- Mifugo

Ubora wa zizi huinua uzalishaji wa mbuzi na kondoo

Sambaza chapisho hili

Ufugaji wa Mbuzi na kondoo ni wa gharama nafuu sana hasa ukilinganisha na ng’ombe kwani wanyama hawa wana uwezo wa kuishi mahali popote na katika mazingira magumu kama yenye maradhi na ukame.

Wanyama hawa kulingana na umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo huku wakihudumiwa na familia zenye nguvu kazi ndogo na kipato cha chini.

Wanyama hawa ambao hufugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi, sufu na mazao mengine kwa matumizi ya familia na kuongeza kipato, endapo utachukuliwa uzao wa muda mfupi, basi mfugaji anaweza kupata mbuzi au kondoo wengi kwa kipindi kifupi mno.

Kanuni bora za ufugaji wa mbuzi na kondoo

  1. Hakikisha mbuzi au kondoo wanafugwa kwenye banda au zizi bora na imara.
  2. Wanyama hawa wachaguliwe kutokana na sifa za koo au aina pamoja na kuzingatia lengo la uzalishaji (nyama, maziwa au sufu).
  • Ni lazima kuhakikisha wanyama hawa wanapatiwa lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya miili yao.
  1. Mfugaji azingatie mbinu za kudhibiti magonjwa kama inavyoshauriwa na wataalam wa mifugo,
  2. Ni lazima mfugaji ahakikishe anaweka na kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji wa wanyama hawa.
  3. Mfugaji ni lazima azingatie kuzalisha nyama, maziwa au sufu yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.

Zizi au banda la kondoo

Wanyama hawa wanaweza kufugwa katika mifumo miwili tofauti (huria na shadidi) au kwa kutumia mifumo yote miwili.

Katika Mfumo huria, zizi hutumika pale ambapo wanyama hawa huchungwa wakati wa mchana na kurejeshwa zizini wakati wa usiku.

Katika mfumo shadidi, wanyama hawa hufugwa zizini (hawapewi nafasi ya kutoka nje) na hulala humo humo.

Sifa za banda/zizi bora la mbuzi au kondoo

  • Zizi linatakiwa liwe imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari.
  • Zizi linatakiwa liwe lenye kupitisha mwanga, hewa na liwe na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi
  • Zizi linatakiwa kujengwa katika eneo lisiloruhusu maji kutuama na liwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu huku ujenzi ukizingatia mwelekeo wa upepo ili hewa kutoka bandani isiende kwenye makazi ya watu
  • Zizi liwe na sakafu ya kichanja chenye mwinuko wa mita 1 kutoka ardhini (Kwa banda la mbuzi)
  • Zizi liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji na mahali pa kuweka jiwe la chumvichumvi kwa ajili ya wanyama kulamba
  • Zizi liwe na vyumba tofauti kwa ajili ya majike, vitoto, mbuzi au kondoo wanaokua, wanaonenepeshwa na wanaougua

Vifaa vya kujengea na vipimo vya banda

Ni rahisi sana kujenga banda kwa ajili ya mbuzi na kondoo kwani unashauriwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika eneo mfugaji alipo.

Ukubwa wa banda utategemea idadi ya mbuzi au kondoo wanaofugwa humo na ukubwa wa umbile lao.

Vifaa hivyo na maeneo yatakayotumika ni kama ifuatavyo;

  • Paa linatakiwa kujengwa kwa kutumia miti, mbao, na kuezekwa kwa nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati au hata vigae kwa kutegemeana na uwezo wa mfugaji
  • Kuta ni muhimu kujengwa kwa kutumia mabanzi, mbao, nguzo, wavu wa waya, fito na matofali

Kuta hizo ziwe imara na zinazoruhusu hewa na mwanga wa kutosha. Mlango uwe na ukubwa wa sentimita 60 kwa 150

  • Sakafu yaweza kuwa ya udongo au zege

Kama sakafu ni ya kichanja inaweza kujengwa kwa kutumia miti, fito, mianzi, mbao au mabanzi na iweze kuruhusu kinyesi na mkojo kupita.

Chumba cha majike na vitoto kiwe na nafasi ya sentimita 1.25 kati ya papi na papi, fito na fito au mti hadi mti.

Chumba cha mbuzi au kondoo wakubwa iwe sentimita 1.9 kati ya mbao na mbao.

Faida za kujenga zizi bora

  • Zizi lililo imara husaidia kumkinga mbuzi na kondoo dhidi ya wanyama hatari na wezi
  • Zizi lililojengwa mahali pa mwinuko husaidia kutokuruhusu maji kutuama
  • Ukubwa wa zizi utakaozingatia idadi na umri wa mifugo na ambao utaruhusu kutengwa kwa wanyama kulingana na umri wao utasaidia wanyama kupata uhuru na kukua vizuri wakiwa na afya imara
  • Zizi likiwa kubwa litasaidia na kuruhusu usafi kufanyika kwa urahisi
  • Zizi bora husaidia kukinga wanyama hawa dhidi ya magonjwa
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *