- Binadamu, Kilimo, Nazi, Usindikaji

Jifunze kusindika nazi na kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali

Sambaza chapisho hili

Kusindika nazi

Katika msimu huu, nazi zinapatikana kwa wingi mashambani na sokoni na hivyo kufanya gaharama za uuzaji kuwa chini kidogo.

Hata hivyo pamoja na upatikanaji huu, wakulima na wauzaji wengi hawajafikiria namna ya kuongezea thamani zao hili ili kuzalisha bidhaa bora zaidi zenye soko na muda mrefu wa matumizi.

Mkulima Mbunifi unashauri kusindika nazi na kuzalisha bidhaa hizo ili kujiongezea pato.

Nazi husindikwa ili kupata bidhaa mbalimbali kama vile tui, mafuta, nazi kavu au jamu.

Kusindika nazi kupata tui

Tui la nazi ni bidhaa inayopatikana baada ya kukuna nazi na kuzikamua.

Vifaa

Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kusindika nazi kupata tui ni pamoja na kibao cha mbuzi cha kukuna nazi, jiko, sufuria au bakuli, chujio au kitambaa safi cha pamba, ungo, chuma au panga la kuvunja nazi na chupa.

Malighafi

Malighafi zinazohitajika ni pamoja na nazi yenye na maji safi na salama.

Jinsi ya kutengeneza

  • Chagua nazi zilizokomaa vizuri na vunja nazi vipande viwili kwa kutumia panga au chuma.
  • Kuna nazi kwa kutumia kibao cha mbuzi kisha weka maji kiasi ya uvuguvugu kwenye nazi iliyokunwa.
  • Kamua kwa kutumia chujio lenye matundu madogo au kitambaa safi cha pamba
  • Chemsha kwenye moto mdogo ukiwa unakoroga kwa muda wa dakika 15, kisha ipua na acha ipoe.
  • Weka kwenye chupa zilizochemshwa au makopo safi kisha funika kwa mifuniko safi na panga kwenye sufuria.
  • Weka maji ya kawaida kwenye sufuria hiyo hadi yafike nusu ya kimo cha chupa.
  • Chemsha kwa muda wa dakika 20 hadi 30 kisha ipua na weka lakiri na lebo.
  • Hifadhi kwenye sehemu safi.

Tui lililosindikwa kwa njia hii linaweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi mitatu, endapo chupa au kifungashio hakitafunguliwa.

Ukishafungua hifadhi yake huwa ni ya muda mfupi na ubora wake pia hushuka.

Matumizi

Tui hutumika katika mapishi mbalimbali kwa ajili ya kuongeza ladha na kuboresha virutubishi.

Virutubishi vilivyoko katika tui la nazi

Maji Asilimia 54
Wanga Gramu 6
Mafuta Gramu 35
Nguvu Kilokari 320
Protini Gramu 5
Vitamini A IU 37
Madini ya chuma Miligramu 2

Kusindika nazi kupata mafuta

Kuna njia mbili za kukamua nazi ili kupata mafuta nazi ambazo ni kukamua kwa kutumia mikono na kukamua kwa kutumia mashine.

Kukamua kwa kutumia mikono

Ili kukamua nazi kwa kutumia mikono kupata mafuta unahitajika kuwa na kibao cha mbuzi cha kukuna nazi, chujio au kitambaa safi, sufuria, bakuli kubwa pamoja na upawa.

Malighafi

Malighafi zinazotakiwa ni nazi zisizopungua 10 na zilizokomaa pamoja na maji safi na salama.

Jinsi ya kukamua mafuta

  • Chagua nazi zilizokomaa vizuri kisha vunja vipande viwili kwa kutumia panga au kipande cha chuma.
  • Kuna nazi kwa kutumia kibao cha mbuzi kisha weka maji ya uvuguvugu kiasi cha lita moja kwenye nazi zilizokunwa.
  • Kamua kisha chuja kwa kutumia chujio au kitambaa safi.
  • Rudia kwa kuweka lita moja ya maji kwenye machicha ya kamuo la kwanza na chuja.
  • Rudia tena kuongeza lita moja ya maji kwenye machicha na kuchuja mara tatu au nne ili kuhakikisha tui lote limetoka.
  • Acha tui kwenye chombo kwa muda wa saa 24 ili kupata malai (krimu).
  • Engua malai au krimu kisha chemsha na wakati wa kuchemsha koroga mfululizo kwa kutumia upawa ili kuzuia mashata kuganda kwenye chombo.
  • Endelea kuchemsha mpaka mlio wa kuchemsha utoweke kisha ipua na acha mafuta yapoe.
  • Mimina mafuta taratibu kwenye chombo kisafi kilichochemshwa kisha chuja mafuta yaliyobaki kwenye masimbi au mashata kwa kutumia kitambaa safi.
  • Yachemshe mafuta hayo kabla ya kuyachanganya na mafuta ya mwanzo.
  • Jaza mafuta kwenye chupa safi na kavu na hakikisha unatumia chupa zilizochemshwa na zenye mifuniko.
  • Hifadhi chupa zenye mafuta sehemu ambayo ni safi, kavu na pasipokuwa na mwanga mkali.

Njia hii ina ufanisi wa ukamuaji wa mafuta wa asilimia 64.

Kukamua mafuta kwa kutumia mashine

Kuna aina mbili za mashine zinazotumika kukamua mafuta kwa kutumia mashine ya ram na kukamua kwa kutumia mashine ya daraja (bridge press).

Mashine hizi huendeshwa kwa mikono lakini pia zipo mashine zinazoendeshwa kwa injini au kwa umeme. Mashine hizi zina uwezo mkubwa wa utendaji kazi kuliko mashine zinazoendeshwa kwa mikono.

Mashine hizi hukamua lita 65 hadi 600 za mafuta kwa saa kutegemeana na aina, ukubwa na ufanisi wa mashine.

Kukamua mafuta kwa kutumia mashine ya Ram

Mashine ya Ram huendeshwa kwa mikono na ina uwezo wa kukamua mbegu mbalimbali za mafuta.

Aina ya mashine hii iliyosambazwa kwa wingi vijijini ina ufanisi wa asilimia 85. Kwa kutumia mashine hii kilo 10 za nazi iliyokunwa hutoa wastani wa lita 5 za mafuta ya nazi.

Vifaa

Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kukamua mafuta ya nazi ni pamoja na mashine ya ram, kibao cha mbuzi cha kukuna nazi, beseni la kuwekea nazi iliyokunwa.

Pia, sufuria ya kukingia mafuta yatokayo kwenye mashine, mkeka wa kuanikia au karatasi la nailoni, chujio, panga au kipande cha chuma cha kuvunja nazi, chupa au vyombo vya kufungashia, lebo na lakiri.

Mahitaji

Malighafi yanayohitajika ni nazi safi zilizokomaa vizuri pamoja na maji safi na salama.

Jinsi ya kukamua mafuta

  • Chagua nazi zilizokomaa vizuri kisha vunja nazi hizo vipande viwili kwa kutumia panga au kipande cha chuma.
  • Kuna nazi kwa kutumia kibao cha mbuzi kisha anika juani hadi zikauke vizuri. Endapo utatumia machicha yaanike juani ili yakauke.
  • Jaza nazi iliyokunwa au machicha safi kwenye mpare wa kulishia.
  • Funga wenzozuia ili nazi zilizokunwa au machicha yasitoke.
  • Nyanyua wenzozuia mpaka juu ili kuruhusu malighafi kuingia kwenye silinda.
  • Shusha chini wenzozuia ili kuruhusu piston kusukuma malighafi ziingie ndani ya eneo la shindilio.
  • Nyanyua tena wenzozuia mpaka juu na kushusha na wakati huohuo ukiendelea kujaza malighafi kwenye mpare wa kulishia.
  • Wenzozuia ukiwa mzito ni dalili kuwa msukumo wa kutosha umejengeka. Msukumo huo utasababisha mafuta kutoka.
  • Mafuta yanapoanza kutoka legeza wenzozuia ili kuruhusu mashudu kutoka.
  • Chuja na jaza mafuta kwenye vyombo safi vyenye mifuniko, hifadhi sehemu kavu na isiyopenyesha mwanga mkali.

Kumbuka: Ukilegeza sana wenzozuia, utapata mafuta kidogo. Ukikaza sana utatumia nguvu nyingi kuendesha mashine na hatimaye kusababisha mashine kuharibika.

Kukamua mafuta kwa kutumia mashine ya daraja (Bridge press)

Mashine ya daraja ni moja ya mashine za kisasa zinazoweza kukamua mafuta ya nazi. Hukamua nazi zilizo na unyevu wa kati ya asilimia 11 hadi 14.

Mashine hizi huendeshwa kwa mikono na zina ufanisi wa kukamua mafuta kwa asilimia 68 hadi 72 ya mafuta yaliyopo kwenye nazi zilizokunwa.

Vifaa

Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kukamua ni kibao cha mbuzi, ungo au sinia la kuhifadhi nazi zilizokunwa, mkeka au makaratasi magumu kwa ajili ya kuanikia nazi.

Pili, chombo kikubwa cha kuchanganyia nazi zilizokunwa, vifuko vya nguo au viroba vyenye upana na urefu wa sentimita 20 na vyenye ujazo wa kilo moja.

Tatu, chupa za kuhifadhia mafuta, chombo cha kukinga mafuta pamoja na vyombo vitano vya kuwekea nazi zilizokunwa.

Pia, chujio kwa ajili ya kuchujia, mpare wa kumiminia mafuta, panga au kipande cha chuma cha kuvunja nazi pamoja na lebo na lakiri.

Malighafi yanayohitajika na nazi safi zilizokomaa vizuri.

Jinsi ya kukamua mafuta

  • Chagua nazi 40 zilizokomaa na zilizolingana kwa ukubwa.
  • Kuna nazi hizo kwa kutumia kibao cha mbuzi kisha anika nazi iliyokunwa juani kwa muda wa saa nne au zaidi kutegemea hali ya jua.
  • Weka nazi iliyokunwa kwa ujazo ulio sawa katika vyombo vitano vyenye ukubwa sawa.
  • Chagua nazi nyingine tano zilizokomaa kisha kuna nazi moja na changanya kwenye kile chombo chenye nazi iliyokaushwa juani.
  • Endelea kufanya hivyo kwa kila nazi kwenye vyombo vilivyobaki .
  • Gawa mchanganyiko wa kila chombo katika sehemu mbili zinazolingana kisha chukua kila sehemu ya mchanganyiko na jaza kwenye mifuko.
  • Hakikisha vifuko hivyo ni vya nguo na vimetayarishwa kwa usafi kisha funga vifuko kwa kamba.
  • Panga vifuko hivyo kwenye silinda na kuanza kuzungusha mhimili hadi mafuta yaanze kutoka kupitia kwenye matundu ya silinda.
  • Acha kwa muda mafuta yaendelee lutoka kisha endelea kuzungusha mhimili (kukamua) hadi mafuta yaishe. Mafuta yakiisha mhimili huacha kuzunguka.
  • Kusanya mafuta, chuja na fungasha kwenye chupa safi zilizochemshwa na zenye mifuniko na hakikisha chupa hizo ni kavu.
  • Weka lakiri na lebo kisha hifadhi mahali pakavu na pasipo na mwanga mkali.

Matumizi ya mafuta ya nazi

  • Hutumika katika mapishi mbalimbali.
  • Hutumika kwa ajili ya kupaka nywele na ngozi.
  • Hutumika kutengenezea siagi pamoja na sabuni mbalimbali.
  • Hutumika kutengeneza marashi, dawa za meno pamoja na shampoo.
  • Hutumika kulainisha mitambo na kukarabati maboti.
  • Hutumika kuchanganya na vyakula vya watoto vilivyosindikwa.

Kusindika nazi kupata mbata

Mbata ni nazi iliyokaushwa na kufikia unyevu wa kati ya asilimia 6 hadi 9.

Vifaa

Vifaa kwa ajili ya kusindika nazi kupata mbata ni chuma au panga la kuvunja nazi, jamvi, tanuru, kifulio na magunia.

Malighafi ni pamoja na nazi zilizokomaa vizuri, pamoja na kuni.

Jinsi ya kukausha

  • Chagua nazi bora zilizofuliwa kisha vunja nazi katika vipande viwili.
  • Kausha nazi kwenye tanuru au jamvi kisha tenganisha nazi na vifuu.
  • Endelea kukausha kwa muda wa wiki moja mpaka unyevu wa mbata uwe umefikia kati ya asilimia 6 na 9. Waweza kutambua mbata iliyokauka vizuri kwa kuivunja na kama imekauka itatoa mlio mkali na pia huwa angavu.

Kumbuka: Ni muhimu kukausha nazi vizuri ili kupata mbata na hatimaye mafuta bora. Nazi ambazo hazikukaushwa vizuri husababisha mafuta yatokanayo na mbata kuharibika na kuoza.

Mafuta yaliyooza yana harufu mbaya na hayafai kwa chakula. Hata hivyo mafuta hayo yanaweza kutumika kutengeneza sabuni na kukarabati maboti.

Kusindika mbata kupata mafuta

Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kusindika ni kisu au mashine ya kukata mbata, mashine ya kukamua mafuta ya ram au daraja, chujio au kitambaa safi, vifungashio, lakiri na lebo.

Malighafi ni mbata zilizo safi na zilizokaushwa na kuhifadhiwa vizuri.

Jinsi ya kukamua mafuta kutoka kwenye mbata

  • Kata mbata katika vipande vidogo visivyozidi unene wa nusu sentimita kwa kutumia kisu au mashine.
  • Weka kwenye mashine kisha kamua mafuta na chuja mafuta hayo kwa chujio au kitambaa safi.
  • Weka mafuta kwenye vyombo safi, vikavu na vyenye mifuniko.
  • Weka lakiri na lebo kisha hifadhi kwenye sehem kavu na isiyo na mwanga mkali.

Matumizi

Mafuta yanayotokana na mbata hutumika kwa kupikia vyakula mbalimbali ili kuongeza ladha na kirutubishi cha mafuta.

Vilevile hutumika katika kutengeneza sabuni, kulainisha mitambo, na kutumika kama mafuta ya ngozi na nywele.

Virutubishi vinavyopatikana kwenye gramu 100 za mafuta ya nazi ni nguvu kilokari 900 pamoja na mafuta gramu 100.

Kusindika nazi kupata unga

Vifaa vinavyotumika kusindika ni kaushio bora, kibao cha mbuzi cha kukuna nazi, mifuko ya kufungashia, panga au chuma la kuvunja nazi, sinia na mashine ya kusaga nazi.

Mahitaji ni nazi za kutosha zilizo safi na zilizokomaa vizuri.

Jinsi ya kutengeneza

  • Chagua nazi bora kisha kuna kwa kutumia kibao cha mbuzi.
  • Anika kwene kaushio bora ili kuzuia vumbi na uchafu mwingine kisha saga kwa kutumia mashine kupata unga.
  • Fungasha kwenye mifuko isiyopenyesha unyevu na hifadhi mahali pakavu na pasipo na mwanga mkali.

Matumizi

Unga wa nazi huchanganywa kwenye vyakula vya watoto, vitafunwa, mboga na vyakula vingine vya mizizi na ndizi.

Virutubishi vinavyopatikana kwenye gramu 100 za unga wa nazi ni kama ifuatavyo;

Maji Asilimia 2
Nguvu Kilokari 735
Wanga Gramu 20
Protini Gramu 6
Madini chuma Miligramu 3.6
Mafuta Gramu 70

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

3 maoni juu ya “Jifunze kusindika nazi na kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali

  1. Napenda kuifahamu zaidi hii kazi na cjui ntawapata sehemu gani hapa afrikca ya mashariki pia nahitaji machine ndogo ya kukamua mafuta nazi naomba mnijuze nami

    1. Habari, Karibu sana Mkulima Mbunifu. Sisi tunapatikana Mkoa wa Arusha Tanzania ndiko ofisi zetu zilipo lakini tunahudumia wakuli wote Afrika Mashariki hivyo kama utahitaji kututembelea karibu sana. Mashine kwa hapa Arusha unaweza kuzipata kupitia SIDO

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *