- Kuku, Mifugo

Namna ya kufanya candling (uchunguzi wa mayai yanayototoleshwa)

Sambaza chapisho hili

Makala hii ni muendelezo wa makala iliyopita ambapo ilijikita katika kuelezea namna ya kutotolesha mayai kwa njia ya asili na pia kwa njia ya mashine (Incubator). Katika muendelezo huu tutaangalia kwa undani jinsi ya kuchunguza yai kwa kutumia mwanga.

Candling ni njia ya kuchunguza mayai kwa kutumia mwanga aidha wa mshumaa au tochi. Tochi ambayo ni kifaa cha kisasa ni nzuri zaidi kwani mionzi yake inakusanywa pamoja kumulika eneo moja na inapenya kirahisi kuona ndani ya yai wakati mwanga wa tochi unatawanyika.

Candling inatakiwa ifanyike kila siku hasa kwa wanaotumia mashine ili kubaini kama kuna tatizo lolote linalotokana na mashine na kulirekebisha. Chunguza yai moja baada ya jingine na hakikisha yai halikai nje ya incubeta zaidi ya nusu saa.

Hatua za kufanya candling

Hatua ya 1: Andaa eneo la giza kama unafanya candling wakati wa mchana hasa kwa utotoleshaji wa asili ukitegea kuku akiwa ametoka kwenda kula. Tumia boksi au kitu chochote kutengeneza giza. Kwa utotoleshaji wa mashine candling ni vizuri ikafanyika wakati wa usiku ambapo taa zitazimwa kuruhusu giza kuwepo.

Hatua ya 2: Chukua yai moja moja kwa uangalifu kutoka kwenye kiota au mashine na liweke upande mkubwa umulikwe na mwanga. Yaani upande mdogo uwe juu na mkubwa chini unakotoka mwanga. Lishike yai upande ule mdogo kwa kidole gumba na kidole cha kati.

Hatua ya 3: Taratibu zungusha yai huku ukiliinamisha kidogo upande mmoja hadi pale unapoona vizuri.

Hatua ya 4: Tazama mayai kama yananyufa na mipasuko ili yaondolewe na weka alama eneo la hewa (uwazi upande ule mkubwa) ukitumia penseli zungusha mstari eneo hilo ili ikusaidie kulinganisha ukubwa kadiri siku zinavyoenda.

Hatua ya 5: Yape namba mayai kwa kutumia penseli tu wala si peni maana wino unaweza kupenya na kudhuru yai. Nayo hii inafanyika mwanzoni.

Hatua ya 6: Anza kufanya candling kila siku kuona maendeleo ya mayai. Toa yai na kurudisha kwenye mashine au kiota kwa umakini ili usivunje.

Kumbuka: Hakikisha mikono yako ni misafi wakati wa candling. Andika matokeo ya candling kwa kila yai kwenye daftari la kumbukumbu.

Muhimu: Unaweza kufanya candling kila siku tangu siku ya 1 hadi 16 au 17. Wengine hufanya siku ya 1, 7, 14 na 16.

Nini unapaswa kuona kwa siku unapofanya candling

Siku ya 1: Huwezi kuona chochote, japo candling siku ya kwanza ni muhimu ili kubaini kuwa mayai yote yanayowekwa kwenye incubator ni mazima, hayana mipasuko.

Mipasukuko itaruhusu bakteria lakini pia kifaranga hakitatengenezwa, hivyo yasitumike.

Siku ya 4: Hapa utaona mishipa ya damu ikisambaa kwenye yai na itaonekana kama nywele. Kama hujaona chochote siku hii subiri siku ya saba kuna mayai mengine huchelewa kidogo.

Siku ya 7: Siku hii unatakiwa kuona mishipa ya damu vizuri na ule upande mkubwa utaanza kuona eneo la uwazi la hewa likijitokeza. Hewa hii itatumiwa na kifaranga.

Siku ya 10: Hapa utaanza kuona kifaranga na kwa kiasi kinacheza cheza. Eneo la hewa sasa limetanuka na kuwa kubwa unaliona vizuri. Utaona pia kidoti cheusi kinachoonekana vizuri ambalo ni jicho la kifaranga. Hakikisha kufikia siku hii uwe umechunguza mayai yote.

Siku ya 17: Kufikia siku hii kila kitu huonekana kusimama na hata hupelekea wafugaji wengi kuogopa wakidhani Vifaranga vimekufa kwasababu hawaoni chochote (giza tupu). Lakini hali hii ni ya kawaida kwasababu kifaranga kimejaa karibu yai lote na kifaranga sasa kinaelekea kuanguliwa. Usijaribu kuchezesha yai sana wakati huu kwani kifaranga kinajiandaa kutoka.

Siku ya 18: Usiendelee na candling siku hii. Sasa ni wakati wa kuacha uchunguzi na tamaa ya kujua nini kinaendelea kwenye mayai kwani vifaranga wako wataanza kutotolewa muda wowote. Ni muhimu sana wakati huu kutokufungua mashine yako tena kwani joto na unyevu vinapaswa visishuke ndani ya.

Siku ya 21: Hii ni siku ya kuanguliwa vifaranga. Hapa kifaranga kwa kutumia mdomo wake hugongagonga yai ili kitoke. Hapa kuna maajabu hutokea, yai hutembea kwasababu ya kugongwagongwa na kifaranga kilichopo ndani. Kunakuwa na kelele za kugonga gamba la yai na wakati kifaranga kikijaribu kutoka kwenye yai. Baada ya jitihada za kutoka mwisho kifaranga hufanikiwa kutoka kikiwa kibichi na kimechoka.

Kwa maelezo zaidi waasiliana na Augustino Chengula, Mtaalamu wa mifugo chuo kikuu cha kilimo Sokoine (SUA) kwa simu namba: 0676605098

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *