- Binadamu, Kilimo

Usindikaji wa vitunguu saumu

Sambaza chapisho hili

Kabla ya kusindika vitunguu saumu ni muhimu kuhakikisha kuwa vitunguu vinavyosindikwa vimekomaa vizuri na vipo kwenye kiwango cha ubora na havijaoza.

Dalili za vitunguu saumu vilivyokomaa

  • Vitunguu saumu huwa tayari kuvunwa katika kipindi cha miezi mitatu hadi mitano tangu kusia mbegu
  • Vitunguu saumu vilivyokomaa huonyesha majani kunyauka na kubadilika rangi na kuwa ya manjano hadi kahawia.
  • Shingo ya vitunguu saumu hulegea na majani yake huanguka.

Bidhaa zitokanazo na kusindika vitunguu saumu

Kitunguu saumu huweza kusindikwa ili kuongeza thamani kwa kuzalisha bidhaa ambazo ni pesti pamoja na unga.

Kusindika kitunguu saumu ili kupata pesti (lahamu)

Kuna njia mbalimbali za kutengeneza lahamu ya vitunguu saumu, lahamu nyingine huchanganywa na viungo, na nyingine hutumia vitunguu saumu ambavyo vimepikwa kidogo.

Vifaa kwa ajili ya kusindika ni pamoja na kisu kikali kisichoshika kutu, meza safi yenye kufunikwa na bati la aluminiamu, chupa zenye mifuniko imara, mashine ndogo ya kusaga vitunguu saumu, jiko, sufuria, lebo, lakiri na mizani.

Malighafi ni pamoja na vitunguu saumu, maji safi, chumvi, siki au sodiamu benzoate na mafuta ya maji.

Jinsi ya kusindika

  • Chagua vitunguu saumu ambavyo havina ukungu na mikwaruzo na ondoa magamba kwa kutumia kisu.
  • Ondoa vikonyo vuyote na menya kisha osha kwa maji safi na salama.
  • Weka vitunguu saumu safi vilivyomenywa kwenye sufuria ya maji safi yanayochemka kwa muda wa dakika moja.
  • Ondoa kwenye maji na saga kwa kutumia mashine kisha pima uzito wa pesti.
  • Ongeza chumvi asilimia 5, yaani gramu 50 kwa kila kilo moja ya pesti.
  • Ongeza ndimu au siki maalumu (balsamic vinegar) gramu 30 kwa kila kilo moja ya pesti.
  • Ongeza mafuta ya maji kiasi cha gramu 30 kwa kila kilo moja ya pesti. Hii husaidia vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
  • Koroga mchanganyiko hadi uwiane na fungasha kwenye chupa safi zilizochemshwa.
  • Panga chupa kwenye sufuria kisha weka maji hadi yafikie nusu kimo cha chupa hizo na chemsha kwenye moto wa kadiri kwa muda wa dakika 25 hadi 30.
  • Ipua, acha zipoe kisha weka lebo na lakiri.
  • Hifadhi sehemu yenye ubaridi, kavu na yenye mwanga uliofifia.
  • Vitunguu saumu vilivyosindikwa vizuri huweza kuhifadhiwa kwa zaidi ya miezi sita katika hali ya kawaida bila kuharibika.

Matumizi ya pesti ya vitunguu saumu

Pesti ya vitunguu saumu hutumika kama kiungo kwatika vyakula mbalimbali, dawa ya kutuliza magonjwa ya moyo, na kuzuia magonjwa mengine.

Kusindika vitunguu saumu kupata unga

Vifaa vinavyohitajika ni pamoja na kaushio bora, mashine ya kusaga, kisu kisichoshika kutu, chekeche, mabeseni na chupa za kuweka viungo.

Maligafi ni vitunguu safi visivyokuwa na ukungu.

Jinsi ya kutengeneza

  • Chagua vitunguu saumu ambavyo havina ukungu wala magonjwa na menya kwa kutumia kisu kisichoshika kutu.
  • Osha kwa maji safi na salama kisha katakata vipande vidogo visivyozidi unene wa milimita 2.
  • Kausha kwa kutumia kaushio au kichanja bora kisha saga kwa kutumia mashine ili kupata unga.
  • Chekecha unga huo ili kupata unga laini na fungasha kwenye chupa safi zilizochemshwa na funga kwa mifuniko.
  • Weka lakiri na lebo kisha hifadhi sehemu iliyo baridi, kavu na yenye mwanga hafifu.

Matumizi ya unga wa vitunguu saumu

Hutumika kama kiungo katika vyakula mbalimbali kama ambavyo kitunguu saumu kibichi inavyotwangwa na kutumiwa.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Usindikaji wa vitunguu saumu

  1. ahsanteh kwa elimu nzuri na pia nina swali swali langu ni kwamba je, kuna anina nyingine ya kuku wa kienyeji wenye faida nzuri tofauti na kuroila?

    1. Habari, Karibu Mkulima Mbunifu.
      Kuku aina ya kuroila ni kuku chotara siyo kuku wa kienyeji asilimia 100 ila nui mchanganyiko. Kuku wengine unaoweza kuwafuga ambao ni chotara ni SASSO, hawa nao ni kuku wazuri na unaoweza kuwafuga kwa urahisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *