- Mifugo

Namna ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa wanyama

Sambaza chapisho hili

Ufugaji ni utunzaji na uzalishaji wa mifugo kwa madhumuni ya kilimo, ikiwa ni pamoja na chakula na bidhaa zingine kutokana na mifugo. Ikifanywa ipasavyo, ni shughuli yenye uwezo mkubwa ya kumkwamua mkulima na kumpa mapato ya kutosheleza mahitaji ya kila siku.

Wengi wa wakulima wadogo huunganisha ufugaji na kuzalisha mazao, ingawa baadhi ya wakulima huzingatia ufugaji pekee, ili kuwawezesha kupata fursa ya kufuga aina moja au mbili kwa ufasaha.

Wafugaji wanatumia rasilimali kama vile nyasi, maji na kadhalika kuwawezesha wanyama kuzalisha. Ufugaji sio tu kuangazia myama bali pia inahusisha mchakato mzima wa kuzalisha rasilimali zinazotumika katika ufugaji.

Bidhaa kutokana na ufugaji kama vile nyama ina uhitaji mkubwa katika soko kwa kuwa na manufaa mengi kiafya. Ni biashara yenye faida kubwa na inaweza pia kuwa na kazi nyingi. Kwa hivyo, ni muhimu kuangalia na kujua chaguo bora kwako ili kuweza kufanya ambayo yatakuletea faida zaidi.

Kwa mfano, hutapata faida nzuri katika hali ambayo unazingatia ufugaji wa nguruwe pekee katika eneo ambapo watu wengi wanapendelea kula kuku au mbuzi. Uelewa wa soko unalolenga unachangia pakubwa katika ufanisi wa biashara ya ufugaji.

Unapofikiria kuingia katika sekta ya ufugaji hapa Tanzania, tunakupa vidokezo vya kuzingatia unapojiandaa kufanya ufugaji wenye mafanikio. Na hapa tunatumia mtazamo wa kibiashara kwa sababu lengo kuu ni mkulima kuinua hali yake kwa kuzalisha zaidi na kuuza zaidi.

Nini Kusudi Lako?

Huwezi kufanikisha ufugaji kama hujui na huelewi lengo lako vizuri. Kujua sababu ya kufanya shughuli za ufugaji ni muhimu sana kwa sababu husaidia kujua nini unataka na jinsi gani unaweza kufikia lengo lako. Ikiwa unapanga kuingia katika ufugaji wa wanyama, wa nyama na bidhaa za maziwa, basi ng’ombe au mbuzi wanaweza kuwa chaguo bora zaidi.

Kuelewa kusudio lako husaidia kuelezea kile unachotaka. Hii ni muhimu sana katika kuanzisha ufugaji kwa sababu unachochagua ndicho kitakachoamua vifaa vinavyohitajika.

Kwa ajili ya kuendesha biashara ya uzalishaji wa maziwa, inahusisha kufuga mifugo hasa kwa ajili ya bidhaa za maziwa, na biashara ya uzalishaji wa nyama inahusisha ufugaji wa mifugo hasa kwa ajili ya matumizi ya nyama. Hivyo, huwezi kuwanunua ng’ombe wa nyama ili kuzalisha maziwa. Hapo, utapoteza au mapato yako yatakuwa ya chini mno.

Tunarudia kwamba, kuna aina nyingi za uzalishaji katika ufugaji. Kwa mfano, unaweza kuwekeza katika ng’ombe kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa na/au kutengeneza na kuuza jibini, mkulima mwingine anaweza kuwekeza kwenye kuku wa nyama au mayai, mwingine kwa nguruwe na kadhalika. Hapa Tanzania, kila mkoa una nguvu na udhaifu wake; mjasiriamali katika nyanja hii ya ufugaji anapaswa kushauriana na idara ya mifugo katika wilaya yake ili kutengeneza mkakati ambao utafanya kazi vyema katika eneo husika.

Tafuta Mahali

Unazalisha wapi? Kupata eneo kunategemea ikiwa unaingia katika biashara kubwa au ndogo; yaani, unatazamia kuwafuga wanyama wengi au wachache. Hii itasaidia kuamua eneo bora kwa biashara yako. Ingawa, unaweza kuanza na eneo dogo na wanyama wachache kisha ukapanua biashara yako kwa utaratibu, hatua kwa hatua kulingana na mapato yako na pia mtaji unaopatikana.

Sambamba na hili, ni muhimu kujua ukubwa wa ardhi unayohitaji kwa uzalishaji wa mifugo yako. Kwa mfano, utahitaji eneo dogo kuzalisha kuku wa mayai kama unanunua chakula cha kuku kutoka madukani. Lakini, kama unapanga kuzalisha malighafi kama vile mahindi, soya, na kadhalika, na kutengeneza chakula nyumbani basi lazima uongeze ukubwa wa shamba kulingana na idadi ya kuku unaowafuga. Vivyo hivyo, kiasi cha ardhi kinachotumika kwa ng’ombe ni tofauti na ile inayotumika kwa ufugaji wa sungura.

Ni muhimu pia kuwa karibu na miundo mbinu muhimu kama vile maji, barabara na umeme. Hakikisha barabara sio mbovu kiasi kwamba italeta shida kubwa kwako kusafirisha mifugo au bidhaa yako kwenda sokoni. Hata hivyo, tunasema anza au fanya ulipo.

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Namna ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa wanyama

  1. Nivizuri kushare habari mpya kuhusu ufugaji km aina mpya bora ya kuku , ng’ombe na mbuz,

    1. Habari,

      Karibu Mkulima Mbunifu na asante sana kwa maoni yake. Ni kweli tumekuwa tukijitahidi kuchapisha habari mbalimbali mpya zinakuja kuhusu mifugo ikiwa ni habari zenye uhakika na zinazoaminika. Soma makala zetu tulizochapisha huku kwenye tovuti na utakutana na taarifa hizo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *