- Binadamu, Kilimo

Maharagwe ni chanzo cha protini na madini kwa watoto

Sambaza chapisho hili

Lishe ni sehemu muhimu ya afya na maendeleo. Lishe bora inahusisha kuboreshwa kwa afya ya watoto wachanga ili kuwawezehsa kukua vyema, kujenga kinga imara zaidi, kupunguza hatari ndogo ya magonjwa na kuwa na maisha marefu.

Watoto wenye afya bora hujifunza mambo kwa haraka na kufanya vyema shuleni. Wanapokuwa watu wazima wana nguvu na uwezo wakujitengenezea nafasi ya kuvunja mzunguko wa umaskini na njaa katika kaya na jamii kwa jumla.

Maharagwe yanachukuliwa kuwa chanzo cha aina nyingi za vitamini, madini, nyuzi, na protini. Faida za kiafya za maharagwe kwa mtoto anayekua zinaweza kuwa nyingi. Kwa hiyo, unaweza kujumuisha maharagwe katika chakula cha mtoto wakati yuko tayari kufanya mabadiliko kutoka kwa maziwa ya mama hadi vyakula vingine.

Madini ndani ya maharagwe

Protini ina majukumu mengi katika mwili. Husaidia kutengeneza na kujenga tishu za mwili, huruhusu michakato ya kimetaboliki na kuratibu kazi za mwili. Ukosefu wa protini kwa watoto husababisha mwili kupoteza misuli na nyama, hali inayoitwa Kwashiorkor.

Madini ya chuma (Iron) ni sehemu kuu ya chembechembe nyekundu za damu ambayo hubeba oksijeni kutoka kwa mapafu hadi sehemu zote za mwili ili kuruhusu misuli na ubongo kufanya kazi vizuri. Bila madini ya chuma ya kutosha, idadi ya chembechembe nyekundu za damu hushuka na kupungua kwa oksijeni inayosafirishwa, ambalo husababisha uchovu wa kudumu. Upungufu wa damu husababisha kupungua kwa ukuaji wa ubongo na kinga ya mwili.

Madini ya Zinc hupatikana katika seli za mwili mzima. Inahitajika ili mfumo wa kinga ya mwili ufanye kazi vizuri. Pia, katika mgawanyiko wa seli, ukuaji wa seli, uponyaji wa jeraha. Upungufu wa zinki husababisha ukuaji duni, na kupunguza kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.

Vitamini B, hasa aina ya vitamini B1 na folate, ambayo husaidia mwili kutumia wanga, mafuta na protini na kuimarisha ubongo na neva.

Muhimu ni kwamba maharagwe yana madini ya chuma (Iron) na Zinc ambayo mara nyingi ukosekana au haitoshi kwa watoto.

Kuanza kumlisha mtoto maharagwe

Wataalamu wanapendekeza kua-nzisha mabadiliko kutoka kwa maziwa pekee hadi vyakula vingine ifanywe kwa utaratibu wakati mtoto amefikisha umri wa miezi 6.

Hata hivyo, huenda lisiwe jambo zuri kuchagua maharagwe kama chakula kigumu cha kwanza cha mtoto, kwani mfumo wake wa mmeng’enyo wa chakula haujakomaa na unaweza kupata ugumu kusaga maharagwe. Mtoto anaweza kupata gesi tumboni, kukosa kusaga na kusababisha usumbufu.

Basi, mlishe mtoto maharagwe wakati mfumo wake wa mmeng’enyo wa chakula unapokuwa unakubali vyakula vigumu vipya. Huu ni wakati wowote kuanzia umri wa miezi 8 hadi mwaka 1. Pia, unaweza kuelekeza zaidi na mtaalamu wa lishe ya watoto.

Vidokezo vya matumizi

Mwanzoni, inaweza kuwa busara kumpa mtoto viwango vidogo-vidogo vya maharagwe kama sehemu ya mlo mzima.

Wape watoto maharagwe kwa kiwango kidogo kwani viwango vya juu vya protini na nyuzi vinaweza kusababisha gesi.

Unaweza kuanza na dengu kwa kuwa ni rahisi kusaga, kisha aina nyingine za maharagwe.

Pika kwa njia rahisi ambapo maharagwe yanaweza kusagwa ama kupondwa ili kuwa laini na rahisi mtoto kutafuna na kumeza.

Njia bora ya kuhakikisha kwamba watoto wanapata kila kirutubisho cha kutosha ni kula mchanganyiko wa vyakula. Walakini, usichanganye aina nyingi za vyakula kwani huchanganya uwezo wa mtoto kuongeza ladha ya chakula.

Mpe mtoto chakula chenye kiungo kimoja mara ya kwanza. Hii hukusaidia kuona kama mtoto ana matatizo yoyote na chakula hicho. Subiri siku 3 hadi 5 kabla ya kumpa chakula kingine kipya. Hivyo, mtoto atafurahia vyakula vingi vipya.

Madini ya chuma (Iron) inayopatikana kwa maharagwe

Vitamini C imeonyeshwa kuimarisha mwili kunyonya madini ya chuma (Iron) inayopatikana kwa maharagwe. Changanya maharagwe na chakula kilicho na vitamini C kama vile mbogamboga ama kumywesha mtoto maji ya matunda (machungwa, tikiti-maji na kadhalika).

Sumu ya asili

Maharagwe yana sumu ya asili inayoitwa lectins. Maharagwe mabichi yanaweza kusababisha maumivu makali ya tumbo, kutapika na kuhara. Sumu hii ya lectin huondolewa wakati maharagwe yaliyokaushwa yanaloweshwa angalau kwa saa 12 kisha kuchemshwa kwa muda mrefu. Hivyo, hakikisha maharagwe yanapikwa vizuri kabla mtoto kulishwa.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *