- Kilimo, Mifugo

Uvunaji wa maji ya mvua kuhakikisha usalama wa chakula

Sambaza chapisho hili

Ni vema kutumia fursa mbalimbali kuhakikisha usalama wa chakula. Katika miaka ya hivi karibuni hali ya hewa imekua ikibadilika mara kwa mara na kusababisha taharuki kwa watu wengi hasa wakulima.

Mwezi wa kumi mwaka 2021, Mamlaka ya hali ya hewa (TMA) ilitoa tahadhari juu ya kiwango cha mvua kati ya mwezi Novemba 2022 had Aprili 2022. Taarifa hio ilieleza mvua za msimu zitakua chini ya kiwango na kwamba kutakua na kipindi kirefu cha ukame.

Taarifa hii inasaidia wakulima katika kupanga vema mazao ya kupanda muda huu na kujiandaa na vipindi vya ukame. Tunatambua ya kua, maji ni muhimu katika kuhakikisha mazao yanakua vizuri. Zaidi ni muhimu kuhakikisha usalama na uwepo wa chakula katika misimu yote.

Katika makala hii Mkulima Mbunifu itaangazia jinsi ya kuvuna maji kwaajili ya kilimo wakati wa kiangazi. Jambo hili linaweza kukuongezea kipato kwa asilimia 50 iwapo utaamua kulima mazao ambayo huadimika nyakati hizo kutokana na ukosefu wa mvua.

Matayarisho ya uvunaji maji ya mvua yanapaswa kufanyika mapema kabla ya msimu wa mvua kuanza ili mvua zinaponyesha uweze kuvuna maji na kuyahifadhi kwa matumizi hayo baadaye. Kumbuka maji ya mvua yanaweza kutunzwa kwa muda mrefu bila ya kuharibika.

Maji ya mvua yanaweza kuvunwa na kutumiwa kwa wakulima wenye maeneo yenye ukame na siyo wakati wa kiangazi tu.

Vifaa vinavyohitajika

Ili kuvuna maji mkulima anapaswa kuandaa vifaa vifuatavyo;

  • Turubai moja
  • Tanki la kuhifadhia maji
  • Nguzo 4 za miti zenye urefu wa mita mbili (2)
  • Bomba la Plastiki lenye ukubwa wa ¾

Eneo la uvunaji maji

Baada ya kukamilisha vifaa mkulima anapaswa kuhakikisha anachagua eneo linalofaa kwa uwekaji mtego wake wa kuvunia maji. Sehemu za muinuko na eneo la kilimo liwe katika mteremko kwa sababu itakuwa rahisi kufikisha maji bondeni kutoka kwenye tanki kwa kutumia njia ya mteremko (gravity).

Hatua za utengenezaji

Baada ya kukamilisha upatikanaji wa vifaa na kuchagua eneo.

  • Hatua ya kwanza ni kuanza kuchimbia nguzo kwa ajili ya kufunga turubai. Turubai linapaswa kubonyea katikati ili kutengeneza tumbo ambalo litaruhusu kuyapokea maji yanayovunwa. Chimbia nguzo yako kiasi cha nusu mita na kuacha mita moja na nusu ikiwa juu, ambayo itahusika kufungia turubai lako.
  • Hatua ya pili ni kutoboa tundu katika turubai lako. Tundu linapaswa kuwa na ukubwa wa kuruhusu bomba ambalo litaruhusu kuchukua maji yanayokusanyika katika turubai wakati wa mvua kunyesha na kuyahifadhi ndani ya tanki.
  • Hatua ya tatu ni kuweka tanki la maji chini ya turubai au eneo ambalo bomba lako litafika ili kuyakusanya maji na kuyahifadhi kwaajili ya matumizi baadae.

Uvunaji maji Zaidi

Ukihitaji maji zaidi inakupasa kuwa na matanki zaidi ili mvua zinapokuwa kubwa uweze kuvuna maji mengi zaidi kadri ya wingi wake na ukubwa wa ujazo wa matenki yako.

Unaweza kuandaa tanki la maji kwa saruji, kwa kulijenga juu au kuchimba shimo chini lenyewe uwezo wa kuhifadhi maji mengi. Changamoto ya tanki la saruji inaweza kuwa ni gharama kubwa za ujengaji na uvutaji maji kutoka ndani ya tanki hilo kwa ajili ya kumwagilia.

Faida za uvunaji maji

Uvunaji wa maji ya mvua unaweza kumsaidia mkulima kuboresha kilimo chake na kujiongezea kipato. Kwani mkulima anaweza kuamua kutumia maji hayo hasa kipindi kuna uhaba wa maji, nah ii itamuhakikishia usalama wa chakula. Aidha, anaweza pia kujiongezea kipato kwana atauza mazao hasa mbogamboga zile ambazo ni ngumu kupatikana wakati wa kiangazi.

Muhimu

Kwa wanaokusudia kujenga matanki ya uvunaji maji wanapaswa kuwasiliana na watalaamu wa ujenzi ili kusaidiwa namna ya kulijenga vyema. Hii itasaidia kutengeneza miundombinu ilio imara.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *