- Mifugo

Unaweza kuepuka umaskini kwa kufanya kilimo cha mihogo

Sambaza chapisho hili

Zao la muhogo ni maarufu zaidi katika nchi za bara la Afrika. Zao hili hulimwa kwenye nchi zaidi ya 34 barani Afrika. Zao hili linajulikana zaidi kama mlinzi wa njaa kwa wakazi wa vijijini.

 

Asili ya zao la muhogo

Mihogo ni zao muhimu kwa chakula kwa nchi nyingi za Afrika na Amerika ya kusini. Kwa mara ya kwanza zao hili lililetwa barani Afrika na Wareno. Zao hili hulimwa kwenye hekari zaidi ya milioni 200. Kilimo cha mihogo huhitaji ujuzi kidogo sana na ni rahisi kulima.

Sifa za muhogo

Zao hili hustahimili ukame na huweza kubakia ardhini kwa muda mrefu kuepukana na baa la njaa. Upatikanaji wa mavuno ni wa uhakika kuliko mazao ya nafaka.

Mizizi ya mihogo ndio tegemeo kubwa la wakulima. Mihogo huwa na kiasi kikubwa cha Vitamini ‘A’ na kiasi kidogo cha protini.

Ulaji wa mihogo huwasaidia walaji kuepukana na ugonjwa wa ukavu macho. Majani ya mihogo hutumika kama mboga za majani (Kisamvu).

ZINGATIA: Kuna kemikali ijulikanayo kitaalamu kama Cynogenic glucoside ambayo inaweza kuwa sumu kama mihogo isipoandaliwa vizuri. Mihogo mitamu ina kiasi kidogo sana cha kemikali hii na huweza kuliwa hata mibichi.Hali ya hewa, udongo na mahitaji ya maji

  • Kwenye ukanda wa Ikweta zao hili hulimwa kwenye mwinuko wa mita 1500 kutoka usawa wa bahari.
  • Halijoto ya nyuzi 20-30° hufaa kwa kilimo cha mihogo.
  • Zao hili halistahimili maji yaliyotuama na hupendelea zaidi jua la kutosha.
  • Mihogo huzaa vizuri kwenye udongo tifutifu-kichanga wenye rutuba ya kutosha.
  • Mihogo huweza kuzalishwa kwenye sehemu iliyoathirika na mmomonyoko wa udongo ambapo mazao mengine hayasitawi.
  • Rutuba ikizidi sana ardhini mihogo huwa na majani mengi sana na mizizi kidogo.

Upandaji wa mihogo

Kupanda mihogo kwa kutumia mizizi (mihogo) iliyohifadhiwa haiwezekani kwa sababu mizizi haina vichipukizi.

Mihogo inapandwa kwa kutumia pingili za shina lake zenye urefu wa sm 20-30 na upana wa sm 2-2.5.

Vipingili vizuri ni vile vitokanavyo na sehemu ya shina iliyokomaa vizuri. Mimea kwa ajili ya mbegu inatakiwa iwe na umri wa miezi 8-14.

Kadiri mimea inavyokuwa na umri mkubwa ubora wake wa kuzalisha mbegu huongezeka.

Pingili ndefu ni nzuri kuliko pingili fupi. Mimea yenye afya nzuri tu itumike kwa ajili ya pingili.

Endapo zimeathirika kidogo zinaweza kutibiwa kwa kuzizamisha kwenye maji yenye joto la 50°C kwa dakika 15 kabla ya kupanda.Baada ya kukatwa vipingili visikae muda mrefu zaidi ya siku mbili.

Panda kwa kusimamisha, inamisha kidogo au kwa mlalo. Wakati wa kupanda epuka kugeuza vipingili juu chini kwani mihogo itazaa kidogo sana.

Nafasi

 Kama mihogo inapandwa peke yake nafasi huwa si sawa na endapo ikipandwa pamoja na mazao mengine.

Kama mihogo ikipandwa peke yake nafasi kutoka mmea hadi mmea ni mita 1. Kwa hiyo kwa eka, vipingili 4,000 vinatosha.

Sehemu nzuri ya kupanda mihogo ni sehemu yenye muinuko kiasi isiyotuamisha maji. Sehemu inayotuamisha maji mihogo hushindwa kutoa mizizi yenye afya.

Utunzaji wa shamba

Shamba lipaliliwe kila baada ya wiki 3-4 mpaka zifikie muda wa miezi 2-3 tangu kupanda.

Baada ya hapo mimea inaweza kufunika na kuzuia magugu yenyewe hivyo kupalilia sio muhimu sana.

Endapo shamba halina rutuba ya kutosha, mbolea ya samadi inafaa zaidi na mkulima anashauriwa kuongeza majivu kama ukuaji si mzuri.

Ni muhimu kuweka matandazo kwenye shamba la mihogo. Hii itasaidia utunzaji wa unyevu na uwepo wa rutuba kwa muda mrefu.

Unaweza kuzalisha mihogo kwa Mzunguko/mchanganyo wa mazao

Mazao ya mikunde kama karanga, kunde, hufaa kupanda pamoja na mihogo kwani huongeza rutuba ya udongo. Pia kuchanganya mihogo na mimea mingine husaidia kuthibiti mmomonyoko wa udongo.

Magonjwa ya mihogo

African Cassava Mosaic Disease (ACMD)

Ugojwa huu ni ugonjwa hatari zaidi wa mihogo barani Afrika na umeenea sehemu zote zinazolima mihogo Africa.

Ugonjwa huu husababishwa na kupanda vipingili vilivyoathiriwa na wadudu weupe wa mihogo. Huu ni ugonjwa hatari zaidi kwani husababisha hasara ya zaidi ya asilimia 90%.

Dalili

Dalili za awali za ugonjwa huu ni muonekano wa michirizi meupe hasa kwenye majani.

Nini cha kufanya

  • Tumia vipandikizi visivyo na ugojwa huu. Inashauriwa kutumia vipingili kutoka kwenye matawi ya mihogo na siyo kwenye shina. Hii ni kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na ugonjwa huu kwenye shina kuliko kwenye matawi.

Mnyauko bakteria (cassava bacterial blight)

Ugonjwa huu ni kizuizi kikubwa cha kuzalisha mihogo hapa Afrika.

Dalili

  • Mwanzoni ugonjwa huu huonekana kwenye majani.
  • Majani huonekana kama yameloweshwa kwa maji.
  • Ugonjwa ukishamiri majani huanza kudondoka.
  • Wakati wa unyevu unyevu bacteria hutoa uchafu kama gundi chini ya majani.
  • Ugonjwa huu huenezwa sana kwa kutumia vapandikizi vilivyoathirika pamoja na matone ya mvua.
  • Wadudu kama vile panzi hueneza ugojwa huu pia.
  • Mkulima pia huweza kueneza huu ugojwa akipita shambani wakati au baada tu ya mvua.

Nini cha kufanya

  • Tumia vipandikizi salama visivyo na ugojwa huu.
  • Inashauriwa kuchanganya mihogo na mahindi au tikiti maji ili kupunguza ugojwa huu.
  • Fanya mzunguko wa mazao na ikiwezekana pumzisha ardhi.
  • Ondoa na choma mimea yote na magugu shambani au kwatua na kuyafukia chini ya ardhi.

Ugonjwa wa madoa ya majani (Brown leaf spot)

Majani yaliyokomaa tuu ndio yanayoonesha dalili za ugojwa huu. Majani huonekana yakiwa na madoa ya kahawia, baada ya muda huwa njano na mwisho kudondoka.

Cassava brown streak virus disease (Potyvirus Potyviridae)

Ugonjwa huu ni hatari zaidi ukanda wa pwani na Zanzibar na huenezwa na wadudu weupe wa mihogo na pia kwa kupanda vipingili vilivyo na ugonjwa huu.

Majani huonekana ya njano ila wakati mwingine majani huweza kuonekana yana afya nzuri wakati mizizi imeshaoza kwa kiasi kikubwa.

Hifadhi Mihogo Mikavu (Chipsi Au Makopa)

  • Njia pekee ya kuhifadhi mihogo kwa muda mrefu ni kwa kuhifadhi mihogo iliyokaushwa. Muhogo uliokaushwa huweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi 6 hadi 12 bila kuharibika.
  • Makopa yanashambuliwa na dumuzi zaidi kuliko chipsi.
  • Inashauriwa kuhifadhi mihogo iliyoparuliwa na kukaushwa (chipsi) ambayo inakuwa katika hali ya unga unga na kufanya mashambulizi ya dumuzi yapungue kabisa.
  • Chipsi za mihogo zinaweza kuhifadhiwa katika magunia safi ya juti na kupangwa ndani ya ghala juu ya chaga.
  • Chipsi zinaweza kuhifadhiwa katika hali ya kichele ndani ya sailo au kihenge bora.
  • Mihogo haihifadhiwi kwa kutumia dawa za viwandani.
  • Hifadhi kwa hali ya ukavu, usafi na kagua ghala mara kwa mara kuona kama kuna mashambulizi ya panya.
  • Chukua tahadhari kuepuka upotevu wa chakula hicho.
  • Hifadhi kwa muda ulioshauriwa ili kudumisha ubora wa bidhaa hiyo.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Unaweza kuepuka umaskini kwa kufanya kilimo cha mihogo

  1. Suwali naomba nitajie Nchi nne maarufu zinazo ongoza kwa uzalishaji wa zao la muhogo africa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *