- Kilimo, Kilimo Biashara

Jifunze kilimo cha mwani na faida zake

Sambaza chapisho hili

Mwani wa bahari si mmea mgeni kwa wakaazi wa maeneo ya pwani. Wengi hukusanya kwa matumizi ya biashara na wachache hujumuisha katika mlo wao. Hivi karibuni, katika mitandao ya kijamii, wataalamu wa lishe wamekua wakishawishi watu kujumuisha mwani katika milo yao, wakisema kuwa mwani una faida nyingi kwa afya.

Mwani ni aina ya mimea inayoota na kukua kwenye maji chumvi (bahari) na maji baridi (mito, ziwa na mabwawa).

Tofauti iliyopo kati ya mwani na mimea mingine inayokua kwenye nchi kavu ni kwamba mwani hautegemei mizizi kufyonza maji na virutubisho vingine. Mwani hutumia sehemu zote za mmea kufyonza virutubisho vinavohitajika kutoka kwenye maji.

Aina ya jamii ya mwani inayolimwa nchini Tanzania kitaalam hujulikana kama Eucheuma denticulatum na pia huitwa Eucheuma spinosum. Aina nyingine ni Kappaphycus alvarezii kwa jina jingine Eucheuma cottonii.

Njia mbalimbali za kilimo cha mwani

Kutumia vigingi: Njia hii hutumika kwa kusimika vigingi chini na kufunga kamba kati ya vigingi ambapo mbegu za mwani hufungwa kwa kutumia taitai.

Kutumia chelezo – ‘raft’: Njia hii hufanyika kwa kufunga mwaniNkatika mianzi iliyounganishwa na kutiwa nanga. Njia hii hufanya mwani kuelea juu kabisa karibu na uso wa maji.

Kilimo cha mwani kwa kutumia chelezo

Uchaguzi wa eneo

  • Chagua eneo ambalo halina mawimbi makubwa ili yasiharibu mazao.
  • Epuka maeneo yaliyo karibu na mwingiliano wa mto.
  • Kiasi cha chumvi kwenye maji kinatakiwa kiwe kati ya gramu 27 hadi 35 za chumvi zilizoyeyushwa katika kilo moja ya maji.
  • Kiasi cha joto la maji liwe kati ya sentigredi 25°C and 30°C.
  • Kina cha maji kinatakiwa kisiwe chini ya futi 2 wakati wa kupwa kwa maji na zaidi ya futi 7 wakati wa kujaa.
  • Ardhi iwe imara ili kuruhusu usimikwaji wa vigingi.
  • Ardhi inatakiwa iwe na mchanganyiko wa mchanga na mawe.
  • Chunguza uwepo wa viumbe wengine wa bahari ambao wana uhusiano wa karibu na mwani, mfano samaki aina ya tasi. Hii ni dalili nzuri kuwa eneo linafaa kwa ajili ya kilimo cha mwani.
  • Zingatia pia upatikanaji wa nguvu kazi, vifaa shamba, miundombinu ya usafiri na mawasiliano.

Uchaguzi na maandalizi ya mbegu

  • Tumia kisu kisafi na chenye makali ili kupata mbegu bora.
  •  Ncha ya tawi la mbegu inatakiwa kuwa iliyonyooka.
  • Usitumie mbegu ambayo matawi yake yamekatika kwa juu.
  • Kabla ya kupanda, safisha mbegu na maji ya bahari kuondoa uchafu na vimelea vingine.
  • Nafasi kati ya mbegu moja na nyingine iwe sentimita 20-25.

Utunzaji wa shamba

  • Tembelea shamba angalau kila baada ya wiki mbili ili kuona vile zao lako linanawiri.
  • Ondoa mimea yote iliyokauka na kufa, na weka mipya iliyo michanga na yenye afya.
  • Ondoa uchafu ulioganda kwenye mwani kwa kutingisha matawi au kamba.
  • Funga kamba zilizofunguka.
  • Badili vigingi na mambo zilizoharibika;
  • Rudishia nanga zilizopotea.
  • Usiruhusu mimea kukua zaidi ya kilogramu 5 maana zitaharibiwa kwa urahisi na mawimbi au mvua.
  • Tunza kumbukumbu za mavuno na gharama za uendeshaji.
  • Iwapo shamba lina ukubwa wa hekta moja (ekari 2.5) na zaidi ni vema kuweka nyavu zenye ukubwa wa nchi 4 mwisho wa shamba ili kuzuia mimea isichukuliwe na mawimbi.

Uvunaji

  • Mwani huvunwa unapofikia uzito wa kati ya gramu 750 hadi 850.
  • Pita kwa kila shina ukivuna kwa kukata mazao yaliyo tayari kwa kutumia kisu kikali. Acha kiasi cha gramu 200 za mmea kwa ajili ya kuchipua tena.
  • Kama unataka kuvuna mwani wote kata shina lote kwa ujumla.
  • Unaweza kutumia wavu aina ya scoopnet kuchota mmea wote.
  • Kusanya mwani wote uliovunwa kwenye chombo (mtumbwi, boti, jahazi).
  • Peleka mwani katika eneo la kukaushia pindi chombo kinapojaa.
  • Hakikisha unapima uzito wa mwani uliovunwa kabla ya kuutandaza kwa ajili ya kukausha.

Ukaushaji wa mwani

  • Tandaza vizuri mwani kwenye eneo la ukaushaji.
  • Usianike mwani chini kwenye ardhi, tumia majani ya minazi, karatasi ya nylon, mwamba ili kuzuia uharibifu na uchafu;
  • Geuza mwani mara kwa mara na ondoa uchafu wote uliojitokeza. Kwa kawaida, mwani hukauka kwa muda wa siku mbili wakati wa kipindi cha jua.
  • Hakikisha hakuna maji yanagusa mwani wakati wa kukausha (funika mwani wakati wa mvua).
  • Tenganisha mwani wakati wa kukausha kulingana na siku ulipovunwa. Mwani uliokauka unakuwa na asilimia 30-35 za unyevu na asilimia isiyozidi 5 za mchanganyiko wa vitu vingine. Pia, unakuwa mlaini na unanata unapoguswa.
  • Ondoa chumvi iliyoganda kwa kutikisa mwani.
  • Pakia mwani msafi uliokauka kwenye magunia au mifuko mikubwa na hifadhi juu ya chanja. Usiweke mfuko moja kwa moja kwenye sakafu kuzuia unyevu.
  • Peleka sokoni tayari kwa kuuza.

Matumizi ya mwani

Mwani unaposindikwa, hutoa ute/gundi utumikao kwenye viwanda.

  • Gundi aina ya kappa carrageenan hutokana na mwani mwekundu na hutumika kwenye usindikaji wa vyakula, rangi za kupaka, dawa za meno, sabuni na shampoo.
  • Ute wa agar utokanao na mwani aina ya gracillaria hutumika kutengenezea vikuzio vya vimelea (culture media) kama bakteria na kuvu.
  • Mwani wa kijani hutumika kama chakula cha binadamu, wanyama na kutengeneza mbolea.

Kwa maelezo kuhusu kilimo cha mwani, wasiliana na: Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, S.L.P 2847 – 40487 Dodoma Simu: +255 (0)769220212, Nukushi: +255(0)2861908, E-mail: daq@uvuvi.go.tz

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *