- Kilimo, Mifugo, Mimea, Samaki, Samaki, Usindikaji

Ufugaji mseto wa samaki na mazao mengine

Sambaza chapisho hili

Katika toleo lililopita tuliangalia utangulizi wa mada hii ya ufugaji mseto wa samaki na mazao mengine. Tuliweza kuangazia mambo kadha wa kadha muhimu, na miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na faida za ufugaji huo, pamoja na manufaa  ya ufugaji wa namna hiyo;

Aina ya samaki wanaofaa katika kilimo mseto

Perege na Kambale ni samaki wanaofugwa katika maeneo mabalimbali nchini Tanzania. Perege ndiyo aina ya samaki inayofahamika zaidi kwa wafugaji.

Chakula cha asili cha Perege ni vimelea vya kijani vilivyomo ndani ya maji, lakini ana uwezo wa kula aina nyingi za vyakula ikiwa ni pamoja na pumba za mahindi na mpunga, majani na mabaki ya jikoni.

Vile vile anakua vizuri kama kutakuwa na mbolea za samadi na za chumvi chumvi, na anaweza kuhimili kiasi kidogo cha hewa ya oksijeni.

Madume ya Perege hukua haraka zaidi kuliko majike, na uvunaji unaweza kufanyika baada ya kufikisha uzito wa gramu 250. Kambale hula vyakula vya asili ndani ya maji kama vile wadudu, konokono, vifaranga wa chura na samaki wengine wadogo.

Vile vile anakula vyakula vya ziada kama vile mabaki ya vyakula hasa yenye asili ya nyama. Kambale hutumika kupunguza wingi wa Perege ndani ya bwawa.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba Perege anazaliana kwa wingi kwenye bwawa. Kambale anakua haraka sana kama chakula chenye protini kinapatikana kwa wingi.

Kambale anaweza kuishi kwenye maji yenye hewa kidogo ya oksijeni. Tofauti na Perege, Kambale ana mifupa michache na minofu mingi na ni mtamu hasa anapokaushwa kwa moshi.

Faida za mboga mboga katika ufugaji mseto

(i)   Chanzo cha chakula cha samaki: Mboga mboga hutumika moja kwa moja kama chakula cha samaki kwa kuwa jamii ya samaki wengi wanaofugwa ni wale wanao kula majani kama jamii ya Sato na Perege na hata jamii ya Kambale.

Hivyo mabaki ya mboga mboga kutoka bustani hukatwa katwa vipande vidogo vidogo kwa ajili ya kulisha samaki.

(ii)   Chakula cha mkulima: Hili huwa lengo kuu la kulima mboga mboga kwenye mseto na ufugaji samaki. Chakula jamii ya mimea huwa na kiwango kikubwa cha madini yanayohitajika katika utunzaji wa afya ya mwanadamu.

Mboga mboga hupunguza gharama ya ununuzi wa chakula kwa mkulima kwa kumwezesha mkulima kupata lishe bora kutoka shambani kwake.
(iii)   Chanzo cha fedha: Ufugaji mseto wa samaki na bustani hulenga kuwa kitega uchumi kikubwa kwa wakulima wadogo.

Mavuno ya mazao ya bustani huuzwa kirahisi kwa kuwa yanahitajika kwa wingi na jamii kutokana na umuhimu wake.

Fedha inayopatikana husaidia katika utunzaji wa shamba mseto au kutumika katika mahitaji mengine ndani ya familia ya mfugaji.

(iv)   Mbolea kwenye bwawa la samaki: Mboga mboga hutumika kama mbolea kwenye bwawa la samaki. Mboga mboga huozeshwa kwenye hori ili iwe mboji ambayo hutoa mimea na wadudu wa asili ambao hutumika kama chakula cha samaki. Hii hupunguza gharama za uzalishaji kwenye bwawa la samaki.

Faida za kuku katika ufugaji mseto

(i)   Chanzo cha mbolea: Lengo kuu la ufugaji wa kuku kwenye ufugaji mseto ni urutubishaji wa bwawa la samaki ili kupata chakula cha asili kwa samaki. Kinyesi cha kuku hutumika kama chanzo cha mbolea kwa sababu kina kiasi kikubwa cha urea.

(ii)   Hutoa chakula cha samaki: Tofauti na kuwa chanzo cha rutuba, kinyesi cha kuku huliwa moja kwa moja na samaki.

Hiki huwapa samaki afya nzuri kwani huwa na chembechembe nyingi za urea, ambazo ni sehemu kubwa ya madini ya Nitrojeni na Fosforasi ambayo huhitajika kwa wingi kwenye chakula cha samaki.

(iii) Chanzo cha chakula kwa wafugaji: Pamoja na kuwa na umuhimu wa kiikolojia katika ufugaji mseto, lengo jingine kubwa ni kuwa chanzo cha lishe bora kwa mfugaji kwani huwa na protini ya kutosha ambayo husaidia katika ukuaji wa mwili.
(iv)    Chanzo cha fedha: Kama ilivyo kwa mifugo wengine, mauzo yatokanayo na mazao kama kuku husaidia kama chanzo kikubwa cha fedha kuanzia wafugaji wadogo wadogo hadi wakubwa.

Kuku hufugwa kirahisi ukilinganisha na wanyama wakubwa kama vile ng’ombe, nguruwe, mbuzi na kondoo ambao huhitaji eneo kubwa, rasilimali kubwa, wasimamizi wengi, n.k.

Hivyo ufugaji wa kuku huwa na gharama ndogo kiuendeshaji na huleta faida kubwa.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *