- Mifugo

Zikaushe mboga za ziada kwa matumizi ya baadaye

Sambaza chapisho hili

Kukausha mavuno kutoka shambani mwako, ni njia nzuri zaidi kukuwezesha kukabiliana na hali ngumu.

Kukausha mboga na matunda ni njia rahisi sana ya uhifadhi inayotumika duniani kote. Hata hivyo, ili kupata matokeo mazuri na bora, baadhi ya kanuni ni lazima zifuatwe.

Kukausha kwa jua

Jua hutumika kwa mazao ambayo hayaharibiki yanapokaushwa kwa kutumia jua moja kwa moja, mfano maharagwe, karanga au kahawa. Pia, nafaka ambazo zina wanga mwingi hazina madhara kutokana na ukaushaji wa kutumia jua. Mazao hayo yanaweza kutandazwa na kuanikwa sehemu ambayo yanapigwa jua moja kwa moja.

Kukausha kwa kutumia hewa

Aina nyingi za matunda na mboga ni lazima zikingwe dhidi ya mwanga wa jua, hii ni kwa sababu unaweza kuathiri ubora wake, ladha na rangi. Bidhaa yenye muonekano mzuri na ladha nzuri, kwa kawaida inaweza kupata bei nzuri muda wote.

Mbinu rahisi ni kukausha kwenye kivuli chini ya mti, chini ya paa, au kwenye chumba ambacho kina hewa ya kutosha. Kwenye kivuli ukaukaji ni wa taratibu mno, ambapo baadhi ya matunda yanaweza kuvunda kabla hayajakauka.

Ukaushaji kwa kutumia kifaa cha sola

Kwenye kifaa cha sola cha kukaushia vyakula, joto la jua hujikusanya, hivyo kufanya ukaushaji kuwa wa haraka zaidi. Kifaa hiki huwa na boksi jeusi au mfuniko mweusi ambao hukusanya mwanga wa jua na kuhifadhi joto. Bidhaa unayohitaji kukausha huwekwa ndani ya boksi.

Unaweza kuhitaji kujaribu kikaushio rahisi kwanza, na ukawa na sola yenye vyumba viwili. Endapo una soko zuri na unahitaji kukausha kiasi kikubwa, utahitajika kutengeneza kikaushio kikubwa zaidi na chenye ubora.

Maandalizi ya matunda na mboga

Matunda kama vile maembe, papai, mapera, na ndizi ni lazima yaivishwe kwanza, lakini yabakie kuwa magumu. Osha vizuri, menya na uondoe mbegu kama ni lazima, kisha uyakate katika vipande vinavyofanana. Kama ukiyatumbukiza kwenye juisi ya limao (kipimo kimoja cha juisi ya limao na vipimo vinne vya maji safi) yatabakia kuwa na rangi yake halisi kwa muda mrefu.

Mboga zenye majani manene na magumu (kama Kale na Kabichi) ni lazima zioshwe na kukatwa katwa, kisha kutumbukiza kwenye maji yaliyochemshwa yenye chumvi kwa muda wa dakika 2, kisha zikaushwe maji kabla ya kutandaza kwenye chombo. Inaweza pia kufanyika hivyo kwa maharagwe mabichi (Green beans) lakini usiyakate kate.

Muda wa kukausha kwenye kikaushio cha sola

Ukaushaji unategemeana na ukubwa na kiwango cha maji. Nusu nyanya inaweza kuhitaji jua la siku 2-3, wakati mboga za majani zinaweza kukauka kwa saa chache tu. Bidhaa zote zilizokaushwa ni lazima zihifadhiwe kwenye mifuko safi, na kuhifadhiwa kwenye sehemu kavu, isiyo na mwanga na yenye ubaridi. Unyevu, joto na mwanga vinaweza kusababisha kupoteza ubora.

Ukaushaji kwa kutumia chumba kimoja

  • Kwanza unahitaji trei au fremu yenye kitako imara, ambayo pia inaruhusu hewa kupita. Hata hivyo, unaweza kutumia trei tofauti tofauti. Unaweza kutengeneza trei kama iliyopo hapo chini na ukatumia fito nyembamba kutengenezea kitako.
  • Ukishajaza mazao yako kwenye trei unaweza kuweka juu ya paa la bati, au darini kama unaweza kufikia kwa urahisi. Bati ni lazima liwe na mteremko usiokuwa mkali.
  • Funika trei kwa kutumia kitambaa cheusi. Unaweza kuweka fito nyembamba ili kuhakikisha kuwa kitambaa hicho hakigusani na zao lako.
  • Sehemu ya juu unaweza kufunika kwa kutumia nailoni au kioo. Hakikisha kuwa upepo haupeperushi kitambaa hicho, na sehemu ya juu iwe na nafasi iliyo wazi ili kuruhusu unyevu kutoka.

Kanuni za jumla za ukaushaji wa vyakula

Uwazi: Ni lazima hewa iruhusiwe kuzunguka. Hewa safi ni lazima iwe inafikia zao unalokausha, huku unyevu ukiondoka kutoka kwenye sehemu ya kukaushia.

Usafi: Uandaaji katika hali ya usafi humlinda mlaji na ni muhimu kwa ajili ya bidhaa kudumu kwa muda zaidi. Trei zote, vitambaa au eneo la kukaushia ni lazima viwe safi. Osha, sugua, na ukaushe kabla haujavitumia . Muda wote osha mikono yako, na vifaa vyote unavyotumia kama vile visu kwa uangalifu.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *