- Mifugo

Ugonjwa wa ng’ombe wa mapele ngozi

Sambaza chapisho hili

Ugonjwa wa mepele ngozi, ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vijulikanavyo kisayansi kwa jina la Capri poxvirus. Takribani asilimia 5 hadi 50 ya ng’ombe katika kundi wanaweza kupatwa na ugonjwa huu, ambapo ng’ombe wa umri wowote anaweza kupatwa na ugonjwa huu. Ugonjwa wa mapele ngozi hauambukizwi kwa binadamu.

Chanzo cha maambukizi na namna ugonjwa unavyoenea

  • Maji maji yanayotoka kwenye vidonda na mate ya ng’ombe mgonjwa huwa na virusi vya ugonjwa huu na hivyo kuwa chanzo cha maambukizi.
  • Mate, mapele na makamasi ya ng’ombe mgonjwa ndiyo chanzo cha maambukizi ya ugonjwa huu kwa ng’ombe wazima.
  • Virusi vinaweza vilevile vikaenezwa na nyasi kutoka sehemu yenye ugonjwa.
  • Wadudu wanaouma jamii ya inzi wanaweza kueneza ugonjwa huu pale wanapomuuma ng’ombe mgonjwa na kwenda kumuuma ng’ombe mzima.
  • Ng’ombe jike wanaweza kuambukizwa kwa kupandwa na dume lenye ugonjwa.

Dalili kuu za ugonjwa huu

Ng’ombe kuwa na mapele ya mviringo katikati ya ngozi hasa sehemu za kichwani, shingoni, sehemu ya chini ya ng’ombe, hasa miguuni na kwenye kiwele.

Ugonjwa huu ambao upo katika kundi la magoonjwa ya ndui, mapele yake huonekana kama manundu na  ni magumu, na kipenyo chake ni kati ya sentimita 1 hadi 4, ambapo hufikia hatu yanapasuka na kuwa vidonda. Ngombe mwenye ugonjwa huu huonyesha dalili zifuatazo;

  • Ng’ombe huwa na homa kali inayofikia nyuzi joto za sentigresi 40 hadi 41.5
  • Kutokwa machozi na makamasi.
  • Ng’ombe kutokwa na mate mengi mdomoni.
  • Wakati mwingine ng’ombe kuchechemea.
  • Kuwa na vidonda kwenye mdomo na pua.
  • Kuvimba kwa tezi, kiwele, kifua, na miguu.
  • Ng’ombe wenye mimba wanaweza kutupa mimba.
  • Kwa wale wanaokamuliwa hupunguza kiasi cha maziwa na kukonda.

Sampuli ya kupima

Ili kujua kama ni ugonjwa wa mapele ngozi, ni vyema mtaalamu au daktari wa mifugo akachukua sampuli zinazotakiwa kitaalamu (kama vile kukata nundu ama upele mmoja) na kwenda kufanyia vipimo katika maabara. Kumbuka, mapele ya ugonjwa huu kwenye ng’ombe huwa makubwa zaidi tofauti na mapele ya kawaida na huweza kuonekana kama manundu.

Chanjo

Ili kuondokana na ng’ombe kupata ugonjwa huu, ni lazima wafugaji wahakikishe wanawapatia ng’ombe wao chanjo dhidi ya ugonjwa huu mara moja kila mwaka.

Tiba

Ugonjwa huu hauna tiba, isipokuwa ng’ombe wagonjwa wanatakiwa kupatiwa dawa ya vijiuasumu (antibiotics) ili kuzuia maambukizi nyemelezi ya bakteria.

Namna ya kuudhibiti 

  • Wafugaji wanashauriwa kuwa na utaratibu wa kuwaogesha ng’ombe wao kwa kutumia dawa za kuogeshea mifugo.
  • Pale ambapo ugonjwa unatokea, ng’ombe walioathirika na ugonjwa huu watengwe mbali na wale wazima.

Madhara yanayoweza kuletwa na ugonjwa huu ni kama ifuatavyo;

  • Kupungua kwa uzalishaji wa maziwa kutokana na ng’ombe kushindwa kula.
  • Ng’ombe hupunguza uzito kutokana na kukonda.
  • Ngozi ya ng’ombe kuharibika na hivyo kupoteza au kupunguza thamani.
  • Ugonjwa huu usipotibiwa mapema hupelekea mnyama kufa.

 

 

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *