- Mifugo

Fahamu wadudu wasumbufu katika ufugaji wa kuku

Sambaza chapisho hili

Ufugaji wa kuku ni moja ya sekta ambayo imekuwa na faida kwa wafugaji walio wengi, na hata watu ambao wanafanya shughuli nyinginezo, lakini bado hujishughulisha na ufugaji wa kuku.

Pamoja na aina hii ya ufugaji kuwa na mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuwatengenezea wafugaji kipato kikubwa, bado inakumbwa na changamoto mbalimbali.  Mojawapo ya changamoto hizo ni pamoja na uwepo wa wadudu wa aina mbalimbali ambao wamekuwa wakishambulia kuku, na hatimaye kueneza magonjwa ambayo mwisho wake husababisha hasara kwa mfugaji.

Utitiri

Wadudu hawa wana rangi ya kikahawia lakini baada ya kufyonza damu hubadilika rangi na kuwa wekundu.

Wadudu hawa hunyonya damu usiku na wakati wa mchana huku wakijificha katika nyufa za nyumba. Aidha, huzaliana kwa wingi sana wakati wa joto kuliko wakati wa baridi.

Chanzo

  • Uchafu ndani ya mabanda ya kuku.

Dalili za utitiri kwa kuku

  • Kupungua kwa utagaji
  • Kuku kuangaika wakati wa usiku.
  • Ukichunguza kuku usiku utaona wadudu wa kikahawia.
  • Upungufu wa damu kwenye mwili wa kuku .
  • Kuwashwa washwa kwa kuku.

Kudhibiti

  • Ondoa kuku kwenye mabanda yaliyo na wadudu hawa
  • Nyunyizia dawa kuku wote .
  • Safisha mabanda la kuku na kunyunyizia dawa.
  • Zingatia usafi wa mabanda ya kuku,weka ratiba ya usafi ya kila siku katika banda la kuku.

Dawa zinazotumika kuzibiti utitiri

  • Seven dust, Poutry dust, Malathion 2%, Nicotine sulphate.

Viroboto

Wadudu hawa wanaosumbua kuku hupenyeza katika ngozi ya kuku na hutaga mayai na kusababisha madonda kwa kuku. Pia, wadudu hawa hukaa sehemu za nje za kuku kama shingoni, usoni na kwenye kishungi na hata kwenye mashavu.

 

 

 

 

 

 

Chanzo

Uchafu katika mabanda ya kuku na katika mazingira yanayozunguka mabanda ya kuku.

Dalili za kuku mwenye viroboto

  • Kuku kujikuna mara kwa mara.
  • Kuku hugandwa na wadudu hawa kwenye sehemu za macho, mapanga, shingo na hata mashavu.
  • Kupauka maeneo ya kishungi kwa kupungukiwa damu.
  • Kwa kuku anayetaga uweza acha kabisa kutaga kwani wadudu hawa husababisha usumbufu mkubwa kwa kuku.

 

Kudhibiti

  • Usafi wa nje na ndani ya banda.
  • Nyunyiza dawa za kuua wadudu ndani na nje ya mabanda ya kuku. Dawa kama bakiller powder, akheri powder au seven dudu dust zinafaa kutumika kuua wadudu hawa.
  • Wanyunyuzie dawa kuku wote.

 

Tiba

  • Tumia mafuta mazito na kupakaa kwenye sehemu ya kuku iliyoshambuliwa,wafugaji wengine hutumia mafuta ya alizeti au mawese nayo huasidia. Pia, nunua dawa ya iodine tincture na pakaa kwenye vidonda hivyo.

Chawa wa kuku

Huweza kushambulia sehemu ya ngozi, kichwa, shingo na hata mabawa.

Dalili za kuku wenye chawa

  • Utagaji wa mayai hupungua.
  • Kudumaa katika ukuaji.
  • Kuonekana kwa mayai ya chawa kwenye ngozi na manyoya ya kuku.

Kuua chawa

Nyunyiza dawa ya kuua chawa kwa kila siku.

Safisha banda la kuku na nyunyiza dawa ya kuua chawa  kama vile seven au  poutry dust.

Kupe wa kuku

Kupe wa kuku huishi kwenye mabawa ya kuku kwa kipindi kirefu hasa wakati wa joto. Kupe hawa siyo rahisi kuonekana kwenye kuku kwani huuma na kukimbia na kujificha katika nyufa za banda.

Dalili za kupe

  • Upungufu wa damu
  • Kuku kuwa na homa.
  • Uzito hupungua.
  • Utagaji hupungua.
  • Kuonekana kwa mabaka mabaka kwenye sehemu ya ngozi ambayo kuku aliumwa.

 

Kudhibiti

  • Safisha banda.
  • Nyunyiza dawa kama malathion 2% emulsion.
  • Kutoa kuku kwenye banda.

Wadudu wengine

Wadudu kama siafu, nyoka na wanyama kama paka pori ,mbwa wa mtaani, vicheche na nyani hushambulia pia kuku.

Kudhibiti wadudu hawa  

  • Hakikisha hakuna matundu ambayo wadudu na wanyama watatumia kupenya na kuvamia kuku katika mabanda yao.
  • Safisha mazingira ya kuzunguka mabanda ya kuku kwa kuondoa vichaka ili kudhibiti siafu na nyoka.
  • Tumia dawa kama duduoll kuua wadudu kama siafu.

Fuata na tekeleza taratibu hizi kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuku

Taratibu za kuzuia kuenea kwa magonjwa hutekelezwa kwa lengo la kuzuia uingiaji na usambaaji wa vimelea vya ugonjwa ndani na kati ya vijiji, kaya na mashamba.

 

Taratibu hizi ni pamoja na kuweka karantini ambapo magonjwa na vimelea vya ugonjwa huzuiwa kuingia katika eneo fulani, au vimelea huharibiwa na kuzuiwa sehemu moja ili visipenye kuingia maeneo mengine.

 

Hivyo basi, taratibu za kuzuia kuenea kwa magonjwa zina vipengele vikuu

Vitatu ambavyo ni: karantini, kudhibiti njia za usafirishaji na usafi wa maeneo. Mfumo imara ya kuzuia kuenea magonjwa ni muhimu sana ili uweze kuendelea kuwa na kuku wenye afya.

 

Unapotayarisha mfumo wa kuzuia magonjwa katika shamba la kuku, vipengele vitatu vya kuzingatia ni:

  1. Eneo lilipo shamba au banda: Shamba au banda la kuku liwe mbali na mashamba mengine ya ndege na mifugo mingine. Ni vyema banda moja likawa na kuku wa umri mmoja ili kuzuia vimelea vya magonjwa kuendelea kubaki bandani.
  2. Ramani ya shamba au banda: Kujenga uzio ili kuzuia watu wasiohusika kuingia shambani au bandani. Mchoro wa mabanda upunguze pita pita za watu na uwezeshe usafi na upuliziaji wa dawa kufanyika kwa urahisi. Jenga mabanda yenye nyavu ambayo ndege pori na panya hawawezi kuingia.
  3. Taratibu za kuendesha shughuli za shamba: Zuia kuingizwa na kuenezwa kwa magonjwa shambani kwa kudhibiti uingiaji wa watu, vyakula, vifaa, wanyama na magari ndani ya shamba.

 

Hatua za Kuzuia Kuingia na Kuenea kwa Magonjwa Shambani

 

  • Tenganisha ndege kufuatana na aina ya ndege na umri wao.
  • Weka karantini kwa ndege/kuku wapya ili wachunguzwe kwa kipindi kisichopungua wiki mbili kabla ya kuingizwa shambani au bandani.
  • Usiruhusu tabia ya kuchangia vifaa/vyombo kama vile makasha ya mayai, makreti ya kubebea kuku kati ya shamba na shamba, n.k.
  • Wafanyakazi waanze kuwahudumia kuku wenye umri mdogo kabla ya wale wenye umri mkubwa.
  • Usiruhusu watoto kucheza na kuku.
  • Jaribu kuzuia idadi ya wageni wanaoingia shambani/bandani.
  • Weka utaratibu wa kuangamiza mizoga ya kuku.
  • Anzisha mfumo jumuishi ya kudhibiti wadudu/wanyama waharibifu.
  • Panga utaratibu mzuri wa kuwapa kuku huduma ya maji na kufanya usafi.
  • Panga utaratibu mzuri wa kuzoa taka na mizoga ya kuku.
  • Weka utaratibu wa kusafisha banda na kupulizia dawa.
  • Vifaa visafishwe na kuwekwa dawa ya kuua vijidudu kabla ya kuingizwa shambani.
  • Hakikisha magari yanapoingia shambani yanapita katika kidimbwi chenye dawa ya kuua vimelea vya magonjwa.
  • Hakikisha mfanyakazi anabadilisha viatu/mabuti kabla ya kuingia katika kila banda.
  • Weka utaratibu mzuri za kuingia shambani, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usafi wa viatu na mikono; au wageni na wafanyakazi kubadilisha nguo/viatu na kuvaa mabuti.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *