilimo hai bila kushawishiwa na mtu yeyote

Kwanini kilimo hai

Laizer mwenye mke mmoja na watoto 2 anasema kuwa, aliamua kuingia kwenye kilimo hai kwasababu yuko alivyo kutokana na anachokula (I am what I eat). Hivyo akaona ni vyema kuzalisha chakula bora na salama kwa ajili yake na familia yake.

“Mbali na kuangalia afya yangu, nilikuwa nikisikia watu wakihangaika sana kutafuta mazao ya kitunguu na tangawizi na wengine wakidai kuwa kilimo cha mazao haya hakiwezekani kwa maeneo ya Arusha. Hivyo nikaamua kuwaonyesha kuwa hiyo ni fursa na kila kitu kinawezekana kikubwa tu ni kuamua’’.

Alianzaje kilimohai

Bw. Laizer anasema, alitafuta elimu ya kilimo hai kwakua ni msomi alikuwa akifahamu kuwa chanzo kikuu cha kilimo hai ni mbolea hivyo alikuwa na uhakika wa kupata mbolea ya samadi jambo lililomtia hamasa na kuamua kuanza moja kwa moja kuzalisha.

Nini cha kuzingatia katika shamba la kilimo hai

Bwa. Laizer anaeleza kuwa, ili kufanya kilimo hai kwa ufanisi, kuna mambo muhimu ni lazima kuhakikisha unafuata ili kupata tija katika uzalishaji. Mambo hayo ni kama ifuatavyo;

  • Hakikisha mfumo wa uzalishaji wa mazao yako yatazingatia kupatikana kwa chakula bora na salama. Usitumie kemikali za viwandani kuzalisha mazao ya kilimo hai.
  • Urutubishaji wa udongo. Chakula kinatoka katika udongo wenye rutuba hivyo, hakikisha shamba lako linakuwa na mbolea wakati wote yaani kuwe na samadi au mboji au mbolea ya chai.
  • Ni lazima uzalishe kwa kulenga soko ili kila unapovuna upeleke mazao sokoni yasiharibike.
  • Fahamu kuhusu uhifadhi wa mazao mara baada ya kuvuna. Ni muhimu kujua kama ukivuna unatakiwa kuyahifadhi vipi na katika usalama kabla ya kupeleka sokoni. Ikiwa hayataenda sokoni kwa wakati huo utayatunza vipi ama utayafanyia usindikaji.

Mazao ya kilimo hai anayozalisha na soko

Bw. Laizer anazalisha maharage machanga (green beans) kwa mkataba na shirika la Home Fresh, ambapo zao hili linavunwa kila baada ya siku tatu na kusafirishwa kwenda nje ya nchi. Pia anazalisha mapapai, vitunguu maji, vitunguu swaumu, ndizi, tangawizi pamoja na kusindika bidhaa mbalimbali kama vile, chai masala, pilau masala, tanagawizi, na asali.

Soko la ndani

Aidha, mazao haya pia huyavuna na kupeleka kwenye soko la bidhaa za kilimo hai Mesula ambalo lipo Arusha, maeneo ya Gymkhana.

Vipi kuhusu mkulima mbunifu

Jarida hili limekuwa tunu sana kwangu kwani nimejifunza vitu vingi ikiwa kunijengea uwezo mkubwa wa ni kwa namna gani niwashauri wakulima kuingia kwenye kilimo hai.

“Kupitia jarida majarida ya MkM nimeweza kujifunza hatua za kufuata wakati wa kufanya kilimo hai, kanuni za msingi za kilimo hai na hivyo kuniongezea wigo mkubwa katika uzalishaji wa chakula bora na salama (Toleo la 119, Agosti 2022)’’.

Wakulima wataaminije kuwa unazalisha bidhaa za kilimo hai

“Nilipoanza tu kujiingiza katika uzalishaji wa mazao ya kilimo hai, niliweza kutembelewa na waidhinishaji wa bidhaa za kilimo hai nchini Tanzania (TOAM). Wao walifanya ukaguzi na upimaji na kuidhinisha kwa kunipa cheti cha mzalishaji wa bidhaa za kilimo hai.

Pia, bidhaa zangu zimeweza kupimwa, kuidhinishwa na kupewa nembo na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa ni bidha salama kwa afya ya walaji’’.

Wito kwa wakulima

Kila kitu kinawezekana pale tu ukiamua kufanya. Ninawashauri wakulima kujikita katika uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo hai hasa kuifanya kama kilimobiashara kwani kinawezekana na kinalipa.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *