- Mifugo

Dume bora ni chanzo cha uzalishaji bora

Sambaza chapisho hili

Unapojipanga kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa au nyama, jambo la msingi ni kuhakikisha ni aina gani ya ng’ombe utachagua/utanunua au utatumia katika uzalishaji.

Aina hii ya ng’ombe pia pamoja na kuwa utanunua lakini hutokana na dume bora hivyo ni jambo la msingi sana kujua aina ya uzalishaji wako umetokana na dume mwenye ubora.

Uchaguzi wa dume hupelekea uzalishaji wenye tija

Nini cha kufanya

Jambo la muhimu ni kuhakikisha unachagua dume litakalotumika kwa ajili ya mbegu, na ni lazima uzingatie ubora na kiwango cha uzalishaji wa maziwa kutoka kwa mama aliyemzaa dume huyo kama unafuga kwa ajili ya maziwa na pia ubora wa nyama kwa suala la uzalishaji wa nyama.

Njia sahihi pekee ya kuchagua dume ni kwa kuangalia uzao wake. Kumbukumbu za uzalishaji wa ng’ombe jike hutegemeana na dume lililotumika, kizazi anachotoka dume huyo ni moja ya kigezo ambacho huzingatiwa pia dume linapochaguliwa.

Wazazi wa dume hilo, hasa jike ni lazima liwe linafahamika kuwa na historia ya kuzaa kirahisi, na kuwa na uwezo wa kustahimili magonjwa kama vile mastitis. Dume lililopitishwa ndilo pekee litumike na mfugaji.

Uangalizi wa dume

Dume ni lazima litunzwe kikamilifu na kwa makini kuanzia kuzaliwa mpaka kukomaa. Dume ni lazima likatwe pembe kwa kuwa linaweza kuwa hatari kwa usalama.

Ni lazima dume lifanyiwe mazoezi mara kwa mara ili awe na umbile zuri. Dume mdogo anaweza kutumika kupanda ng’ombe kuanzia akiwa na miezi 18. Upandishaji unaweza kuongezeka taratibu kufikia mara tatu kwa wiki, zaidi ya hapo unaweza kumchosha na kumdhoofisha na kupunguza uwezo wake wa kuzalisha.

Banda la dume

Dume awekwe kwenye banda lake mwenyewe na apelekwe kwenye banda la majike kwa muda ule tu anaotakiwa kupanda.

Endapo dume litaachwa kuzunguka na ng’ombe jike muda wote, ng’ombe walioko kwenye joto watabeba mimba bila ya mfugaji kufahamu. Hiyo huathiri uwekaji wa kumbukumbu kwa mfugaji. Kuzaliana kwa kizazi kimoja ni dhahiri endapo hakutakuwa na uangalifu wa kutosha.

Dume pia anaweza kupanda mitamba ambao bado ni wadogo na hawajafikisha umri wa kupandwa.

Endapo uchaguzi wa dume hautafanyika kwa usahihi, unaweza kuwa na kizazi dhaifu. Kuepuka kizazi kujirudia dume linaweza kubadilishwa kila baada ya miaka miwili, na hii inaweza kuwa gharama sana. Dume mwenye uzito mkubwa asiruhusiwe kupanda mtamba mdogo ili asije kumuumiza. Dume ambaye ni mgonjwa anaweza kusambaza ugonjwa haraka.

Kwanini dume

Bado dume wanatumika na wafugaji walio wengi hapa nchini Tanzania kwa sababu dume huwa halikosei ng’ombe anapokuwa kwenye joto. Mfugaji wa kisasa inapendekezwa kutumia mbegu za mpira kwa kuwa zina faida na ni za gharama ndogo, hasa endapo mfugaji ataweza kumudu mbinu zinazotumika, ikiwa ni pamoja na kufahamu muda na wakati ng’ombe anapokuwa kwenye joto, kuweka kumbukumbu kwa usahihi na kutunza mifugo vizuri.

Kila mfugaji anahitaji kuwa na ng’ombe anayezalisha maziwa mengi au kupata madume wenye nyama nyingi na bora, hivyo unashauriwa kuwa unapoanza mradi wa ufugaji wa ng’ombe unachagua dume mzuri na aliyethibitishwa, atakayeweza kukidhi sifa unayohitaji kwa ajili ya  uzalishaji wa hapo baadaye.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *