- Mifugo

Siku ya tokomeza gugu karoti Arusha (2020)

Sambaza chapisho hili

Athari za gugu karoti na mbinu za kukabiliana nalo

Gugu karoti ambalo kitaalamu linajulikana kama (Parthenium hysterophorus) ni mmea vamizi ambao una athiri binadamu, mazao, wanyama au mifugo pamoja na kuharibu uoto wa asili.

Nchini Tanzania, gugu karoti limegundulika au kuonekana kuwepo tangu mwaka 2010 katika mkoa wa Arusha hasa maeneo ya pembezoni mwa baadhi ya barabara, na baadaye kuanza kuonekana mkoani Kagera (Kyerwa).

Hadi kufikia sasa, mmea huu wa gugu karoti umethibitika kuwepo na kuenea katika mikoa minne ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Kagera.

Juhudi za kutokomeza gugu karoti mkoani Arusha

Kutokana na athari za gugu hili, baadhi ya wadau mkoani Arusha mnamo mwaka 2016 waliamua kuunda kamati ya kutokomeza gugu karoti, na baadaye kushirikisha watu mbalimbali ambao kwapamoja walianzisha siku maalumu ya “Tokomeza gugu karoti”.

Kamati hii ilifanikiwa kutenga siku moja katika kila mwaka ambapo wadau hukusanyika pamoja na kujadili namna ya kutokomeza mmea huu.

Jinsi ya kutokomeza mmea wa gugu karoti

Juhudi za kutokomeza mmea huu ni pamoja na

  • Kutoa elimu sahihi kwa wanajamii katika maeneo mbalimbali ambapo mmea huu umeonekana.
  • Kuung’oa mmea huu na kisha kuchoma moto.

Aidha, kwa ushirikiano wa serikali, mashirika mbalimbali, waandishi wa habari pamoja watu binafsi, kupitia siku hii imesaidia kuongeza uelewa katika jamii. Sasa watu wameanza kufahamu madhara ya gugu karoti na kuendelea kuling’oa katika maeneo yao.

Siku ya kutokomeza gugu karoti mwaka 2020

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya kutokomeza gugu karoti yaliyofanyika ukumbi wa ALMC (Seliani hospital), na kuudhuriwa na wadau mbalimbali,  mgeni rasmi, Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Iddi Kimantha amesema kuwa, athari za gugu karoti zinafahamika na juhudi za kutokomeza zisiposhughulikiwa madhara yataongezeka.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Iddi Kimantha (5 toka kulia kwa waliokaa) akiwa na wadau mbalimbali waliohudhuria siku ya tokomeza gugu karoti mkoani Arusha

Alisema kuwa madhara ya gugu hili ni ya kiafya kwa binadamu, wanyama, mimea na hata uoto wa asili.

Alitaja madhara kwa binadamu kuwa ni muwasho unaoweza kusababisha kujikuna na kupata malengelenge, ugonjwa wa pumu na muwasho wa macho unaosababishwa na vumbi la gugu.

Kwa upande wa wanyama;

  • Mnyama anapokula mmea wa gugu karoti huweza kupasuka na kuvimba midomo.
  • Maziwa yanayotoka kwa ng’ombe aliyekula jani la gugu karoti huwa machungu na yakitumiwa huweza kuleta madhara kwa afya ya mtumiaji.
  • Mnyama akila majani ya gugu karoti hupunguza uzalishaji wa maziwa.
  • Nyama zinazotokana na mnyama aliyekula majani ya gugu karoti hupungua thamani au ubora wake.
  • Vumbi la mmea wa gugu karoti linapogusa mwili wa mnyama humsababishia kuwasha na hatimaye kunyonyoka kwa manyoya.

Kwa upande wa mimea;

  • Mbegu za gugu karoti au majani yenyewe yakiwepo katika eneo linalooteshwa mazao, huzuia mbegu ya mazao husika kuota.
  • Gugu karoti hupunguza upatikanaji wa mavuno ya kutosha hasa kwa mahindi na mtama.
  • Majani ya gugu karoti huzuia mimea kuendeleza ukuaji wake.
  • Vumbi la gugu karoti huzuia mimea ya matunda kuweka matunda.

Aidha Bw. Kimantha ameongeza kuwa, gugu karoti hubadili kabisa uoto wa asili na kuua malisho hivyo wilaya zote zinazotegemea mifugo kwaajili ya uchumi zitakuwa kwenye athari kubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Iddi Kimantha akitoa mkono wa pongezi kwa mjume wa kamati Bi. Flora Laanyuni toka Mkulima Mbunifu

Nini cha kufanya

Bw. Kimantha amesema kuwa, ili kuweza kulitokomeza gugu hili, viongozi wote wa mkoa kuanzia vijijini wawe katika mstari wa mbele kuhamasisha jamii juu ya madhara, namna ya kulitokomeza na kuonyesha mfano wa namna ya kuliondoa.

Halmashauri zote za wilaya kushirikiana na taasisi za kitaalamu pamoja na wanajamii kuhakikisha wanakuwa pamoja katika utokomezaji wa gugu karoti.

Vijiji vyote katika mkoa kuweka siku moja maalumu kwa kila wiki kwa ajili ya wanajamii kung’oa na kuchoma gugu hili.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Siku ya tokomeza gugu karoti Arusha (2020)

  1. Nawapongeza kwa jitihada za kutoa elimu hususani katika nyanja ya kilimo hili tuweze kukuza uchumi was nchi na maendeleo kwa ujumla
    Ningependa mzidi kuendelea kutoa makala mbalimbali za kilimo na mifugo kwa kupitia wakulima mbalimbali na vikundi vya wajasiriamali

    1. Habari. Karibu sana Mkulima Mbunifu.
      Kama una vikundi unayofahamu zaidi unaweza ukatupatia taarifa za kila kikundi kuanzia jina la mwenyekiti/kiongozi/katibu, namba za simu, jina la kikundi, idadi ya wanakikundi pamoja na sanduku la posta ili tuweze kuwatumia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *