- Binadamu, Kilimo

Uji wa chaya, lishe bora kwa familia

Sambaza chapisho hili

Chaya ni mboga ya kijani kibichi iliyo katika kundi la kisamvu ambayo huota ikiwa kwenye uonekano wa kisamvu yaani huwa na shina nyingi na majani mengi ambapo majani hayo hutumika kama mboga.

Mboga aina ya Chaya, huota katika hali yeyote hata katika maeneo yenye kame kwani hustahimili hali ya ukame na hivyo hufanya jamii ya eneo husika kuwa na mboga msimu wote.

Kwanini ni muhimu sana kula chaya

  • Majani ya chaya ni chanzo kikubwa cha madini ya chuma, protini, kalshiamu, Vitamini A na C, foliki, asidi na Vitamini B.
  • Protini; Inajenga misuli. Mlo mmoja tu wa chaya ni sawa na kiwango cha protini kinachopatikana kwenye yai.
  • Madini ya chuma; Kwa afya ya damu na nguvu nyingi. Chaya ina kiasi kikubwa cha madini ya chuma mara mbili zaidi ya kiasi kinachopatikana kwenye spinachi.
  • Kalshiamu; Kwa mifupa yenye nguvu, chaya ina kiasi kikubwa cha kalshiamu kuliko mboga zingine zote.
  • Vitamini A; Inazuia upofu, inapunguza kiwango cha maambukizi ya magonjwa ya kuhara.
  • Vitamini C, foliki asidi na Vitamini B; Vyote hivi ni muhimu sana kwa afya. Kwa watoto wa miezi 6 hadi miaka 2, chaya halisi ni nzuri sana kwa kupata protini na vitamini hasahasa wakati ambapo wameachishwa kunyonya maziwa ya mama. Supu ya chaya ni nzuri sana kwa watoto wa miaka 2 na kuendelea, na inaweza kutumika kama mlo ikichanganywa na vyakula vingine.

Mama anayenyonyesha ambae anakula chaya ana maziwa mengi na bora kwa ajili ya mtoto wake.

Namna ya kutengeneza uji wa chaya

Chaya imezoeleka kutumiwa kama mboga za majani, lakini inawezekana pia kusaga na kutumia kupika uji na virutubisho vilevile vikawa bado vinapatikana.

Hatua za utengenezaji wa unga wa chaya

Mahitaji

Vifaa vinavyohitajika ni kisu kikali, kaushio la jua [dryer], mboga ya chaya, mahindi makavu, chombo cha kuhifadhi.

Namna ya kutengeneza

  • Chuma majani ya chaya kisha chambua kuondoa taka, na osha vizuri kwa maji safi na salama.
  • Tumia kisu katakata kama mboga ya kupika yaani vipisi vidogovidogo kisha weka kwenye kaushio la jua.
  • Acha mpaka utakapoona imekauka vizuri, inaweza kukauka ndani ya siku 1 hadi 2 kulingana na hali ya hewa.
  • Baada ya kukauka toa kwenye kaushio kisha fikicha kwa mikono.
  • Chukua mahindi makavu kisha osha kwa kutumia maji safi na salama na kausha.
  • Pima mahindi kilo 3 na changanya na mboga ya chaya gramu 500.
  • Saga na rudia mara tatu ili unga ulainike vizuri na tayari kupika uji.

Kuna aina mbili ya uji wa chaya ambayo ni uji wa kukatia mboga za chaya na uji wa unga wa mboga za chaya.

Namna ya kupika uji wa unga wa chaya

  • Chukua maji safi na salama, weka kwenye sufuria ya kupikia uji na injika jikoni.
  • Maji yakishaanza kupata uvuguvugu ongeza unga na koroga vizuri mpaka utakapochemka. Waweza kupima maji lita moja kwa vijiko 4 vya unga au kulingana na uzito utakopendelea.
  • Acha uji uchemke kwa muda zisizopungua 45 na uji wako utakuwa tayari kunywa. Unaweza ukaongeza maziwa kama utapenda.

Namna ya kupika uji wa mboga iliyokatwa ya chaya

  • Chuma na safisha mboga za chaya kisha kata vipisi vidogo.
  • Chemsha mboga hiyo kisha ipua na weka pembeni.
  • Chukua sufuria kisha pika uji kwa kutumia unga wenye mchanganyiko wa mahindi na chaya kwa dakika 30.
  • Chukua mboga uliyochemsha kisha ongeza kwenye uji [ongeza kwa kiwango utakachopenda].
  • Endele kuchemsha kwa muda usipungua dakika 15 kisha ipua tayari kwa matumizi.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *