- Mifugo

Njia bora ya utunzaji wa  ng’ombe wa maziwa

Sambaza chapisho hili

Nina mradi mdogo wa ng’ombe wa maziwa, ninahitaji kuboresha, naomba ushauri namna ya kuwa na banda bora na matunzo yake kwa ajili ya ng’ombe wangu

Ng’ombe wa maziwa wanaweza kuzalisha vizuri kutokana na kuwa na mazingira mazuri, banda zuri na lishe. Zingatia usafi na uhakikishe kuwa ng’ombe wana nafasi ya kutosha.

Nafasi: Kila ng’ombe mkubwa anahitaji walau skwea mita 8, mbali na eneo la kupumzika. Njia rahisi ni kutenga eneo hilo mbele ya banda.

  • Ng’ombe wote ni lazima wapate kivuli na malazi mazuri. Ni lazima banda liwe na kina cha kutosha mtu kusimama humo ndani na kufanya shughuli zinazohitajika.
  • Sakafu iwe ya sementi au iliyotengenezwa kwa udongo mgumu au wa mfinyanzi. Ni vizuri kutengeneza sakafu ya simenti kwa kuwa ni rahisi kusafisha.
  • Sakafu isiwe nyororo sana, vinginevyo, ng’ombe watateleza.
  • Sakafu iwe na mwinuko kidogo utakaowezesha mkojo na maji kutiririka kutoka nje ya banda kupitia sehemu ya kutolea kinyesi nje ya banda.
  • Kila ng’ombe ni lazima awe na mahali pake pa kupumzikia, ambapo anaweza kulala.

Maji: Banda ni lazima lijengwe sehemu ambayo ni rahisi maji safi kupatikana. Ng’ombe mmoja anahitaji maji kati ya lita 50 na 180 kwa siku.

Eneo la kukamulia: Tenga eneo la kukamulia na liwe na kihondi ili ng’ombe aweze kulishwa wakati wa kukamua.

Utunzaji:

  • Ni lazima kuhakikisha banda ni safi wakati wote. Ni muhimu banda lisafishwe kila siku kuondoa kinyesi na mkojo, angalau mara moja kwa siku.
  • Matandiko yaliyomo bandani ni lazima yabadilishwe mara moja yanapolowana na kuchafuka. Hii ni muhimu kwa ajili ya kufanya mifugo kuwa wasafi muda wote jambo ambalo litasaidia kuwakinga dhidi ya maambukizi ya aina mbalimbali kama vile ugonjwa miguu na midomo.
  • Safisha kihondi kila mara kabla ya kuongezea chakula kingine
  • Chombo au sehemu ya kunyweshea pia inafaa kusafishwa kwa uangalifu mara kwa mara.

Dang’a haina madhara kwa matumizi ya binadamu

Mimi ni msomaji wa jarida la Mkulima Mbunifu, nataka kufahamu endapo dang’a ina madhara yoyote endapo itatumiwa na binadamu?

Danga ni maziwa ya mwanzo ambayo ngombe, mbuzi, kondoo  hutoa mara baada ya kuzaa, na maziwa haya huwa mfugaji hayatumii kwani ni kwaajili ya ndama pekee.

Kwa kipindi cha siku ya kwanza mpaka ya nne, dang’a hupewa ndama ilia pate nguvu kwa kuwa huwa na virutubisho vingi tofauti na maziwa ya kawaida.

Maziwa haya  ni mazito sana na yana rangi ya njano.

Endapo mfugaji au mtu yeyote ataamua kutumia danga (maziwa ya awali) hayana madhara yoyote.

Kuna faida gani ndama kutumia dang’a!

  • Dang’a husafisha matumbo ya ndama. Ili ndama apate kinyesi chake cha kwanza, ni lazima apate dang’a ya kutosha, jambo litakalosaidia kusafisha tumbo la ndama.
  • Maziwa haya ya awali yana virutubisho vingi zaidi kuliko maziwa ya kawaida. Virutubisho hivyo ni pamoja na vitamini A, C ,D na E.
  • Dang’a huwa na chumvi nyingi na protini kwa wingi zaidi kuliko maziwa ya kawaida.
  • Dang’a humpa ndama kinga. Maziwa haya humsaidia ndama kupata kinga ya mwili, yaani kinga ya mama anaipata kupitia maziwa haya ambayo humsaidia kujikinga na magonjwa mbali mbali.

Muhimu: Ndama asipopata maziwa haya hudhoofu na pia hushambuliwa na magonjwa mbalimbali kwa haraka zaidi.

Maji ni muhimu sana kwa ng’ombe wa maziwa

Ni kwa nini ng’ombe wa mawazi wanatakiwa kupata kiwango kikubwa cha maji kuliko wanyama wengine?

Maziwa yana kiasi cha asilimia tisini ya maji. Hii inamaanisha kuwa, kiasi kikubwa sana cha maji kinahitajika kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa. Wafugaji wanaweza kusahau jambo hili hasa katika ukanda ambao maji ni ya shida.

Mahitaji ya maji yanalingana kabisa na kiwango cha uzalishaji wa maziwa. Kwa mfano, ng’ombe asiyekamuliwa anahitaji kiasi cha lita 30-50 za maji kulingana na umbile lake, wakati ng’ombe anaekamuliwa anahitaji nyongeza ya kiasi cha lita moja na nusu kwa kila lita moja ya maziwa anayozalisha.

Hii inamaanisha kuwa ng’ombe mwenye umbile la kati,  ambae anazalisha lita 20 za maziwa, anahitaji lita 70 za maji kila siku. Hii ikiwa na maana kwamba,  anahitaji lita 40 kwa ajili ya mwili wake, na lita 30 kwa ajili ya kuzalisha lita 20 za maziwa.

Muhimu: Endapo ng’ombe anaekamuliwa hatapata maji ya kutosha, kiwango cha maziwa kitashuka na kusababisha hasara kwa mfugaji.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

10 maoni juu ya “Njia bora ya utunzaji wa  ng’ombe wa maziwa

    1. Noel Alphayo: You are most welcome. With this information, you can improve your dairy farming. Unaboresha na kujiongezea kipato. Asante

      1. Habari za asubui wadau ni mimi mfugaji naomba kuuliza je ni chumvi Gani inamfaa ngombe wa maziwa maana soko lime sheeni bidhaa bandia na kutokea kwa matokeo duni kwa ngombe alfu je tumpe kia si Gani kwasiku AM….PM naombeni msaada please
        Noel alphayo kutoka Arusha. Sanawari

  1. Mimi nahitaji kununua ngombe wa maziwa kutoka SUA jee wanapatikana na kuna utaratibu gani wa kuweza kuwapata? asante

    1. Habari

      Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za MkM.
      Kuhusu kununua ng’ombe kutoka SUA tafadhali unaweza wasiliana nao moja kwa moja kupitia tovuti yao ya ufugaji.co.tz

      Karibu sana Mkulima Mbunifu

  2. Tafadhali Nina ngo’mbe mtamba aina ya fresian naomba mnifundishe namna ya kupatia chakula chenye mchanganyiko wenye virutibisho vyote ili apate joto kwa haraka

    1. Habari,
      Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa swali lako. Tunaandaa mchoro wa banda la ng’ombe likiwa na vifaa na vipimo sahihi hivyo tukishamaliza kuchapisha utapata kuona.

  3. Mungu azidi kuwapa maisha marefu ili mzidi kusaidia jamii ya ufugaji tuweze kuwa wafugaji wa kisasa zaidi

    1. Asante sana na tafadhali endelea kufuatilia na kusoma makala zetu kila zinapotoka

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *