- Mifugo

Usimamizi bora wa ulishaji na udhibiti wa magonjwa katika ufugaji

Sambaza chapisho hili

Ulishaji na udhibiti wa magonjwa huchangia sehemu kubwa katika ufugaji. Ikiwa mfugaji atashindwa kuwapa mifugo wake lishe bora na kudhibiti magonjwa basi biashara ya ufugaji itadorora na kuleta mapato ya chini mno. Lishe bora na udhibiti mzuri wa magonjwa hurahisisha kazi ya mfugaji na kumhakikishia faida.

Lishe ni muhimu kwa mifugo ingawa sio kila chakula ni lishe kamili. Lishe kamili ni mchanganyiko wa vyakula mbalimbali ambavyo vina virutubishi vyote vinavyohitajika kwa mifugo kwa ajili ya ukuaji na uzalishaji. Hii ndio sababu wafugaji wanapaswa kulisha mifugo yao malisho yenye utajiri mkubwa wa virutubishi.

Kama lishe yoyote ya binadamu, mifugo inaweza kuwa na afya ikiwa italishwa chakula chenye virutubishi sahihi kilichochanganywa pamoja kwa uwiano sawia. Hii ina maana kuwa ni lazima mfugaji ahakikishe anasimamia lishe ya mifugo yake kwa umakini.

Makundi ya vyakula

Virutubisho ni sehemu ya vyakula ambavyo huwezesha viumbehai kuishi na kukua.

Virutubisho vya msingi ni pamoja na maji, protini (kujenga mwili), wanga (kuupa mwili nguvu, mafuta, vitamini na madini.

Unapofuga, ni lazima kuangalia katika mazingira yako kwanza kufahamu ni vyanzo gani vya virutubishi vinapatikana kwa urahisi, kwa bei gani au gharama kiasi gani.

Kwa mfano, kama kuna nyasi kwa wingi basi unatumia nyasi kama chakula cha msingi na kutafuta mbinu za kuzalisha nyasi ya hali ya juu. Kama ni mahindi, basi unatafuta mbinu za kuzalisha mahindi mengi yenye ubora na kwa gharama nafuu.

Mara baada ya kuwa na chakula kikuu, anza kuzalisha vyakula vingine au kununua kutoka kwa wakulima wengine, zingatia gharama ya jumla inakuruhusu kupata faida kutokana na ufugaji wako. MkM itaendelea kukupa vidokezo kuhusu ulishaji wa mifugo tofauti kama vile kuku, nguruwe, ng’ombe kila mmoja kwa namna yake kwa kuwa mahitaji ya kila aina ya mnyama ni tofauti.

Huwezi kufuga bila maji

Maji ni muhimu kwa kudumisha uhai. Maji yanahitajika kwa wingi kuliko kitu kingine chochote kinacholiwa au kunywewa na mnyama ndio maana ni moja katika makundi ya vyakula ya mifugo.

Vyanzo vya maji kwa mifugo ni pamoja na maji ya kunywa na maji ya kimetaboliki (yanayotolewa wakati wa umeng’enyaji wa chakula, yaani sehemu kubwa ya chakula vingi ni maji hasa nyasi na mbogamboga).

Unapoanza ufugaji, hakikisha una chanzo cha maji cha uhakika kwa mwaka nzima na kisichokauka.

Kuzuia magonjwa

Magonjwa ndio changamoto kubwa sana kwa wafugaji na yanaweza kukatiza na kumaliza kabisa uzalishaji kupunguza faida na kuvunja moyo wa mfugaji. Hivyo, lazima mfugaji kuweka mikakati tangu mwanzo wa mradi ya kukabiliana na magonjwa, na kuchagua njia inayofaa Zaidi kuweza kuzuia magonjwa kwa kadri awezavyo.

Wafugaji wana uzoefu tofauti na kwa viwango tofauti kulingana na maeneo na desturi. Usihofu kujenga uzoefu wako katika kupambana na magonjwa. Kuna wakati unaweza kupoteza mifugo mingi kutokana na magonjwa, lakini isiwe ndio sababu ya kuachana na ufugaji, ila iwe nafasi ya kujifunza na kufanya marekebisho.

Kutokana na uzoefu wa wafugaji, inaonyesha kwamba usafi na kuweka banda katika hali ya usafi, kulisha ipasavyo na kuwapatia maji safi, ndiyo njia kuu ya kupambana na magonjwa yaliyo mengi.

Watenge wanyama wapya

Unapoanza ufugaji, hakikisha kwamba wanyama unaowaleta shambani mwako ni wenye afya na hawaleti vimelea. Chagua wanyama wenye miili mzuri na wanaoonekana wenye nguvu na afya. Unaponunua mifugo wapya, tafuta ushauri wa afisa wa mifugo katika eneo lako au mkulima mwenzako mwenye uzoefu mkubwa ili akuelekeze vyema katika kuchagua wanyama wanaofaa.

Muhimu

Sio rahisi mfugaji kuuza mifugo yake yenye ubora, wengi wanauzwa sababu ya matatizo ya uzalishaji, na wengine wanauza mifugo yenye matatizo ya kiafya. Mkulima anayeanza ufugaji sharti awe makini asianze mradi wake na mifugo dhaifu. Wanyama wenye udhaifu watakuwa chanzo cha matatizo na changamoto kwa mfugaji.

Unapowaleta wanyama wapya bandani, watenge kwa muda wa wiki mbili au zaidi ili kujua changamoto zao na kuzuia maambukizi yoyote kwa wanyama wengine shambani au kuleta viini na vimelea kwenye banda.

Kwenye banda, ondoa matandazo yote, vyombo vya kulishia na kunyweshea pamoja na uchafu wote unaoonekana bandani. Safisha banda lote kwa kutumia maji na dawa kisha uache likauke na upulize dawa ya kuua wadudu kabla ya kuweka matandazo mapya na vyombo vya kulishia na kunyweshea.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na mtaalamu Bw. Eliudi Letungaa kwa simu 0754438136 au MkM kwa nambari 0717266007.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *