- Kilimo, Mifugo

Kilimohai kimenifungua macho na kunionyesha fursa za kilimo

Sambaza chapisho hili

“Mwanzoni ni kama nilikuwa gizani, sikuwa najishughulisha na kitu chochote Zaidi ya kukaa nyumbani, sikuwahi kujua kama nina nguvu na nikisimama kama mama bora naweza kuzalisha vitu mbalimbali kwa faida ya familia yangu, hakika mimi ni kipofu niliyeona”.

Ndivyo alivyoanza kueleza Bi. Renalda Lawrent, kutoka Kijiji cha Kambi ya simba (wilayani Karatu) ambaye kwasasa anajishughulisha na uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa misingi ya kilimo hai.

Maisha kabla ya kilimo hai

Bi. Renalda anasema kuwa, hapo mwanzo mara baada ya kuolewa, hakuwa akifanya kazi yeyote zaidi ya kuwa mama wa nyumbani, na mara moja moja kushiriki katika kilimo hususani uzalishaji wa mahindi ambao ulikuwa ukifanywa kulingana na msimu wa mvu pekee.

Hata hivyo, mazao hayo mara baada ya kuvunwa ndiyo hutumika kwa ajili ya kulisha familia na kuuza sehemu kidogo kwa ajili ya kununua mahitaji mengine ya familia kama nguo.

Mama huyu mwenye familia ya watoto 6 anaongeza kuwa, haikuwa kazi rahisi kuitunza familia yake kwa kile kidogo wanachozalisha, lakini hakuwa na suluhu nini afanye na hivyo kuhisi kuwa hivyo ndivyo tu maisha yalivyo.

Ilikuwaje mpaka kuanza kuzalisha kwa misingi ya kilimo hai

“Mwaka 2017, nilipata elimu ya ujasiriamali kupitia shirika la TRIAS walioweza kunifungua macho na kunifundisha wajibu wa mama katika familia, namna ya kuitumia nguvu yangu kwa faida lakini pia namna ya kuzalisha kwa wingi na kupata faida” alisema.

 

Bi.Renalda anaeleza kuwa, alipata mafunzo ya biogesi ambayo ina faida nyingi katika kilimohai na ni muhimu sana mkulima au mfugaji kuwa nayo nyumbani kwake.

Maisha baada ya kupata elimu ya kilimo hai

Nilikuwa nafuga ng’ombe hivyo mara baada ya kufundishwa kuhusu biogesi na kufungiwa mtambo nikaanza rasmi kutumia disemba 2017 na wakati huo huo nikaanza kuotesha migomba, maua, mbogamboga na kutengeneza shamba langu kwa mpangilio wa kilimo hai.

Baada ya miezi michache nilianza kuona faida ya kilimo hai kwani, biogesi yenyewe iliweza kunipatia moto ambao ulinipa uhuru na muda wa kutosha kuendeleza kilimohai kwani sikuwa na harakaharaka ya kukimbia kutafuta kuni hivyo nikaanza kufurahia kilimohai na kuweka juhudi sana shambani.

Hakuishia hapo tu, alianza kuzalisha mahindi yale yale katika shamba lilelile lakini kwa kutumia kilimo hai hivyo mavuno yakaongezeaka na chakula cha mifugo kikapatikana kwa wingi.

Niliweza pia kuona fursa, kwani mara baada ya kuanza kutumia bioslari katika migomba na katika shamba langu la mahindi, nilijiongeza kuanza kuzalisha malisho ya matete kwa ajili ya ng’ombe na kwa kutumia mbolea hiyo niliweza kupata malisho mengi ambayo nayakata mara kwa mara kulishia.

Faida za kilimohai

Bi. Renalda anaeleza kuwa toka aanze kuzalisha kwa misingi ya kilimo hai ameweza kupata faida mbalimbali kama ifuatavyo;

  • Kuzalisha mazao mbalimbali kwa kutumia gharama nafuu kwani malighafi zinazotumika zinapatikana katika mazingira ya nyumbani.
  • Kupata mavuno bora na mengi ya mahindi kuliko awali.
  • Kuweza kuzalisha matunda yatokana na migomba kwa ajili ya familia yake.
  • Kulibadilisha eneo la nyumbani toka kwenye ukame na kuwa kwenye ukijani ikiwa ni pamoja na kuweza kuotesha maua.
  • Kupata fedha kwa kuuza mazao mbalimbali kama mahindi ya kula pamoja na mbegu, ndizi, maziwa na mbogamboga.
  • Kupata moto wa uhakika masaa 24 bila kuhangaika na kupoteza muda kutafuta kuni lakini pia bila kuharibu misitu.
  • Kupata mbolea inayotokana na wanyama pamoja na mabaki mbalimbali ya mimea toka shambani.
  • Kushirika kwenye makongamano mbalimbali ya wakulima hivyo kupata fursa ya kujifunza Zaidi kwa wakulima wengine waliofanikiwa.
  • Kuwa na uhakika wa chakula cha mifugo msimu wote wa mwaka kwa kuhifadhi malisho ya ziada pamoja na kuwa nae neo la kuzalisha malisho pekee.

Vipi kuhusu Mkulima Mbunifu

“Jarida hili nilianza kuliona mwaka huu mwezi wa 10 katika maonyesho ya wakulima Karatu, na niliposoma nakala mbili tu niligundua kuwa lina manufaa kwangu kwani nimejifunza namna ya kupanua miradi yangu ya kilimo hasa kwa kufuga mbuzi na kuku lakini pia namna rahisi ya kuzalisha mbogamboga katika eneo dogo”alisema.

Bi. Renalda ameongeza kuwa, kupitia jarida hili ameona aina bora ya mbuzi na namna ya kufuga, na tayari ameshaanza kutafuta mbuzi hao ili aanze kufuga mapema mwaka 2022.

“Nimejifunza pia namna ya kuzalisha mbogamboga kwa kutumia mifuko hivyo naanza kukusanya mbolea kwa ajili ya uzalishaji. Nawashauri tu wakulima wengine wahakikishe wanapata nakala za jarida hili kwani kwa muda mfupi nimeona faida yake lukuki” aliongeza.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *