- Binadamu, Kilimo, Kilimo Biashara, Mazingira, Udongo

TAHADHARI: Mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli (Oktoba – Disemba, 2026) na uwepo wa El Nino

Sambaza chapisho hili

Katika msimu huu wa Vuli ambao huanza mwezi Oktoba, inatarajiwa kuwa joto la bahari katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuendelea kuwa la Juu ya Wastani, hali inayoashiria uwepo wa El Niño yenye nguvu kubwa. Aidha, joto la bahari la Juu ya Wastani linatarajiwa zaidi katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi ikilinganishwa na eneo la mashariki, hali inayotarajiwa kusababisha upepo wa bahari wenye unyevu kuvuma kuelekea maeneo ya nchi yetu. Vilevile, joto la bahari la Wastani hadi Juu kidogo ya Wastani linatarajiwa katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Atlantiki (karibu na pwani ya Angola). Kwa ujumla, hali hizi za bahari zinatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo mengi ya nchi.

Msimu wa mvua za Vuli, 2026 unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Nino yenye nguvu kubwa.

Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za Juu ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Aidha, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba na wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba, 2026 katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria na baadae kusambaa taratibu katika maeneo mengine mwezi Oktoba ambapop kwa kawaida huisha mwezi Desemba; hata hivyo, katika msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Januari, 2027 hivyo ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Novemba, 2026.

Kutokana na uwepo wa El-Niño, vipindi vya mvua vinatarajiwa kwa mwezi Septemba, 2026 katika baadhi ya maeneo nchini. Na mvua za Vuli kuanza rasmi mwezi Oktoba, 2026 katika maeneo mengi.

Kuwepo kwa hali ya El Niño kuelekea mwishoni mwa mwaka kunaweza kusababisha kuanza mapema kwa mvua za Novemba 2026 – Aprili 2027 (Msimu) katika baadhi ya maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, ambako kwa kawaida msimu wa mvua huanza mwezi Novemba.

Athari

Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi kwenye udongo pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo. Magonjwa ya mazao yanayosababishwa na kuvu, bakteria na virusi yanaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji, ubora na mavuno ya mazao mbalimbali. Aidha, Mvua za muda mrefu zinaweza kuathiri shughuli za uvunaji na kusababisha upotevu wa mazao baada kuvuna.

Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati. Pia wakulima wanashauriwa kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba; na kuchagua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu huu wa Vuli, kama wanavyoshauriiwa na maafisa ugani na taarifa za hali ya hewa za mara kwa mara.

Wafugaji wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho ya mifugo na chakula cha samaki. Hata hivyo, mlipuko wa magonjwa ya mifugo kama vile ugonjwa wa homa ya bonde la ufa, kuoza kwa kwato na kuzaliana kwa wadudu wanaosambaza magojwa vinaweza kujitokeza.

Wafugaji wanashauriwa kutumia mbinu bora za ufugaji ili kutunza malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya baadae.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *