- Mifugo

Miaka tisa nikitumia jarida la Mkulima Mbunifu na kupata mafanikio lukuki

Sambaza chapisho hili

Mipango thabiti huzaa matunda mema na kila jambo likiwekwa katika mipango imara husababisha mafanikio.

Hayo ni maneno ya Mzee Goodluck Lazaro Kimario na mkewe Rose Goodluck Kimario ambao ni miongoni mwa wakulima wa muda mrefu na wanufaika wa jarida la Mkulima Mbunifu.

Wakulima hawa walikua wakiishi wilaya ya Tarime mkoani Mara ambapo mzee Goodluck alijishughulisha na majukumu ya kanisa huku akiwa muajiriwa wa serikali kama Afisa kilimo wilaya ya Tarime.

Mzee Goodluck alianza kupokea majarida ya Mkulima Mbunifu na pia jarida mama la TOF (The organic farmer Magazine) akiwa Tarime tangu mwaka 2011.

Mnamo mwaka 2013 alistaafu kazi za kanisa na kuhamia Arusha katika wilaya ya Meru ambako aliendelea na shughuli za kilimo huku akiendelea kusoma jarida la MkM.

Kwanini anajivunia jarida la Mkulima Mbunifu

Mzee Goodluck analisifu jarida la Mkulima Mbunifu kwa sababu, kwa muda wote akifanya kilimo amekua akizingatia kilimo endelevu na amejifunza bunifu mbalimbali za kilimo kupitia jarida la Mkulima Mbunifu ambazo ametumia kufanya kilimo mpaka sasa.

Katika miradi yake ya kilimo, anafanya ufugaji wa kuku wa kienyeji, ng’ombe wa maziwa na mbuzi, pia anafanya kilimo cha mazao mchanganyiko kwa kutumia mbolea ya samadi na zaidi amejikita katika kilimo cha migomba, mahindi na maharagwe. Kwa sasa anaandaa shamba ili kufanya kilimo cha papai.

Aidha, wazee hawa waliamua kutengeneza mtambo wa kuvuna maji ya mvua ambayo huyategemea kwa matumizi ya nyumbani na pia kwa ajili ya mifugo wakati wa kiangazi kikali.

 

 

 

Kwa nini kilimo endelevu

Mzee Goodluck aliamini kuwa kilimo ndio msingi wa maisha. Pia akiwa katika ajira alitambua kua kazi hiyo itafika kikomo ambapo atahitajika kustaafu. Kwa mantiki hiyo, aliandaa mazingira ambayo yatakayomuwezesha kumudu maisha baada ya kustaafu.

Kupitia kilimo endelevu ameweza kuzalisha mazao bora na kupata kipato kilichomsaidia kusomesha watoto hadi ngazi ya chuo kikuu. Lakini pia kipato hicho ameweza kukitumia kupanua miradi ya kilimo na kuendeleza majengo ambayo wanaishi kwa sasa jijini Arusha.

Mzee Goodluck na mkewe wanapata wastani wa shilingi za kitanzania milioni moja na nusu (1.5m/TZS) kutokana na ufugaji pia kilimo  kila mwezi.

Walifuga ng’ombe wawili (2) ambao kwa siku ng’ombe mmoja hutoa lita 20-25 za maziwa ambayo anauza kwa bei ya kati 800/- hadi 1,000/- kufuatana na msimu.

Katika kilimo cha mahindi, mkoani Arusha analima shamba la ekari 2 ambapo kwa hizo ekari 2 alipata gunia 25. Mahindi hayo huyahifadhi kwenye mapipa bila kuweka dawa yoyote na kuuza msimu ambapo bei imenzuri. Hata hivyo alitenga gunia 10 kwa ajili ya matumizi ya familia.

Ushauri kwa wastaafu

Bwana na Bibi Goodluck Mushi wanashauri wafanyakazi wote ambao bado hawajastaafu kutobweteka na kazi zao, kwani ni muhimu kuwekeza kwa ajili ya maisha baada ya kustaafu.

Waanzishe miradi mingine na hasa katika nyanja ya kilimo kwani chakula hutoka shambani na ni vyema kujizoesha kula ulichopanda shambani kwako kuliko kutegemea kununua kila wakati.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na Bw na Bi Goodluck kwa simu +255(0)784454790

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *