Moringa (Moringa spp.) maarufu kama mlonge ni miongoni mwa miti muhimu kwa matumizi ya binadamu, wanyama na hata katika kutengeneza virutubishi kadhaa.
Mti huu ukuao haraka hupandwa katika maeneo mengi na hutumika kama chakula cha binadamu, lishe ya mifugo, tiba mbadala na kusafisha maji.
Faida na matumizi ya mti wa Moringa
1.Virutubishi
Faida na matumizi ya mti wa MoringaKaribu kila sehemu ya mti wa Moringa inatumika au inalika kama chakula.
Majani ndio sehemu kuu ya mti wa Moringa, unaweza kuyala yakiwa mabichi au yakiwa yamepikwa kama mboga yoyote ya majani.
Unaweza ukayakausha na kuyahifadhi kama unga-unga kwa miezi mingi huku ukitumia kama kiungo kwenye mboga na mchuzi. Pia majani yanaweza kutumika kama lishe bora ya mifugo.
Utafiti wa kisayansi umeonesha kuwa majani ya Moringa ni chanzo kikubwa cha virutubishi. Virutubishi hivi ni pamoja na;
Vitamini C – Kirutubishi hiki ni muhimu katika kutengeneza kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali. Kiwango chake katika majani ya Moringa ni zaidi ya mara saba ya ile inayopatikana kutoka kwenye machungwa.
Calcium (madini chuma)- Kirutubishi hiki ni muhimu katika kuimarisha pamoja na kujenga mifupa na meno mwilini. Kiwango chake katika majani ya Moringa ni mara nne zaidi ya yale yanayopatikana kutoka kwenye maziwa.
Protini- Kirutubishi hiki ni muhimu katika kujenga mwili na kuimarisha ngozi. Kiwango chake katika majani ya Moringa ni mara mbili zaidi ya ile inayopatikana kutoka kwenye maziwa.
Vitamini A- Kirutubishi hiki ni muhimu katika kuimarisha macho na kuongeza uwezo wa kuona. Kiwango chake katika majani ya Moringa ni mara nne zaidi ya ile inayopatikana kutoka kwenye Karoti.
Potassium- Kirutubishi hiki ni muhimu katika kujenga na kuupatia mwili nguvu. Kiwango chake katika majani ya Moringa ni mara tatu zaidi ya ile ipatikanayo kutoka kwenye ndizi.
Maua ya Moringa yamejaliwa madini chuma (calcium) na Potassium kwa wingi na yanaweza kuchemshwa au kupikwa na kuliwa kama mboga.
2.Mboga
Majani ya Moringa huliwa kama mboga nyingine za majani kwa mfano mchicha. Majani yanaweza kuvunwa wakati wa kiangazi ambapo mboga nyingine hazipatikani.
Pia matunda mateke ya Moringa huweza kutumika kama mboga, hutayariswa kama maharage mabichi (machanga).Matunda yalikomaa hutoa mbegu ambazo zinaweza kutumika kama njegere au kukaangwa kama karanga.
3.Mafuta
Mafuta kutoka kwenye mbegu za mti wa Moringa huweza kutumika katika kupikia na kuwasha katika nyumba. Pia hutumika sana kwenye viwanda katika utengenazaji wa sabuni na bidhaa za urembo. Mafuta hukamuliwa kutoka kwenye mbegu kama ambavyo alizeti hukamuliwa.
4.Lishe ya Mifugo
Majani ya Moringa huliwa na ng’ombe, mbuzi, kondoo, sungura na kuku. Mbegu huliwa na kuku pamoja na wanyama wengine kwenye jamii ya ndege.
5.Pambo la nyumba
Mti wa Moringa hupandwa kwa wingi kwenye bustani kama ua au mti wa kivuli na hutumika katika upambaji. Pia miti ya moringa ikipandwa karibu karibu inaweza kutumika kama fensi.
6.Chanzo cha kipato
Mti wa Moringa ukitumiwa vizuri ni chanzo kizuri cha kipato. Mfano ni uuzaji wa miche ya mti wa moringa na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na moringa.