- Mifugo

Ulishaji sahihi wa mifugo

Sambaza chapisho hili

Kulisha ni muhimu sana katika ufugaji wa mifugo, hivyo kama unajishughulisha na ufugaji wa kondoo, ng’ombe, mbuzi, na mwanyama wengine wanaokula nyasi, inashauriwa kupanda nyasi shambani mwako au karibu na eneo lako kwa sababu itasaidia kupunguza gharama zinazoweza kutokea katika utoaji wa chakula na virutubisho vingine.

Ulishaji unajulikana kuwa moja ya sababu muhimu kwa ufugaji wa mifugo wenye mafanikio kwa sababu wakilishwa vizuri, watazalisha inavyopaswa. Kulisha mifugo vizuri haimaanishi kulisha kupita kiasi, lakini inamaanisha kuwapa chakula kinachofaa na kinachotosheleza mahitaji.

Kulisha mifugo kunahitaji maarifa, ujuzi na uzoefu mwingi ili kuweza kulisha inavyotakiwa. Ni muhimu sana kuelewa aina mbalimbali za vyakula vinavyoweza kulishwa kwa mifugo, na kisha kujifunza jinsi vyakula mbalimbali vinavyoweza kuunganishwa pamoja ili kutengeneza mgao sawia kwa wanyama.

Ukweli ni kwamba, unaponunua mnyama mzuri kisha unashindwa kumlisha hiyo ni hasara ama kazi isiyo na faida.

Hivyo, tuwekeze katika ulishaji, hasa kuelewa ni nini tunawalisha mifugo, wanahitaji virutubisho gani kwa viwango gani, na inagharimu kiasi gani. Hapa ndio inatofautisha yule mkulima atapata faida na yule wa hasara.

Fahamu kuhusu Soko

Kufikiria swala la soko mwanzoni, ni muhimu sana, kwa sababu sio tu kuelewa upatikanaji wa soko bali pia soko hili litafikiwa vipi? Kuzingatia tu kuzalisha bidhaa za ubora wa juu haitoshi, lakini ni muhimu kujua utakavyouza bidhaa zako; na wapi unaweza kuuza bidhaa.

Elewa nyakati ambazo soko huwa na bei bora zaidi ili kuendana na mzunguko wa uzalishaji. Utakuwa unatabasamu wakati wengine wananung’unika. Kumbuka, unaanza na kufikiria juu ya soko kwa sababu ndio itaamua unafuga nini na wapi.

Tenga Muda

Ufugaji wa mifugo unahitaji kujitolea sana. Wanyama wengi wanahitaji kulishwa na kupewa maji kila siku. Kuchunguza mara kwa mara kiwango cha maji ni muhimu sana, pia ni lazima kama unapanga kuanzisha ufugaji. Ukaguzi wa kila siku wa mifugo wako ni mojawapo ya njia bora za kuzuia majeraha, hivyo, lazima uwe karibu.

Ukitaka kuwa na ufugaji wenye faida na mafanikio unahitaji kuwekeza muda wako ili kuwatunza mifugo ipasavyo.

Ikiwa umeajiriwa ama unapanga kuondoka nyumbani kwa muda mrefu, unahitaji kupata mtu ambaye atasaidia katika kuangalia na kuwatunza wanyama wako. Lakini hii itategemea mapato yako na ufugaji wenyewe.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *