- Mifugo

Umuhimu wa maji katika mnyororo wa ongezeko la thamani

Sambaza chapisho hili

Kwa muda mrefu sasa sehemu kubwa ya nchi ya Tanzania imekumbwa na ukame. Hali hii imefifisha kwa kiasi kikubwa shughuli za wakulima na wafugaji kwa kuwa asilimia kubwa hutegemea mvua.

Kama wasemavyo maji ni uhai sio kwa binadamu peke yake, hata kwa wanyama na mimea pia.  Kwa mkulima kutegemea mvua hawezi kuwa na kilimo cha kibiashara kwa kuwa hana uhakika mvua itanyesha lini, na kwa kiasi gani, ili atayarishe shamba kwa wakati na vile vile kuweka mbegu aradhini.

Kutokuwa na uhakika wa mvua itanyesha lini mkulima hawezi kujua lini ajipange na palizi na vile vile kuwa na uhakika wa mvua ya kukuzia mazao.

Mkulima hatakuwa na uhakikika kuwa mvua itakatika lini ili mazao yake yaliyo shambani yakauke tayari kwa kuvunwa. Ndio sababu mkulima anayetegemea maji ya mvua ni vigumu kuwa na kilimo cha kibiashara kwani hawezi kujua atavuna kiasi gani ili kumhakikishia mnunuaji upatikanaji wa mazao.

Katika hali hii uwezekano wa kutumia mbegu bora, mbolea sahihi unakuwa wa mashaka kwani mkulima hana uhakika na uzalishaji katika aina ya kilimo anachofanya.

Kilimo cha umwagiliaji kinachotokana na maji yaliyovunwa au yaliyojengewa kutoka kwenye vyanzo vya maji au kwa kutumia maji yaliyo chini ya ardhi ni muhimu katika kufanikisha kilimo cha kibiashara.

Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo vya maji ya kutosha kinachotakiwa ni mipango mizuri ya uvunaji na matumizi ya maji hayo.  Licha ya kuwa bado hatujafanya bidii kubwa kujenga utaratibu wa kuvuna maji na kuyatumia kwa njia sahihihi bado tunatumia asilimia 21% peke ya miundo mbinu ya umwagiliaji iliyopo.

Mbinu za kilimo biashara kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani itafanya gharama za maji ziwe ni miongoni mwa gharama ambazo lazima zibebwe na mlaji ambazo zitajumuishwa kwenye gharama ya kuuza bidhaa.

Ili kuwa na matumizi mazuri ya maji ni lazima jamii iwe na mpango wa usimamizi, wa kutunza vyanzo vya maji matunzo ya miundo mbinu na ugawaji wa maji usiokuwa na upendeleo.  Lazima maji yawe na gharama na kila mtumiaji maji awe anatambua kuwa kila atakapotumia maji kwa kasi fulani itabidi alipe.

Hali ya hewa; changamoto kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani

Kwa mwaka huu wa kilimo tumeona jinsi hali ya hewa hasa kwa vikundi vya wakulima wa mpunga wilayani kilombero walivyoathirika na hali ya hewa mbaya ambayo mvua za vuli hazikunyesha na uwezekano wa mvua ya masika kutokuwa ya kutosha.

Hali ya hewa ya ukame iliwaathiri hata wanavikundi kwenye skimu za umwagiliaji kwani kutokana na ukame hata skimu za umwagiliaji hazitakuwa na uzalishaji wa kutosha mwaka huu kutokana na kukosa maji ya kutosha.

Ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji iko haja ya kuwa na mabwawa ambayo yatahakikisha upatikani wa maji kwenye msimu wa kilimo.  Hii ina maana vyombo vya fedha vikishirikiana na sekta binafsi kuna uwezekano wa kuvuna maji ya mvua ambayo yanaweza kuuzwa  kama bidhaa nyingine.

Wakulima hawatakuwa na matatizo ya kununua maji kwa ajili ya kilimo ali mradi gharama za maji zinaweza kubebeka kwenye bei ya bidhaa kwenye soko.   Kama ilivyoelezwa hapo awali faida ya kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani, ni kubwa na gharama zote zile kutoka kuzalisha, kusindika na kuuza zinaweza kubebwa na bei ya mauzo.

Katika mkakati wa kuvuna maji ya mvua na kuuza kuna haja ya sekta binafsi kufanya utafiti na kuandika mpango biashara utakaoonesha kiuhalisia gharama zote za kujenga miundo mbinu, mkakati wa kuuza bidhaa ya maji, ukusanyaji wa mapato na vihatarishi vya aina yoyote ambavyo vinaweza kuwa ni kikwazo kwa biashara kufanakiwa.

Ili kukabiliana na hali ya hewa isiyotabirika kuna ulazima wa kuangalia uwezekano wa kujenga visima virefu ambayo vinatoa maji kwenye mito mikubwa ambayo iko chini ya ardhi ambayo inaaminika kuwa si rahisi kukauka.

Tatizo la mafuriko lazima nalo liangaliwe kwa umuhimu wake na kutengeneza mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.

Mikakati ni pamoja na kujenga mitaro ya kuhamisha maji yaliyozidi kwenye mashamba.  Kuwa na bima ni kati ya mikakati ingawa bima ni suluhu ya mwisho kwani madhumuni ya biashara ya kilimo ni kuzalisha, kusindika na kuuza.  Kutokuwa na mazao ya kutosha hata kama bima inaweza kutumika kupunguza madhara ya hasara bado ni tatizo ikiwa hali ya hewa itazuia upatikanaji wa mazao.

Mkakati mahususi wa kukabiliana na upatikanaji wa uhakika wa maji utachangia kwa kiwango kikubwa sera ya kilimo chenye tija.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *