- Mifugo

Ulishaji wa chakula bora kwa kuku hupelekea utagaji wa mayai mengi na yenye ubora

Sambaza chapisho hili

Wafugaji walio wengi mara kwa mara wamekuwa wakilalamika sana hasa katika msimu wa baridi kuwa kuku hawatagi ama wakitaga basi utagaji wao huwa hafifu tofauti na msimu wa joto.

Jambo hili limekuwa la kawaida sana na wafugaji wengi wamekuwa hawajishughulishi na ulishaji bora kwa kuku katika msimu wa baridi huku wakilisha vyema katika msimu wa joto.

Hii si sawa kwani kuku wanaweza kutaga wakati wowote ikiwa tu watapata chakula bora chenye virutubisho vyote na cha kushiba.

 

Chakula bora ni nini

Chakula bora ni kile ambacho kimetengenezwa kwa njia iliyokidhi upatikanaji wa viinilishe vyote vinavyoweza kujenga mwili wa kuku na kupelekea uzalishaji bora.

Chakula hiki lazima kiwe kinampatia kuku kiasi  cha virutubisho vinavyohitajika mwilini kama; wanga, protini, vitamini, madini  pamoja na maji. Hivi vyakula vitasaidia kujenga, kulinda na kukinga mwili dhidi ya magonjwa, kuupa mwili nguvu na uzito pamoja na kunenepesha.

Ili kuku atage anahitaji chakula cha aina gani?

Kuku wa asili au wa kienyeji ili aweze kutaga mayai wakati wote, hakikisha unawapa chakula chenye mjumuisho kama ufuatao; mahindi, pumba za mahindi, soya, mashudu ya alizeti/mashudu ya pamba, dagaa iliyokaushwa, damu, mifupa iliyosagwa, chokaa, chumvi na vitamini.

Vyakula hivi vyote vinahitajika kuchanganywa kwa kiwango maalumu ili kuwezesha upatikanaji sawa wa viinilishe katika mwili na kupelekea uzalishaji bora na wenye tija.

Mchanganyiko sawia wa chakula

Chakula hiki unaweza kununua kwenye maduka ya vyakula vya mifugo ama ukatengeneza wewe mwenyewe. Jambo la msingi ni kuhakikisha mchanganyiko utakaonunua au kutengeneza una makundi yote ya vyakula na kwa kiwango kinachohitajika.

 

Unaweza kutengeneza chakula kwa mchanganyiko huu;

Malighafi aina ya kwanza na kiwango

Mahindi kilogramu 40, pumba ya mahindi kilogramu 25, mtama kilogramu 5, mashudu ya alizeti kilogramu 10, dagaa kilogramu 4, damu kilogramu 5, mifupa iliyosagwa kilogramu 4.50, chokaa kilogramu 4, vitamini kilogramu 2, na chumvi kilogramu 0.50.

Mchanganyiko huu wote utaleta jumla ya kilogramu 100 za chakula. Hivyo utakapolisha kuku, watakuwa wamepata viini vyote kwa uwiano sawia unaotakiwa mwilini.

Malighafi aina ya pili na kiwango

Aidha, unaweza pia kujumlisha mchanganyiko huu na ukawa na uwiano sawa wa virutubisho kama ulivyo mchanganyiko wa kwanza.

Dagaa kilogramu 4.5, soya kilogramu 18, mahindi kilogramu 50, pumba ya mahindi kilogramu 15, mashudu ya pamba kilogramu 5, mifupa iliyosagwa kilogramu 3, vitamini kilogramu 2, chumvi nusu kilogramu (0.5) na chokaa kilogramu 2. Yote jumla kilogramu 100.

Mara utakapotengeneza chakula hiki, hakikisha unakihifadhi sehemu salama, kavu na yenye hewa safi. Ni vyema kutengeneza chakula kwa kiwango kidogo ili kisikae sana muda mrefu bila kutumiwa kuepusha uharibifu.

Unaweza kutengeneza chakula cha kilogramu 50 badala ya 100, kwa mchanganyiko huo huo, isipokuwa kiwango katika kila malighafi Utagawa nusu yake.

Muhimu: Hakikisha chakula utakachokitengeneza, malighafi zote ni kavu, na hazijakaa muda mrefu wala hazijapata uvundo wala ukungu. Hii itasaidia kuhakikisha ubora wa chakula na kuepusha kuku kupata magonjwa yatokanayo na sumu kuvu.

Banda la kuku lisikose maji masafi, salama naya kutosha wakati wote. Vyombo vya maji visafishwe kila siku kabla ya kuweka maji mengine.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Linus Prosper kwa simu namba 0692 792 797 au 0756 663 247

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

7 maoni juu ya “Ulishaji wa chakula bora kwa kuku hupelekea utagaji wa mayai mengi na yenye ubora

    1. Asante sana nahitaji kufuga kuku wa mayai ila wawe wa kienyeji nahitaji msaada wako hapo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *