- Kilimo, Mifugo

Kilimo hai ni rafiki kwa mazingira

Sambaza chapisho hili

Njia nyingi zinazotumika katika kilimo siyo rafiki na mazingira. Njia za kawaida/ mazoea za kilimo ikiwemo, kilimo cha kuhama hama, kufyeka misitu na kuchoma majani/mabaki, vyote husababisha uharibifu wa mazingira.

Maana ya Kilimo rafiki kwa mazingira

Hii ni aina ya kilimo chenye kutumia mbinu bora za kilimo zenye tija kwa mkulima na kuyalinda mazingira. Ni mfumo unaohusisha ulimaji / matumizi ya udongo na mazao kwa utaratibu ambao hupunguza mmomonyoko wa udongo na utoaji wa hewa ukaa mashambani.

Kwa nini tunahitaji Kilimo rafiki na Mazingira

Kilimo kinachangia kati ya asilimia 10 -14 ya hewa ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia nchi, na wanaoathirika zaidi na athari za mabadiliko ya tabia nchi ni wakulima wenyewe kwa kuwa hutegemea kilimo kwa asilimia 100.

Njia zinazotumika katika kilimo siyo rafiki na mazingira, njia za kawaida/ mazoea za kilimo ikiwemo, kilimo cha kuhama hama, kufyeka misitu na kuchoma majani/mabaki mashambani vyote husababisha uharibifu wa mazingira Tanzania na duniani kwa ujumla.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo wakulima wadogo wadogo wanashauriwa kutumia mbinu/njia bora za kilimo ambazo zitasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kupunguza umasikini.

Mbinu za Kilimo rafiki na Mazingira zinazoshauriwa

Kutifua udongo kwa kiwango kidogo (mabeseni)

Mbinu hii ni ile inayofanyika kwa kupanda moja kwa moja kwenye udongo bila kutifua au kuchimba mashimo ya kupandia bila kulima kwa mkono, trekta au plau.

Kutifua udongo kwa kiwango kidogo au kutotifua kabisa kunaongeza uwezo wa ardhi kuhifadhi maji, kuingiza hewa, kurahisisha kunywea maji, kupata joto na kuhifadhi hewa ukaa ndani ya udongo.

Tunapolima kwa kutifua ardhi kwa mazoea mara nyingi tunasababisha ardhi kutoa hewa ukaa ambayo mara nyingi huhifadhiwa ardhini. Muundo wa udongo ambao hurahisha maji kuingia kwa urahisi kwenye udongo huharibika na hivyo kusababisha mmomonyoko wa udongo.

Kufunika ardhi muda wote

Mbinu hii ya kufunika ardhi ina lengo la kuukinga udongo kutokana na jua kali na mvua kubwa. Tunazuia mmomonyoko wa udongo na kuhifadhi unyevu. Kuna aina mbili za kufunika ardhi ambazo ni:-

Kufunika udongo kwa kutumia Matandazo (vitu vikavu)

Mbinu hii ni ya kutumia magugu, misitu, majani, matawi, vijiti, na mabua katika kufunika udongo huongeza kasi ya kazi za viumbe hai ndani ya ardhi, maji yaweza kunywea ndani kiurahisi, na hupunguza mmomonyoko.

Matandazo yanapo oza tunapata mboji inayoshikiza sehemu za udongo vizuri ili zisichukuliwe na maji na hivyo kuongeza rutuba ya udongo.

Matandazo hutoa chakula cha wadudu rafiki waishio udongoni, kuzuia magugu, udongo haupati joto kali na kukakamaa.

Kufunika udongo kwa kuacha masalia ya mazao

Mbinu ya kufunika udongo kwa kuacha masalia ya mazao shambani hufanyika pindi mkulima anapomaliza kuvuna mazao ya msimu uliopita.

Masalia ya mazao kama mahindi, maharagwe, mtama, alizeti yakatwe na kulazwa juu ya udongo ili kuzuia Matone ya mvua na jua kupiga ardhini moja kwa moja.

Kufunika udongo kwa kutumia mazao funika

Mbinu ya kufunika udongo kwa kutumia mazao funika hufanywa kwa kupanda mazao shambani kwa lengo la kurundika virutubisho vya zao muhimu kabla na baada ya msimu wa kupanda mazao pamoja na kupunguza mmomonyoko na kuhifadhi unyevu wa ardhi.

 

Mimea hii huchanganywa na ile ya mazao muhimu na yanaweza kuachwa shambani baada ya kuvuna mazao. Matumizi ya mazao funika huongeza naitrojeni kwenye udongo. Mara nyingi mimea inayopandwa ni ile isiyokuwa na ushindani wa mwanga kwenye zao muhimu.

Ni mbinu inayotumika kutengeneza matuta ya kudumu kwenye maeneo yenye miinuko. Fanya juu ni mfereji uliopimwa upana, kina na urefu kulingana na shamba.

Udongo huchimbwa toka mferejini na kuwekwa upande wa juu na wakati mwingine mawe na vijiti hutumika kuzuia matuta hayo.

Mifereji hii hutengenezwa katika shamba kwa madhumuni ya kupunguza kasi ya maji na kuzuia udongo usiporomoke kuelekea bondeni au kwenye shamba la jirani.

Aina hii ya kilimo hufaa zaidi kwenye mashamba yenye mwinuko wa asilimia 12%- 35%. Shughuli ya kutengeneza fanya juu ni kubwa hasa katika hatua ya awali ya kilimo bali siku zinavyozidi kwenda kazi hupungua na kubakia kuufanyia marekebisho tu.

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *